Prime
TUMIA HELA! Mkwanja ulivyotumika kunasa vifaa vipya, Big Six balaa zito
Muktasari:
- Hata hivyo, kwenye ishu ya pesa taslimu zilizotumika msimu huu kwenye kusajili wachezaji, Manchester United inashika namba moja. Wakati kocha mpya
LONDON, ENGLAND: PEP Guardiola alibonyeza kitufe cha hali ya hatari kwenye usajili wa dirisha la Januari.
Baada ya kuanza msimu vibaya kwenye historia yake ya ukocha - ikiwamo kukumbana na vichapo vitano mfululizo kabla ya kufanya hovyo tena dhidi ya Feyenoord - Guardiola ametumia Pauni 182 milioni kusajili mastaa wapya kujaribu kubadili hali ya mambo kwenye kikosi cha Manchester City.
Man City ilifungua dirisha la usajili kwa kumnasa beki wa kati Abdukodir Khusanov kwa Pauni 33.6 milioni. Guardiola alisajili tena beki mwingine, Vitor Reis kwa ada ya Pauni 29.6 milioni. Kwenye fowadi, Man City ilitoa Pauni 64 milioni kumsajili Omar Marmoush kutoka Eintracht Frankfurt.
Juma Bah alijiunga na Man City kwa ada ya Pauni 5.1 milioni na kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili ilitoa Pauni 50 milioni kumnasa kiungo wa Kihispaniola, Nico Gonzalez. Pamoja na Savinho, aliyenaswa kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana kwa ada ya Pauni 21 milioni, jambo hilo limefanya Man City kutumia zaidi ya Pauni 200 milioni kwenye usajili wa wachezaji msimu huu.
Lakini, pia iliingiza Pauni 159 milioni kwa kuuza wachezaji. Zaidi ya pesa hizo za mauzo ilizipata kwa Julian Alvarez, aliyeuzwa Atletico Madrid, wakati uhamisho wa Joao Cancelo kwenda Saudi Arabia pia umeongeza pesa kwenye akaunti yao. Hata hivyo, kwa pesa waliyotumia kwenye kununua wachezaji, ukitoa mapato ambayo ilivuna kwenye mauzo ya wachezaji, Man City inakuwa imetumia pesa taslimu Pauni 42 milioni kwenye usajili.
Hata hivyo, kwenye ishu ya pesa taslimu zilizotumika msimu huu kwenye kusajili wachezaji, Manchester United inashika namba moja. Wakati kocha mpya
Ruben Amorim akitumia Pauni 29 milioni tu kwenye dirisha la Januari kumsajili beki wa kushoto, Patrick Dorgu - pesa hiyo inaongezeka kwenye Pauni 200 milioni iliyotumika kwenye dirisha la kiangazi kuwasajili Joshua Zirkzee, Leny Yoro, Matthijs de Ligt, Noussair Mazraoui na Manuel Ugarte.
Kutokana na kuingiza Pauni 86 milioni tu kwenye mauzo ya wachezaji, hiyo ina maana Man United imetumia pesa taslimu Pauni 143 milioni msimu huu.
Makala haya yanahusu matumizi taslimu kwenye usajili zilizotumika na klabu za Big Six kwenye Ligi Kuu England kwa kuanzia mwaka 2016.
1. Man United – Pauni 1 bilioni
Tangu mwaka 2016, Manchester United imetumia Pauni 1.37 bilioni kwenye usajili wa nyota wapya.
Paul Pogba aliwasili Man United kwa Pauni 89 milioni mwaka huo, kisha zikaja dili za pesa nyingi kama za Antony (Pauni 85.5milioni), Harry Maguire (Pauni 85milioni), Romelu Lukaku (Pauni 75milioni), Jadon Sancho (Pauni 73milioni) na Rasmus Hojlund (Pauni 72milioni) wote hao walinaswa. Kwa msimu huu, usajili wao wa pesa nyingi ni wa Leny Yoro, Pauni 52 milioni. Mauzo ya mchezaji ya pesa nyingi kwa Man United yanabaki yale ya Cristiano Ronaldo, aliyeuzwa Real Madrid kwa Pauni 80 milioni mwaka 2009, lakini kwa kuanzia 2016 mauzo makubwa ni yale ya Pauni 73 milioni ilipomuuza straika Romelu Lukaku kwenda Inter Milan mwaka 2019. Ilivuna pia kwenye mauzo ya Mason Greenwood (Pauni 26.6milioni) na Scott McTominay (Pauni 25milioni) na kwa ujumla Man United iliingiza Pauni 371 milioni kwenye mauzo na hivyo kuwafanya kutumia pesa taslimi Pauni 1 bilioni kwenye usajili tangu 2006.
