Uholanzi mastaa kibao, ndo kwanza wanasaka taji la kwanza World Cup
Muktasari:
- Mwaka 2026, Oranje wanarudi tena kwenye michuano hiyo mikubwa zaidi duniani wakiwa na matumaini mapya, kocha mwenye uzoefu mkubwa, kizazi kipya cha mastaa na kiu ya kuandika historia mpya.
AMSTERDAM, UHOLANZI: KWA zaidi ya nusu karne sasa, timu ya taifa ya Uholanzi imeendelea kubeba hadhi ya kuwa moja ya timu bora zaidi kuwahi kucheza soka duniani bila kunyanyua Kombe la Dunia.
Pamoja na historia yao kubwa huku kikosi chao kikiundwa na mastaa wengi wakubwa barani Ulaya kwa nyakati tofauti, bado kuna jambo moja ambalo limeendelea kuwatesa mashabiki wa taifa hilo ambalo ni kukosa taji la dunia.
Mwaka 2026, Oranje wanarudi tena kwenye michuano hiyo mikubwa zaidi duniani wakiwa na matumaini mapya, kocha mwenye uzoefu mkubwa, kizazi kipya cha mastaa na kiu ya kuandika historia mpya.
Kwa taifa ambalo limewahi kufika fainali mara tatu lakini likaambulia maumivu, safari ya kuelekea Marekani, Canada na Mexico siyo ya kawaida. Ni safari ya kufufua ndoto ambazo zimekuwa zikisubiriwa kwa miaka mingi.
TIMU INAYOHESHIMIWA DUNIANI
Katika historia ya soka, si mataifa mengi yanaweza kujivunia ushawishi mkubwa wa kimfumo kama Uholanzi. Taifa hilo limekuwa moja ya nchi zilizobadilisha kabisa namna soka linavyochezwa. Kutoka mfumo wa ‘Total Football’ wa miaka ya 1970 hadi kizazi cha sasa chenye kasi, ubunifu na nidhamu ya kiuchezaji, Oranje wameendelea kuwa timu inayotazamwa kwa jicho la tofauti.
Cha kushangaza zaidi ni kwamba Uholanzi si taifa lenye idadi kubwa ya watu kama Brazil, Argentina au Ujerumani. Wakiwa na watu wasiozidi 18 milioni, wameweza kuzalisha vipaji vikubwa vilivyotikisa dunia.
Majina kama Johan Cruyff, Marco van Basten, Ruud Gullit, Dennis Bergkamp, Wesley Sneijder, Robin van Persie na Virgil van Dijk yamekuwa sehemu ya historia kubwa ya soka la dunia. Lakini licha ya majina hayo yote makubwa, Kombe la Dunia limeendelea kuwa ndoto ambayo bado haijatimia.
WALIVYOFUZU KOMBE LA DUNIA 2026
Uholanzi waliingia kwenye kampeni ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 wakijua wazi kuwa mashabiki wao walihitaji kuona timu yenye ubora na uwezo wa kurejesha matumaini baada ya kuishia robo fainali mwaka 2022 nchini Qatar.
Katika kundi lao la kufuzu, Oranje walionyesha kiwango bora tangu mwanzo hadi mwisho. Walimaliza vinara wa Kundi G bila kupoteza hata mchezo mmoja. Walicheza mechi nane, wakashinda sita na kutoka sare mbili dhidi ya Poland pekee. Katika michezo hiyo walifunga mabao 27 huku wakiruhusu manne tu.
Mechi ya mwisho dhidi ya Lithuania ndiyo iliyohitimisha rasmi safari yao ya kufuzu baada ya ushindi wa mabao 4-0. Kipindi chote cha mechi za kufuzu, Uholanzi walionekana kuwa timu yenye uwiano mzuri kati ya ushambuliaji na ulinzi. Walicheza soka la kushambulia lakini pia walionyesha nidhamu kubwa ya kiulinzi, jambo ambalo limekuwa likisisitizwa sana na kocha Ronald Koeman.
KOEMAN NA MISSION YA HISTORIA
Kocha Ronald Koeman si jina geni katika soka la Uholanzi. Mbali na kuwa mmoja wa makocha wenye uzoefu mkubwa Ulaya pia ni sehemu ya historia ya taifa hilo akiwa mchezaji.
