Lionel Messi ashusha presha Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Nyota huyo wa Inter Miami aliwatia hofu mashabiki juzi Jumapili, Mei 24, 2026 baada ya kuondoka uwanjani akichechemea kutokana na maumivu ya misuli ya paja, wakati wa ushindi wa Inter Miami wa mabao 6-4 dhidi ya Philadelphia Union.
Kambi ya timu ya taifa ya Argentina imepata habari njema baada ya kubainika kuwa jeraha la nahodha Lionel Messi siyo kubwa kama ilivyohofiwa.
Nyota huyo wa Inter Miami aliwatia hofu mashabiki juzi Jumapili, Mei 24, 2026 baada ya kuondoka uwanjani akichechemea kutokana na maumivu ya misuli ya paja, wakati wa ushindi wa Inter Miami wa mabao 6-4 dhidi ya Philadelphia Union.
Hata hivyo, klabu ya Inter Miami imetoa taarifa baada ya vipimo vya kina vya daktari. Klabu hiyo imeeleza kuwa Messi anasumbuliwa na uchovu mkubwa wa misuli kwenye paja lake la kushoto, na siyo mpasuko wa misuli, hivyo muda wa kurejea uwanjani utategemea jinsi mwili wake utakavyoendelea kuimarika siku hadi siku chini ya uangalizi wa madaktari.
Kwa sasa, Ligi Kuu ya Marekani (MLS) imesimama kupisha michuano hiyo mikubwa, hali inayompa Messi nafasi nzuri ya kupumzika.
Messi (38) alionekana akishika paja lake kabla ya kuomba kufanyiwa mabadiliko dakika ya 73 ya mchezo na kuelekea moja kwa moja vyumbani. Changamoto hiyo ilijitokeza zikisalia siku chache kabla ya Argentina kuanza kambi yao ya maandalizi huko Kansas City, kwa ajili ya kutetea ubingwa wao wa dunia walioupata miaka minne iliyopita nchini Qatar.
Argentina itashuka dimbani Juni 16, 2026 kucheza mechi ya kwanza ya Kundi J dhidi ya Algeria huko Kansas City, kabla ya kumenyana na mataifa ya Austria na Jordan katika hatua hiyo ya makundi.