Juma Choki dhidi ya Tony Rashid: Fedha, heshima na gari viko mezani
Muktasari:
- Ni pambano la Juma Choki dhidi ya Tony Rashid, litakaloongoza kadi kuu ya Dar Boxing Derby 2026 lakini tofauti na mapambano mengi yaliyopita, safari hii mshindi ataondoka na zawadi ya gari aina ya Toyota Crown New Model, zawadi iliyowekwa na wadhamini Euromax Limited kwa kushirikiana na QFK Motor kupitia Pick Time Media na Pent Promotion.
UKIZUNGUMZIA pambano kubwa, mara nyingi watu huzungumzia mikanda ya ubingwa, rekodi za mabondia au historia zao lakini safari hii, kuna sababu nyingine ambayo imefanya macho ya mashabiki wengi wa ngumi nchini kuelekezwa kwenye viwanja vya Ubungo East African Logistic Center Ijumaa hii.
Ni pambano la Juma Choki dhidi ya Tony Rashid, litakaloongoza kadi kuu ya Dar Boxing Derby 2026 lakini tofauti na mapambano mengi yaliyopita, safari hii mshindi ataondoka na zawadi ya gari aina ya Toyota Crown New Model, zawadi iliyowekwa na wadhamini Euromax Limited kwa kushirikiana na QFK Motor kupitia Pick Time Media na Pent Promotion.
Hata hivyo, gari hilo si sababu pekee inayolifanya pambano hili kuwa kubwa. Ukweli ni kwamba, ndani ya ulingo kutakuwa na vita ya falsafa mbili tofauti za ngumi, mabondia wawili wenye njaa ya ushindi na kila mmoja akiwa na sababu zake za kutaka kuondoka akiwa mshindi.
Kwa mujibu wa waandaaji, zawadi ya gari haimaanishi mabondia wanapigania gari hilo pekee. Tayari walishalipwa kwa mujibu wa mikataba yao kama ilivyo katika ngumi za kulipwa. Gari limeongezwa kama motisha ya kuongeza ushindani na kuonyesha kwamba ngumi zinaweza kuwa mchezo unaobadilisha maisha.
Kauli hiyo ina maana kubwa kwa sababu kwa miaka mingi mabondia wengi wamekuwa wakihangaika kupata mapambano yenye thamani kubwa. Kuona mshindi akiondoka na gari la kisasa ni ishara kwamba sekta ya ngumi inavutia wawekezaji wanaotaka kuongeza thamani ya mchezo huo.
HAKUNA UNYONGE
Choki anaingia kwenye pambano hili akiwa mmoja wa mabondia waliopata mafanikio makubwa ndani ya miaka ya karibuni. Safari yake ya ngumi za kulipwa imekuwa ikipanda hatua kwa hatua huku akikutana na changamoto mbalimbali zilizomjenga kuwa mmoja wa mabondia wanaofanya vizuri.
Kupambana na mabondia wenye majina makubwa kama Nasibu Ramadhani, kushiriki mashindano ya kimataifa nchini Saudi Arabia kupitia mashindano ya WBC Grand Prix pamoja na kuendelea kujenga jina kwenye jukwaa la kimataifa, kumemfanya Choki kuwa bondia mwenye uzoefu wa mapambano makubwa.
Kwa mujibu wa rekodi za BoxRec, Choki ambaye anapigana katika uzito wa Lightweight, amekuwa katika ngumi za kulipwa tangu mwaka 2017. Rekodi yake inaonyesha amecheza mapambano 13 ya kulipwa, akishinda mapambano 11, kupoteza moja na kutoka sare moja huku akiwa na uwezo wa kumaliza mapambano mapema baada ya kupata ushindi wa KO mara nne.
Bondia huyo mwenye mtindo wa kupigana kwa mkono wa kushoto (southpaw) alianza safari yake ya kulipwa Septemba 30, 2017 na tangu hapo ameendelea kupanda viwango kwa kukutana na wapinzani kutoka maeneo mbalimbali.
Miongoni mwa mapambano yake makubwa ni ushindi dhidi ya Nasibu Ramadhani Juni 2024, pambano ambalo lilionyesha uwezo wake wa kuvumilia presha na kutumia nafasi muhimu ndani ya ulingo baada ya kumwangusha mpinzani wake raundi ya saba.
Pia Choki amewahi kuwakabili mabondia wa kimataifa kama Bryx Piala na Bhekizizwe Maitse nchini Saudi Arabia katika mashindano ya WBC Grand Prix, hatua iliyompa uzoefu mkubwa wa kupambana kwenye mazingira ya kimataifa.
