Jinsi makosa ya kunyoa yanavyoharibu ngozi yako
Muktasari:
- Mwishowe wanapata vipele, muwasho, majipu au hata maambukizi ya ngozi, halafu wanaanza kulaumu ngozi zao. Ukweli ni kwamba, mara nyingi tatizo siyo kunyoa, bali ni namna unavyofanya zoezi hilo.
KUNA watu wakishika mashine ya kunyolea au wembe wanajiona tayari ni wataalamu. Wengine wananyoa kwa kutumia wembe uliotumika mara nyingi, wengine wanakimbilia saluni yoyote iliyo karibu bila kujali usafi wake.
Mwishowe wanapata vipele, muwasho, majipu au hata maambukizi ya ngozi, halafu wanaanza kulaumu ngozi zao. Ukweli ni kwamba, mara nyingi tatizo siyo kunyoa, bali ni namna unavyofanya zoezi hilo.
Kama unapenda kunyoa ndevu, nywele au sehemu nyingine za mwili, ni muhimu kujua makosa yanayoweza kuhatarisha afya yako. Haya ndiyo makosa makubwa ambayo wengi huyafanya.
USITUMIE WEMBE AU MASHINE CHAFU
Hili ni kosa ambalo watu wengi hulifanya bila kujua madhara yake. Wembe au mashine isiposafishwa vizuri hubeba uchafu, bakteria na vijidudu vinavyoweza kuingia kwenye ngozi wakati wa kunyoa.
Ngozi inapokatika hata kidogo, bakteria hupata nafasi ya kuingia mwilini na kusababisha maambukizi. Ndiyo maana ni muhimu kusafisha vifaa vya kunyolea kila baada ya matumizi na kuhakikisha vinahifadhiwa sehemu safi.
USISHIRIKIANE WEMBE AU MASHINE NA MTU MWINGINE
Kuna watu wanaona siyo tatizo kutumia mashine ya rafiki au mwanafamilia. Lakini ukweli ni kwamba kufanya hivyo kunaweza kuongeza hatari ya kuambukizana baadhi ya magonjwa ya ngozi.
Hata kama huoni damu kwa macho, wakati wa kunyoa kunaweza kutokea michubuko midogo midogo sana ambayo hubaki na mabaki yasiyoonekana. Kwa hiyo, ni salama kila mtu akatumia vifaa vyake binafsi.
USINYOE NGOZI ILIYO KAVU
Kunyoa ngozi kavu kunaongeza uwezekano wa kupata mikato, kuwashwa na maumivu. Pia nywele huwa ngumu kukatika vizuri na hivyo kulazimika kurudia sehemu moja mara nyingi.
Ni vizuri kwanza kuosha eneo husika kwa maji ya uvuguvugu ili ngozi na nywele zilainike. Unaweza pia kutumia povu au krimu maalumu ya kunyolea ili wembe uteleze vizuri bila kuharibu ngozi.
USITUMIE NGUVU
Baadhi ya watu wanaamini kuwa kubonyeza wembe kwa nguvu kunatoa matokeo mazuri zaidi. Ukweli ni tofauti.
Ukibonyeza sana unaweza kujikata, kuharibu ngozi na kusababisha maumivu. Wembe unatakiwa kupita taratibu bila kutumia nguvu nyingi. Kama wembe haukata vizuri, mara nyingi tatizo ni kuwa umepitwa na wakati na unahitaji kubadilishwa.
BADILISHA VIFAA MARA KWA MARA
Kutumia wembe uliopitwa na wakati kunaweza kusababisha michubuko na muwasho kwa sababu unakuwa haukati vizuri.
Kadiri unavyoendelea kuutumia, ndivyo unavyopoteza makali na kukusanya uchafu. Kubadilisha wembe kwa wakati husaidia kupata matokeo mazuri na kulinda afya ya ngozi.
USAFI BAADA YA KUNYOA
Baada ya kunyoa, watu wengi huondoka tu bila kuosha eneo walilonyoa. Hili siyo jambo zuri.
Ni muhimu kuosha ngozi kwa maji safi ili kuondoa mabaki ya nywele na povu. Baada ya hapo paka bidhaa nyepesi inayosaidia kutuliza ngozi. Kama ngozi yako ni nyeti, epuka bidhaa zenye kemikali kali au harufu nyingi ambazo zinaweza kuongeza muwasho.
CHAGUA SALUNI USAFI
Kama hunyoi nyumbani, hakikisha saluni unayokwenda inazingatia usafi.
Mashine zinapaswa kusafishwa baada ya kila mteja, taulo ziwe safi na wembe uwe mpya au umetengwa kwa matumizi ya mteja mmoja. Ukiona mazingira siyo safi au vifaa vinatumika kwa watu wengi bila kusafishwa, ni bora uondoke kuliko kuhatarisha afya yako.
USIPUUZE DALILI HIZI
Ukiona baada ya kunyoa una vipele vinavyozidi kuongezeka, maumivu makali, usaha, uvimbe au ngozi kuwa nyekundu kwa muda mrefu, usipuuzie hali hiyo.
Dalili hizo zinaweza kuashiria maambukizi yanayohitaji ushauri au matibabu kutoka kwa mtaalamu wa afya. Kutafuta msaada mapema kunaweza kuzuia tatizo kuwa kubwa zaidi.
Kunyoa ni sehemu ya kujitunza na kuongeza nadhifu ya mwonekano, lakini hakupaswi kuhatarisha afya yako. Ukiwa makini na usafi wa vifaa, ukitumia njia sahihi za kunyoa na ukachagua saluni zinazozingatia usafi, utaweza kuwa nadhifu huku ukilinda ngozi yako dhidi ya maambukizi. Kumbuka, urembo wa kweli huanza na afya njema ya ngozi.
MSIKIE MTAALAMU WA NGOZI
Daktari Dorcas Natse anasema; “Watu wengi hudhani maambukizi baada ya kunyoa ni jambo la kawaida, lakini mara nyingi husababishwa na kutumia wembe au mashine isiyo safi.
Ngozi inapopata mikato midogo, bakteria wanaweza kuingia kwa urahisi na kusababisha vipele, majipu au maambukizi mengine. Ndiyo maana usafi wa vifaa vya kunyolea ni muhimu kama ilivyo usafi wa ngozi yenyewe.”
MSIKIE KINYOZI
Mmoja kati ya wamiliki wa saluni hapa Jijini Dar es salaam anasema kuwa;“Mteja anapaswa kuwa makini na saluni anayochagua.
Kila mteja anatakiwa kutumia wembe mpya au kifaa kilichosafishwa na kuwekewa dawa ya kuua vijidudu. Pia, baada ya kunyoa ni vizuri kusafisha ngozi na kutumia bidhaa zinazotuliza ngozi ili kupunguza muwasho na kuzuia maambukizi.”