Koeman alicheza Kombe la Dunia mwaka 1990 na 1994 akiwa beki mwenye uwezo mkubwa wa kupiga mipira ya adhabu na penalti. Baadaye akaingia kwenye ukocha na kufundisha klabu kubwa kama Barcelona, Ajax, PSV Eindhoven, Benfica na Everton. Alirejea kuinoa Oranje mwaka 2023 baada ya Louis van Gaal kustaafu kufuatia Kombe la Dunia la Qatar. Kwa Koeman, kazi yake kubwa siyo tu kuijenga timu nzuri, bali kuivusha Uholanzi kutoka kwenye historia ya ‘karibu’ hadi kuwa mabingwa wa dunia.
Katika moja ya mahojiano yake ya hivi karibuni, Koeman alisema anaamini Uholanzi wana uwezo wa kushindana na taifa lolote duniani. Kauli hiyo imeongeza matumaini kwa mashabiki wa Oranje ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiamini timu yao imekuwa ikipewa heshima ndogo kuliko inavyostahili.
KUNDI GUMU LA 2026
Katika Kombe la Dunia 2026, Uholanzi watakuwa kwenye kundi lenye ushindani mkubwa pamoja na Japan, Sweden na Tunisia.
Ratiba yao itaanza kwa mchezo dhidi ya Japan mjini Dallas kabla ya kucheza dhidi ya Sweden huko Houston na kuhitimisha hatua ya makundi dhidi ya Tunisia katika Uwanja wa Kansas City.
Ingawa wengi wanaiona Oranje kama timu yenye nafasi kubwa ya kufuzu hatua ya mtoano, kundi hilo linaonekana kuwa moja ya makundi yenye ushindani mkubwa kutokana na ubora wa Japan pamoja na uzoefu wa Sweden katika michuano mikubwa. Hata hivyo, Uholanzi wanaonekana kuingia kwenye mashindano hayo wakiwa na faida ya uzoefu, ubora wa kikosi pamoja na mfumo wao wa kiuchezaji.
HISTORIA YA MAUMIVU YA FAINALI
Hakuna taifa ambalo limewahi kuumizwa na fainali za Kombe la Dunia kama Uholanzi.
Mwaka 1974, Oranje waliingia fainali dhidi ya Ujerumani Magharibi wakiwa timu iliyokuwa ikicheza soka bora zaidi duniani. Wakiwa chini ya Johan Cruyff, walikuwa wameibadili kabisa dunia ya soka kupitia mfumo wa ‘Total Football’. Walitangulia kufunga mapema lakini wakapoteza mchezo huo kwa mabao 2-1.
Miaka minne baadaye, walifika tena fainali nchini Argentina lakini safari hii bila Johan Cruyff. Argentina waliwashinda mabao 3-1 baada ya muda wa nyongeza mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.
Mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, Oranje walipata nafasi nyingine ya kuandika historia. Kikosi kilichoongozwa na Wesley Sneijder, Arjen Robben na Robin van Persie kilifika fainali dhidi ya Hispania. Lakini kama ilivyokuwa mara mbili zilizopita, ndoto zao zilivunjika dakika za mwisho baada ya Andres Iniesta kufunga bao lililoipa Hispania ushindi wa 1-0. Mpaka leo, mashabiki wengi wa Oranje bado wanaamini hiyo ndiyo fainali iliyokuwa karibu zaidi kwao kushinda Kombe la Dunia.
KIVUMBI CHA QATAR 2022
Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar lilionyesha kuwa Uholanzi bado ni moja ya mataifa yenye uwezo mkubwa wa kushindana kwenye kiwango cha juu. Walimaliza vinara wa kundi lao lililokuwa na Senegal, Ecuador na Qatar kabla ya kuiondoa Marekani hatua ya 16 bora.
Lakini robo fainali dhidi ya Argentina ndiyo iligeuka kuwa moja ya mechi bora zaidi za mashindano hayo.