Licha ya mafanikio hayo yote, Choki amesema hataingia ulingoni akiwa na hisia kwamba tayari ni bondia mkubwa au kwamba historia yake inaweza kumpa ushindi wa moja kwa moja dhidi ya Tony Rashid. Badala yake, amesema ataingia akiwa na mtazamo wa bondia anayepigana pambano lake la kwanza.
Akizungumzia namna anavyoliangalia pambano hilo, Choki amesema hatatumia historia yake kama sababu ya kujiona bora, bali ataingia ulingoni akiwa tayari kwa vita mpya.
“Mimi sitaingia kwenye pambano hili nikifikiria kwamba nimecheza na Nasibu, nimecheza Saudi Arabia au nimepata mafanikio fulani. Hapana. Nitaingia kama vile ndiyo naanza safari yangu ya ngumi, kama vile ni pambano langu la kwanza. Tony Rashid namheshimu na nimejiandaa kwa ajili ya kitu kikubwa,” anasema Choki.
Kauli hiyo inaonyesha namna ambavyo Choki anavyoliheshimu pambano hilo na kutambua ukubwa wa changamoto iliyopo mbele yake. Kwa bondia ambaye tayari ameshapanda kwenye majukwaa makubwa na kukutana na wapinzani wa viwango tofauti, uwezo wa kusahau mafanikio ya nyuma na kuanza upya ni sehemu muhimu ya maandalizi ya kiakili.
Katika mchezo wa ngumi, kosa kubwa ambalo bondia anaweza kufanya ni kumdharau mpinzani wake. Historia ya mchezo huo imeonyesha mara nyingi mabondia wenye majina makubwa wameanguka kwa sababu ya kuingia ulingoni wakiwa na imani kupita kiasi.
Choki anaonekana kulifahamu hilo vizuri, ndiyo maana amekuwa akisisitiza kuwa kila bondia anayekubali kusaini pambano anastahili heshima kwa sababu tayari ameonyesha ujasiri wa kukubali changamoto hiyo.
“Siwezi kumdharau mpinzani wangu yeyote. Kila ninayekutana naye namheshimu kwa sababu mpaka amekubali kusaini kupigana na mimi maana yake amejiamini. Mimi najiandaa kila siku na kila pambano ninalichukulia kwa uzito ule ule,” anasema Choki.
Mtazamo huo unaweza kuwa moja ya silaha kubwa za Choki kuelekea pambano la Ijumaa. Bondia anayemheshimu mpinzani wake mara nyingi huingia ulingoni akiwa na umakini mkubwa, akiepuka makosa ya kujiamini kupita kiasi na kuhakikisha anafuata mpango wake wa mchezo.
Kwa Choki, pambano dhidi ya Tony Rashid si nafasi ya kuthibitisha tu uwezo wake wa kupiga ngumi, bali pia ni nafasi ya kuonyesha ukomavu wake kama bondia aliyepitia changamoto mbalimbali na bado ana njaa ya mafanikio mapya.
Zaidi ya rekodi zake za ushindi, jambo linalomtofautisha Choki ni uwezo wake wa kuhimili mapambano yenye presha. Ameonyesha mara kadhaa kwamba anaweza kucheza kwenye mazingira magumu, dhidi ya wapinzani wanaokuja na mitindo tofauti, jambo ambalo linaweza kuwa muhimu katika pambano dhidi ya Tony.
PIGA NIKUPIGE
Upande wa pili pia kuna Tony, bondia ambaye amejijengea utambulisho wake katika ngumi kwa mtindo wa kupambana bila kurudi nyuma. Kwa mashabiki wengi wa mchezo huu, Tony amekuwa akitambulika kama bondia anayependa vita vya ndani ya ulingo, anayekubali kubadilishana makonde na anayefurahia pambano linapokuwa na presha kubwa.
Ndiyo maana amebatizwa jina la “AK-47 Bad Belle”, jina linaloendana na namna ambavyo amekuwa akipigana kwa kasi, ujasiri na kutokuwa na hofu ya kukutana uso kwa uso na wapinzani wake.
Lakini kuelekea pambano dhidi ya Choki, Tony anataka kuonyesha kwamba yeye si bondia wa aina moja pekee. Anataka kuvunja mtazamo kwamba mafanikio yake yanategemea tu kupigana kwa nguvu na kubadilishana makonde.