2. Chelsea – Pauni 836 milioni
Matumizi ya Chelsea kwenye usajili yamekuwa ya kibabe zaidi hasa baada ya ujio wa tajiri mpya, bilionea Todd Boehly mwaka 2022. Lakini, katika kipindi cha miaka tisa iliyopita, kwa ujumla The Blues ilitumia Pauni 1.97 bilioni kunasa nyota wapya.
Msimu huu ililipa Pauni 54 milioni kumnsajili Pedro Neto milioni, lakini Chelsea ilitumia pesa nyingi kuwanasa Wesley Fofana (Pauni 75milioni), Kai Havertz (Pauni 70milioni) na Romelu Lukaku (Pauni 97.5milioni). The Blues inabaki kuwa timu pekee England kutumia zaidi ya Pauni 100 milioni kwa wachezaji wawili tofauti, Enzo Fernandes (Pauni 106 milioni) na Moises Caicedo (Pauni 115milioni). Kama ilivyoongoza kwenye matumizi, Chelsea pia ni wazuri kwenye kuuuza, ambapo ilivuna hadi Pauni 1.13 bilioni kwenye mauzo ya wachezaji, ikiwamo Eden Hazard (Pauni 88milioni), Havertz (Pauni 65milioni), Mason Mount (Pauni 60 milioni), Lewis Hall (Pauni 28milioni), Conor Callagher (Pauni 36milioni), Lukaku (Pauni 25.2milioni) na Ian Maatsen (Pauni 37.5 milioni) na hivyo kuifanya timu hiyo kuwa na matumizi taslimu kwenye usajili kuwa Pauni 836 milioni.
3. Man City – Pauni 695 milioni
Umeshapata mchongo wote wa Man City kuhusu matumizi yao ya msimu huu kwenye dirisha la usajili lile la majira ya kiangazi la mwaka jana na hili la majira ya baridi la Januari lililofungwa Jumatatu iliyopita. Lakini, umeshapata picha halisi ya matumizi ya Man City kwenye usajili katika zama za Guardiola?
Kwa ujumla wake, miamba hiyo ya Etihad imetumia Pauni 1.46 bilioni kwenye ishu ya usajili na kushika namba mbili nyuma ya Chelsea.
Usajili wa Marmoush anashika namba nne kwa kuwa ghari, nyuma ya Ruben Dias na Josko Gvardiol (Pauni 77 milioni) na ule wa Jack Grealish, uliowagharimu Pauni 100 milioni. Kama ilivyo kwa Chelsea, Man City nayo imevuna pesa za kutosha kwenye mauzo ya wachezaji hasa kwa makinda, ambao walivuna faida ya moja kwa moja kutokana na kuibukia kwenye akademia. Alvarez dili lake linaweza kupanda hadi Pauni 81.5 milioni, huku pia ikivuna pesa kupitia makinda Taylor Harwood-Bellis (Pauni 20milioni), Liam Delap (Pauni 15milioni), Sergio Gomez (Pauni 8.4milioni) na Tommy Doyle (Pauni 4.3milioni).
Baada ya After Alvarez, Man City mauzo yao makubwa ni ya mastaa Raheem Sterling, Ferran Torres, Gabriel Jesus, Leroy Sane na Cole Palmer (wote iliwauza kwa bei kati ya Pauni Pauni 40 milioni na Pauni 47.5 milioni. Kwa ujumla wake, Man City imetumia pesa taslimu Pauni 695 milioni.
4. Arsenal – Pauni 688 milioni
Man City imetumia pesa taslimu kwenye usajili kwa zaidi ya Pauni 7 milioni au zaidi kuliko Arsenal katika kipindi hicho kinacholingana. Hata hivyo, ndani ya muda huo, Man City imeshinda mataji sita ya Ligi Kuu England, manne ya Kombe la Ligi na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya na jingine la Klabu Bingwa Dunia na mataji ya Kombe la FA. Kwa Arsenal, pesa taslimu iliyotumia kwenye usajili ni Pauni 688 milioni, ikiwamo Pauni 23 milioni ilizotumia msimu huu, ambapo ilitua Pauni 100 kunasa nyota wapya, huku ikiwa umeingiza Pauni 77 milioni kwa kuuza.