Wakiwa nyuma kwa mabao 2-0, Oranje walionekana wamekata tamaa. Lakini mshambuliaji Wout Weghorst aliingia na kubadilisha kila kitu.
Alifunga bao la kwanza kabla ya kufunga tena dakika za mwisho kupitia mpira wa adhabu uliochezwa kwa ujanja mkubwa na kupeleka mchezo muda wa nyongeza. Katika mikwaju ya penalti, Argentina walishinda 4-3 na kusonga mbele hadi kutwaa ubingwa wa dunia.
Licha ya kuondolewa, Uholanzi walionyesha moyo mkubwa wa kupambana na kuacha ujumbe kwamba bado ni timu ya kuogopwa duniani.
JOHAN CRUYFF NA URITHI WAKE
Ukizungumza historia ya Uholanzi lazima umtaje staa wa nchi, Johan Cruyff.
Huyu siyo tu gwiji wa Uholanzi bali ni mmoja wa watu waliobadilisha kabisa mchezo wa soka duniani.
Cruyff alikuwa moyo wa mfumo wa ‘Total Football’, mfumo ulioruhusu kila mchezaji kubadilika nafasi kwa uhuru bila kupoteza umoja wa timu.
Katika Kombe la Dunia 1974, Cruyff alitengeneza moja ya matukio maarufu zaidi duniani yaliyokuja kuitwa ‘Cruyff Turn’.
Mpaka leo, mzunguko huo wa kiufundi unaendelea kufundishwa kwenye akademi mbalimbali duniani.
Urithi wa Cruyff haukuishia akiwa mchezaji pekee. Mfumo wake wa soka uliendelea kuathiri klabu kama Barcelona na hata timu nyingi duniani.
WACHEZAJI WENYE HISTORIA KUBWA
Katika historia ya Kombe la Dunia, Johnny Rep ndiye mfungaji bora wa Oranje akiwa na mabao saba. Mabao yake yaliisaidia Uholanzi kufika fainali mwaka 1974 na 1978.
Kwa upande wa kucheza mechi nyingi zaidi, Wesley Sneijder na Robin van Persie wanashikilia rekodi hiyo kwa kucheza michezo 17 kila mmoja.
Dennis Bergkamp naye ameendelea kukumbukwa kutokana na bao lake la ajabu dhidi ya Argentina mwaka 1998 ambalo wengi hulitaja kama moja ya mabao bora zaidi katika historia ya Kombe la Dunia.
Robin van Persie naye aliandika historia mwaka 2014 kwa bao lake la kichwa dhidi ya Hispania lililoshangaza wengi.
UBORA KIZAZI CHA SASA
Kuelekea Kombe la Dunia 2026, Uholanzi wana kizazi kipya chenye uwezo mkubwa.
Virgil van Dijk anaendelea kuwa kiongozi mkubwa wa safu ya ulinzi huku Memphis Depay akiwa tegemeo kubwa katika ushambuliaji. Hata hivyo, Oranje wamekuwa wakikumbwa na wasiwasi wa majeraha kwa baadhi ya mastaa wao akiwemo Jurrien Timber.
Koeman pia amekuwa akitegemea vijana wenye kasi na uwezo mkubwa wa kucheza soka la kisasa. Mfumo wa Oranje kwa sasa unaonekana kuwa wa kasi zaidi, wenye presha kubwa na matumizi mazuri ya mipira ya pembeni.
Hilo ndilo linalowafanya wengi kuamini kuwa wanaweza kwenda mbali katika mashindano hayo.
JE, MWAKA 2026 NI WA ORANJE?
Kwa miaka mingi, Uholanzi wamekuwa timu inayopendwa duniani kutokana na aina yao ya soka. Lakini sasa mashabiki wao hawataki tena sifa za kucheza vizuri pekee. Wanataka ubingwa.
Kombe la Dunia 2026 linaweza kuwa nafasi nyingine kubwa kwa taifa hilo kuondoa laana ya kushindwa fainali.
Wana kocha mwenye uzoefu, kikosi chenye ubora, historia kubwa na mfumo wa uchezaji unaoweza kushindana na taifa lolote duniani.
Lakini pia wana kitu kingine muhimu zaidi njaa ya mafanikio.