Amesema katika mapambano yake ya hivi karibuni ameonyesha uwezo wa kutumia mbinu tofauti, ikiwemo kucheza kwa umbali (outboxing) pale mazingira yanapohitaji hivyo.
Kwa Tony, uwezo wa kubadilika ndani ya ulingo ndiyo silaha ambayo anaamini inaweza kumsaidia dhidi ya Choki ambaye anafahamika kwa kutumia miguu vizuri na kupenda kudhibiti umbali wa pambano.
“Tumeangalia namna mpinzani wangu anavyocheza. Makocha wangu wameshachambua mchezo wake na tumefanya maandalizi kulingana na kile tunachokwenda kukutana nacho. Ngumi hazitabiriki, kwa hiyo lazima uwe tayari kubadilika kulingana na hali ya pambano,” anasema Tony.
Kauli hiyo inaonyesha kwamba Tony hataki kuingia kwenye mtego wa kupigana kwa hisia pekee. Anajua kwamba Choki si bondia wa kukimbizwa hovyo, bali ni mpinzani anayejua kutumia nafasi, muda na makosa ya mpinzani wake.
Kwa mujibu wa rekodi za BoxRec, Tony ana uzoefu mkubwa zaidi kwa idadi ya mapambano ukilinganisha na Choki. Bondia huyo wa uzito wa Super Featherweight amecheza mapambano 24 ya kulipwa, akishinda 17, kupoteza manne na kutoka sare tatu huku akiwa na uwezo mkubwa wa kumaliza mapambano mapema baada ya kupata ushindi wa KO mara 11.
Tony alianza safari yake ya ngumi za kulipwa mwaka 2017 na katika kipindi hicho amekutana na mabondia mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Rekodi yake inaonyesha amewahi kupigana kwenye mapambano yenye ushindani mkubwa, ikiwemo dhidi ya mabondia waliokuwa wakigombea mataji ya Afrika.
Miongoni mwa mapambano yaliyomjenga ni ushindi dhidi ya Oscar Duge mwaka 2024, pambano lililomrudisha kwenye mstari baada ya changamoto za nyuma, pamoja na mapambano dhidi ya mabondia wa kimataifa kama Hovhannes Martirosyan nchini Ubelgiji na Asanda Gingqi nchini Afrika Kusini.
Pia Tony amewahi kushindana kwenye mapambano ya mataji ya African Boxing Union (ABU), jambo lililompa uzoefu wa kukutana na mazingira yenye presha kubwa. Hivyo, tofauti na baadhi ya wanaoweza kumwona kama bondia anayategemea zaidi mapigano ya karibu, rekodi yake inaonyesha amekuwa akipitia viwango tofauti vya ushindani.
SASA ITAKUWAJE?
Kwenye makaratasi, hili ni pambano ambalo ni vigumu kulitabiri. Choki anaingia akiwa na faida ya mbinu, nidhamu ya kupigana na uwezo wa kusoma pambano hatua kwa hatua huku Tony akija na uzoefu mkubwa zaidi wa mapambano ya kulipwa, nguvu za kumaliza pambano mapema na ujasiri wa kupambana bila hofu.
Tofauti kubwa inaweza kuonekana kwenye mtindo wa kila mmoja. Choki ni bondia anayependa kutawala umbali, kutumia miguu vizuri na kumpa mpinzani kazi ya kumfuata. Kwa upande mwingine, Tony hupenda kupunguza nafasi haraka, kuingia ndani na kulazimisha kubadilishana makonde, jambo linaloweza kufanya pambano hili kuwa la kasi kuanzia raundi za mwanzo.
Iwapo Choki atafanikiwa kumdhibiti Tony kwa kutumia 'jab zake', mwendo wa miguu na nidhamu ya kutotekwa na presha, ana nafasi kubwa ya kulifanya pambano liende kwa maamuzi ya majaji. Lakini akijikuta anakubali vita vya karibu, anaweza kujikuta akicheza mchezo ambao mpinzani wake anaupenda zaidi.
Kwa upande wa Tony, kazi yake kubwa itakuwa kuvunja mfumo wa Choki mapema. Atahitaji kukata ulingo vizuri, kumzuia asizunguke sana na kumlazimisha kupigana ndani ambako nguvu zake za makonde zinaweza kufanya tofauti. Kadri pambano litakavyozidi kuwa la kushambuliana uso kwa uso, ndivyo nafasi zake za ushindi zinavyoongezeka.
