Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukurasa wa CHAN 2024 unapofunguliwa

CHAN Pict

Muktasari:

  • Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Veron Mosengo-Omba, alipozungumza namna ambavyo maandalizi na utayari wa kuanza kwa michuano ya CHAN 2024 itakayofanyika kuanzia Agosti 2 hadi 30 mwaka huu na Tanzania ni nchi mwenyeji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

SASA zimesalia wiki mbili tu kuandika sura mpya katika soka la Afrika. CHAN 2024 ni zaidi ya mashindano, ni kauli yenye nguvu ya ubora wa Afrika, umoja na imani katika vipaji vya ndani. Afrika Mashariki iko tayari kulikaribisha bara kuwa pamoja.”

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Veron Mosengo-Omba, alipozungumza namna ambavyo maandalizi na utayari wa kuanza kwa michuano ya CHAN 2024 itakayofanyika kuanzia Agosti 2 hadi 30 mwaka huu na Tanzania ni nchi mwenyeji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Tanzania imepewa heshima ya kufungua mashindano haya ambayo kwa mara ya kwanza nchi tatu zinashiriki kuyaandaa kwani haikuwa kutokea tangu kuanza kwake mwaka 2009. Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam, ndiyo utatumika kwa mechi ya ufunguzi.

Uwanja huu ni mojawapo ya viwanja vya kisasa na vya kihistoria Afrika. Utatumika kama moja ya viwanja vya fainali za mashindano ya CHAN 2024. Umeandaliwa kikamilifu kuwa mwenyeji wa mechi ya ufunguzi itakayopigwa Agosti 2, wakati Tanzania wakiikaribisha Burkina Faso. Pia uwanja huo utatumika kwa mechi za Kundi B lenye timu za Tanzania, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

CHA 04

Uwezo wa mashabiki

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, maboresho yaliyofanyika ya ufungaji wa viti ikiwa ni sehemu ya programu ya mkandarasi, vimeagizwa viti 62,000 na kuwa uwanja mkubwa zaidi kwenye michuano hii mwaka huu. Awali uwanja huo ulikuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki wapatao 60,000. Maboresho hayo yanaufanya uwanja huo kuwa kati ya viwanja vikubwa zaidi Afrika Mashariki.

Uwezo huu mkubwa pia huongeza faida kiuchumi na kijamii wakati wa mashindano, kwa kuwa unahimiza mahudhurio makubwa kutoka kwa mashabiki wa ndani na wageni kutoka nje ya nchi. Aidha, miundombinu ya uwanja huu imezingatia watu wa aina zote.

CHA 01

Teknolojia ya kisasa

Katika maandalizi ya michuano ya CHAN 2024, Uwanja wa Benjamin Mkapa umeboreshwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuendana na viwango vya kimataifa. Miongoni mwa vifaa vya kisasa vilivyopo ni pamoja na skrini kubwa ya LED inayoonesha matukio ya moja kwa moja ya mchezo, matangazo na taarifa nyingine muhimu kwa mashabiki waliopo uwanjani.

Aidha, uwanja huu umefungwa taa zenye mwanga wa kisasa ambazo huruhusu mechi kuchezwa kwa ubora mkubwa hata wakati wa usiku. Taa hizi zinakidhi viwango vya CAF na FIFA kwa matumizi ya michezo ya kimataifa.

Pia uwanja umeunganishwa na mfumo wa ufuatiliaji wa usalama kwa kamera (CCTV) unaosaidia kudhibiti na kusimamia hali ya usalama kwa mashabiki, wachezaji, na wahudumu. Mfumo huu umeunganishwa na kituo cha uangalizi (control room) ambacho huwezesha mawasiliano ya haraka na vyombo vya ulinzi pale panapotokea hitilafu yoyote.

Mbali na hayo, eneo la kukaa waandishi wa habari na chumba cha mikutano kuna maboresho makubwa yanayomuwezesha mwandishi wa habari kufanya kazi yake akiwa kwenye utulivu wa hali ya juu. Maboresho hayo yamezingatia uwepo wa internet na sehemu za kuchajia vifaa vinavyotumia umeme.

