TRA kuinunua Tabora Utd ituzindue
Muktasari:
- Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, Tabora United itaendelea kuwa mkoani Tabora, ikiwa chini ya uongozi wa TRA Tabora hadi mwishoni mwa mwaka na baadaye kuhamia Dar es Salaam ambako itakuwa chini ya makao makuu.
KAMA nilivyoandika wiki iliyopita kuhusu ununuzi wa klabu, hatimaye imewekwa bayana kuwa klabu ya Tabora United sasa imeuzwa na kununuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambayo imesema itaitumia kuhamasisha watu kulipa kodi.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, Tabora United itaendelea kuwa mkoani Tabora, ikiwa chini ya uongozi wa TRA Tabora hadi mwishoni mwa mwaka na baadaye kuhamia Dar es Salaam ambako itakuwa chini ya makao makuu.
Na badala ya kujulikana kama Tabora United, sasa itaitwa TRA United.
Kwa uimara wa kiuchumi, mpango huo ni bora kwa klabu hiyo ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na taasisi ya Kitayosce ya Kilimanjaro kabla ya kuuzwa kwa mmiliki mwingine mkoani Tabora.
Lakini kwa utamaduni wa soka, uamuzi huo ni kama unakwenda kinyume na utamaduni wa mchezo huo maarufu duniani. Na hii ni kwa sababu hakuna kanuni zinazoongoza umiliki na ununuzi wa klabu za soka.
Kwanza ununuzi huo unaohusisha kubadili jina na makazi unawanyima wakazi wa Tabora haki yao waliyoanza kuifurahia ya kushabikia klabu ya mkoani kwao kama wao walivyopoka haki hiyo kutoka kwa wananchi wapenda soka wa mkoani Kilimanjaro na baadae Lindi.
Kwa miaka miwili ambayo Tabora United imecheza Ligi Kuu iliamsha ari ya kupenda soka kwa wakazi wa Tabora, mkoa ambao pia ulikuwa ukizalisha wachezaji wazuri wakati kulipokuwapo na taasisi ya Chipukizi katikati ya mji huo.
Mbali na kujenga mapenzi kwa Tabora United, klabu hiyo iliwawezesha wakazi wa mkoa huo na mingine ya jirani kuona klabu zote za Ligi Kuu wakati zikienda kucheza mechi za ugenini kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Wakazi hao sasa wataikosa timu waliyoanza kuipenda na watakuwa wakikumbuka tu kwamba ilikuwa timu yao wakati watakapoiona kupitia runinga ikicheza mechi za Ligi Kuu kwa jina la TRA.
Ununuzi huo, ambao umeshakuwa utamaduni, ni njia ya mkato ya kutafuta mafanikio ya haraka kama ambavyo klabu nyingi za Ligi Kuu zimefanya. Na badala yake, maendeleo katika ngazi za chini hayapati msukumo wa kifedha, bali juhudi binafsi zinazoambatana na shida nyingi.
Klabu kama Pan Africans, Cosmopolitan na nyingine zimejaribu kutumia mtindo huo kwa kununua klabu za Ligi Daraja la Kwanza, lakini njia ya kufika Ligi Kuu ikawa ndefu zaidi na hivyo kuishia ngazi za chini.
Ni lazima Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) zitengeneze mwongozo wa umiliki na ununuzi wa klabu ili kuwe na uhakika wa kuwapo kwa klabu kama Tabora United, Singida Black Stars, Tukuyu Stars na nyingine.
Mwongozo wa umiliki na ununuzi wa klabu utatofautiana kwa klabu zinazomilikiwa na taasisi, mtu binafsi au wanachama na utawezesha klabu nyingi za wanachama kuzinduka kwa kuwa zina chapa isiyosahaulika inayoambatana na utamaduni fulani ambao wadhamini wangependa kujihusisha nao na hivyo wawekezaji kuona umuhimu wa kununua hisa za klabu hiyo ili wanufaike na udhamini.
Kwa sasa umiliki wa klabu za wanachama unaongozwa na Kamisheni ya Ushindani Sawia (FCC), lakini nayo itaweza kufanya kwa ufanisi usimamizi huo iwapo kutakuwa na mwongozo wa umiliki na ununuzi. Mwongozo huo wa FCC unataka taasisi ya wanachama iuze asilimia 49 za hisa zake kwa watu wasiopungua wawili.
Lakini kuna mambo zaidi ya kuzingatia katika umiliki na ununuzi wa klabu ambayo yatawezesha masuala hayo kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Mwongozo huo ungekuwapo, isingekuwa rahisi kwa TRA kwenda kuinunua Tabora United, na badala yake ingeangalia kama TFF au Bodi ya Ligi wana vifurushi vitakavyowawezesha kuhamasisha umma kulipa kodi.
Kwa mfano taasisi yenye kampeni kubwa kama hiyo kwenda kumiliki klabu moja ni kuidogosha kampeni yenyewe. TRA ilitakiwa iwe mshirika wa Bodi ya Ligi katika kampeni yake ya kuhamasisha watu kulipa kodi.
Hiyo itategemea jinsi TFF au TPLB ilivyotengeneza bidhaa zake, kikiwapo hicho cha washirika (partners) wa kushirikiana nao katika kampeni mbalimbali kama Bodi ya Utalii, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, TRA na zile za kimataifa zinazojishughulisha na masuala ya kiafya.
Hawa wanatakiwa waonyeshwe watanufaikaje kwa kuwa washirika wa Ligi Kuu na hivyo kutumbukiza fedha zao ambazo zitasaidia programu za maendeleo ya soka, hasa katika ngazi za chini.
Ni muhimu sana kwa mamlaka za soka kuona haja ya kuongoza mabadiliko hayo ya umiliki wa klabu na ununuzi. Utamaduni wa kampuni au taasisi za serikali kumiliki klabu kwa ajili ya kujitangaza ni wa kizamani sana na uliathiri mpira wakati serikali ilipoanza sera ya kubana matumizi, hasa baada ya kulegeza masharti ya kiuchumi.
Si vizuri kuona soka likiathirika tena kutokana na mabadiliko ya sera za kisiasa wakati uwezo wa kuzuia athari hizo upo.
Hadi sasa TFF na TPLB hazijui baadhi ya wamiliki wa baadhi ya klabu wala taarifa zao za fedha zilizokaguliwa. Hii ni hatari kwa ligi. Hakuna kanuni za udhibiti wa matumizi ya fedha kama wenzetu barani Ulaya walivyo na FFP.
Kama hatuna hayo machache kati ya mengi, kwanini tusianze na moja?
Uamuzi wa TRA kuinunua Tabora United utuzindue.