David Raya (Pauni 27milioni), Riccardo Calafiori (Pauni 42milioni) na Mikel Merino (Pauni 31milioni) ulikuwa usajili mkubwa wa waliokuja, lakini Emile Smith Rowe (Pauni 27milioni), Aaron Ramsdale (Pauni 18milioni) na Eddie Nketiah (Pauni 25milioni) wote hao waliuzwa. Arsenal imeonyesha ni timu isiyoogopa kusajili kwa pesa nyingi, ililipa Pauni 60 milioni kumnasa Pierre-Emerick Aubameyang, Pauni 72 milioni kumsajili Nicolas Pepe kabla ya dili za karibuni za kuwanasa Kai Havertz (Pauni 65milioni) na Declan Rice (Pauni 105milioni). Ukichukua matumizi na mauzo ya wachezaji, kwa ujumla wake, Arsenal imetumia pesa taslimu Pauni 688 milioni kwenye usajili wa wakati wapya kwenye kikosi chao.
5. Tottenham – Pauni 580 milioni
Tottenham Hotspur imebaki kidogo tu kufikisha matumizi ya Pauni 1 bilioni kwenye usajili kwa kuanzia mwaka 2016 - ambapo imetumia Pauni 995 milioni.
Pesa hiyo inajumlisha Pauni 145 milioni ilizolipa msimu huu kunasa mastaa Dominic Solanke (Pauni 65milioni), Archie Gray (Pauni 40milioni), Wilson Odobert (Pauni 25milioni) na kipa Antonin Kinsky (Pauni 12.5milioni), ambaye alisajiliwa kwenye dirisha la Januari.
Wachezaji wengine waliosajiliwa kwa pesa nyingi ni Richarlison (Pauni 50milioni), Dejan Kulusevski (Pauni 25milioni), James Maddison (Pauni 40milioni), Pedro Porro (Pauni 37.3milioni), Micky van de Ven (Pauni 35milioni) na Brennan Johnson (Pauni 47.5milioni).
Kwenye upande wa mauzo yao, Spurs imevuna Pauni 415 milioni ndani ya muda huo, huku mauzo yao makubwa ni ya straika Harry Kane, aliyekwenda Bayern Munich mwisnoni mwa msimu uliopita kwa ada ya Pauni 86 milioni. Kyle Walker uhamisho wake wa kwenda Manchester City mwaka 2017 uliwaingizia Pauni 50 milioni, huku mauzo makubwa ya msimu huu ni ya Oliver Skipp (Pauni 20milioni), Emerson Royal (Pauni 12.8milioni) na Joe Rodon (Pauni 10milioni).
Na kwa ujumla wake, Spurs imetumia pesa taslimu Pauni 580 milioni kwenye usajili wa mastaa wake wote tangu mwaka 2016.
6. Liverpool – Pauni 282 milioni
Haishangazi kuona Liverpool ikiwa na kiwango bora kabisa cha pesa taslimu kwenye matumizi ya timu hiyo kwenye usajili kikiwa Pauni 282 milioni kwa kipindi cha misimu tisa iliyopita. Kwa kifupi, Liverpool ilitengeneza faida msimu wa 2024-25, ambapo ilitumia Pauni 10 milioni tu kumsajili Federico Chiesa na ilikusanya zaidi ya Pauni 50 milioni kwenye mauzo ya wachezaji, ilipowapiga bei Fabio Carvalho (Pauni 20milioni), Sepp van den Berg (Pauni 20milioni) na Bobby Clark (Pauni 10milioni). Liverpool imekuwa ikifanya mambo yake kijanja sana, hasa kwenye mauzo ya wachezaji kwa bei kubwa, huku yenyewe ikifanya usajili kwa kuzingatia usahihi kuanzia kwenye mchezaji na bei. Kabla ya 2016, Liverpool ilifanya biashara nzuri ya kuuza wachezaji kama Luis Suarez, Fernando Torres na Raheem Sterling. Ilipiga mkwanja mrefu, Pauni 145 milioni kwenye mauzo ya Philippe Coutinho mwaka 2018.
Liverpool pia haijawahi kuwa na uoga kwenye matumizi ya pesa, Pauni 787 milioni imetumia tangu mwaka 2016 - ambapo ilitumia Pauni 85.3 milioni kumnasa Darwin Nunez mwaka 2022 ambayo ni rekodi yao kwenye uhamisho mbele ya Virgil van Dijk (Pauni 75milioni), Alisson (Pauni 67milioni), Dominik Szoboszlai (Pauni 60milioni) na Naby Keita (Pauni 53milioni). Lakini, kinachovutia ni kwamba Liverpool imetumia pesa taslimu Pauni 282 milioni tangu mwaka 2016, ikiwa ni kiwango kidogo kuliko ilichotumia West Ham (Pauni 451milioni) na Newcastle (Pauni 396milioni) na Pauni 8 milioni tu zaidi ya Aston Villa baada ya kumuuza Jaden Philogene (Pauni 20milioni), Diego Carlos (Pauni 8.5milioni) na Jhon Duran (Pauni 64milioni).