CHA 02

Historia ya uwanja

Uwanja wa Benjamin Mkapa ulianza kutumika rasmi mwaka 2007 baada ya matengenezo yake kukamilika kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China, kama sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu ya michezo nchini huku ukiwa na nyasi asili. Tangu kukamilika kwake, umekuwa ni sehemu ya historia ya michezo nchini Tanzania, ukihusishwa moja kwa moja na mechi kubwa za kitaifa na kimataifa.

Uwanja huu umekuwa ukitumiwa si tu na timu za Tanzania, bali hata timu kutoka mataifa mbalimbali zinazokuja kuomba kwa ajili ya mechi za kimashindano.

Kabla ya kufanyiwa maboresho, Burundi iliwahi kuutumia uwanja huo kwa mechi mbili za nyumbani wakati wa kufuzu michuano ya Afcon 2023 ilipocheza dhidi ya Cameroon na Namimbia, pia klabu mbalimbali za nje ya Tanzania zimewahi kuutumia kwa mechi za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Mwaka 2019, uwanja huo ulitumika kwa mechi za AFCON U17 na mchezo wa fainali uliopigwa hapo Cameroon U17 iliichapa Guinea U17 kwa penalti 5-3.

Oktoba 20, 2023, tukio la kihistoria lilifanyika uwanjani hapo ikiwa ni ufunguzi wa mashindano mapya ya African Football League ambapo Simba ilicheza dhidi ya Al Ahly kutoka Misri.

Mara ya mwisho uwanja huu umetumika kwa mechi ya Dabi ya Kariakoo, Juni 25 mwaka huu Yanga ilipoifunga Simba mabao 2-0.

Kupitia matukio haya, uwanja huu umejipatia hadhi ya kimataifa na heshima kama moja ya maeneo bora ya michezo Afrika Mashariki na sasa unajiandaa kuandika historia mpya kupitia michuano ya CHAN, huku pia mwaka 2027 utatumika kwa michuano ya AFCON.

CHA 03

Mahali uliopo

Uwanja huu unapatikana Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, ambao ni mji mkubwa na wa kibiashara wa Tanzania. Mahali hapa ni rahisi kufikika kwa usafiri wa barabara kutoka maeneo mbalimbali ya jiji, pia uko karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Umbali kutoka uwanja wa ndege hadi Benjamin Mkapa ni mwendo wa takribani dakika 22 kwa usafiri wa gari na unapitia Barabara ya Nyerere, ukifika Tazara kwenye makutano ya Barabara ya Nyerere na Nelson Mandela, unakata kulia kuifuata Barabara ya Nelson Mandela ambayo inakufikisha hadi uwanjani ikiwa ni takribani kilomita 11.1.

Huduma za kijamii kama hoteli, vituo vya afya na vituo vya polisi vipo karibu, hivyo kuufanya kuwa eneo salama na lenye urahisi wa huduma muhimu wakati wa mashindano.


Usalama na huduma mbalimbali

Uwanja wa Mkapa umeweka kipaumbele kikubwa katika eneo la usalama kuhakikisha mashabiki, wachezaji na maofisa wa michezo wapo katika mazingira salama wakati wote wa michuano. Mbali na kamera za usalama, uwanja una lango maalum la ukaguzi wa mashabiki kabla ya kuingia.

Kwa upande wa huduma kwa mashabiki, pembezoni mwa uwanja kuna maeneo ya huduma kama vile migahawa midogo, vibanda vya kuuza bidhaa mbalimbali, maeneo ya kupumzika, huku ndani ukiwa ni vyoo safi vinavyozingatia usafi na afya ya watumiaji.

Aidha, kuna vyumba vya kubadilishia nguo vya kisasa kwa ajili ya wachezaji na waamuzi, vilivyo na vifaa vyote muhimu ikiwa ni pamoja na bafu, sehemu za tiba ya dharura, na sehemu ya kujipasha moto.

Zaidi ya hayo, katika maandalizi ya CHAN, uwanja umeboreshwa zaidi kwa kuweka maeneo ya kusaidia huduma ya kwanza kwa mashabiki, zikiwemo timu za matibabu zitakazokuwa tayari kushughulikia hali za dharura.

Kupitia mchanganyiko wa teknolojia ya kisasa, historia ya kuvutia, uwezo mkubwa wa mashabiki, na huduma bora, uwanja huu uko tayari kwa mechi ya ufunguzi wa michuano ya CHAN kati ya Tanzania na Burkina Faso.