Kinachoongeza uzito wa pambano hili ni kwamba hakuna anayehitaji kushinda kwa pointi. Gari aina ya Toyota Crown New Model, heshima ya kuwa mshindi wa Dar Boxing Derby 2026 na nafasi ya kujitangaza mbele ya wadhamini na waandaaji wa mapambano makubwa ya baadaye, vyote vimeweka presha kwa mabondia hao wawili.
Wachambuzi wengi wa ngumi wanaamini raundi nne za kwanza zinaweza kuamua mwelekeo wa pambano. Kama Choki atazidhibiti kwa mbinu zake, anaweza kujenga msingi wa ushindi. Lakini Tony akifanikiwa kumweka kwenye vita vya karibu mapema, pambano linaweza kubadilika na kuwa moja ya mapambano makali zaidi.
Kwa mashabiki, hii ni aina ya pambano ambalo kila mmoja ana hoja ya kumtetea bondia wake. Rekodi, uzoefu na mitindo yao vinaonyesha hakuna anayemzidi mwenzake kwa kiwango kikubwa, jambo linalofanya matokeo kubaki kuwa fumbo hadi kengele ya mwisho au hadi mmoja wao ashindwe kuendelea.
MSIKIE IBRAHIM CLASS
Akizungumzia pambano hilo, bingwa wa ngumi za kulipwa Tanzania, Ibrahim "King Class Mawe", amesema mashabiki wanapaswa kutarajia pambano la kiwango cha juu kwa sababu mabondia wote wawili wana uwezo wa kushinda na hakuna anayepaswa kumdharau mwenzake.
"Hili si pambano la kawaida. Choki na Tony wote ni mabondia wazuri wenye uwezo tofauti. Choki ni fundi wa kutumia mbinu na miguu yake vizuri, wakati Tony ni bondia anayependa kushambulia na ana nguvu za kumaliza pambano mapema. Mashabiki watarajie pambano kali ambalo linaweza kuamuliwa na makosa madogo sana, " anasema.
Class ambaye ni mmoja wa mabondia wenye mafanikio makubwa nchini, alisema jambo litakalobeba uzito mkubwa ni namna kila bondia atakavyotekeleza mpango wake wa mchezo ndani ya ulingo.
"Choki akifanikiwa kulidhibiti pambano kwa umbali atakuwa na nafasi nzuri, lakini Tony akimlazimisha kupigana ndani, mambo yanaweza kubadilika haraka. Haya ndiyo mapambano ambayo yanawavutia mashabiki."
MCHONGO KWA MABONDIA
Mbali na mshindi kuondoka na Toyota Crown New Model, waandaaji na wadhamini wamesema lengo lao si kutoa zawadi ya gari pekee, bali kuwasaidia mabondia kujenga maisha yenye uhakika hata baada ya kustaafu mchezo wa ngumi.
Mwakilishi wa Distinction Limited, Danstan Myava, anasema kampuni hiyo imeandaa mpango maalumu wa kumfundisha mshindi wa pambano misingi ya biashara kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita ili aweze kutumia zawadi hiyo kama sehemu ya kujenga uchumi wake na si kuishia kuifurahia kwa muda mfupi.
"Tunataka zawadi hii isiishie kuwa gari pekee. Tutamfundisha bingwa namna ya kufanya biashara ili ajenge maisha yake hata baada ya kuachana na ndondi," anasema Myava.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Euromax Limited, wazalishaji wa Smart Gin, Peter Michael, anasema kampuni yao imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono maendeleo ya ngumi za kulipwa tangu mwaka 2017, lakini safari hii imeamua kwenda hatua nyingine kwa kushirikiana na Distinction Limited kuwawezesha mabondia kujitegemea kiuchumi.
"Hii si zawadi ya gari tu. Tunataka kufungua ukurasa mpya ambapo mabondia watakuwa na biashara na vyanzo vya uhakika vya mapato hata baada ya kustaafu mchezo wa ngumi," anasema Peter.
Naye mwakilishi wa PK Pharmacy, Dk. Omari Semunyo, anasema jukumu lao litakuwa kuhakikisha mabondia wanakuwa salama kabla, wakati na baada ya pambano kwa kutoa huduma za kitabibu, akisisitiza kuwa afya ya bondia ni msingi wa mafanikio yake ya sasa na ya baadaye.
"Kuna maisha baada ya ngumi. Ndiyo maana tunahakikisha mabondia wanapata huduma bora za afya ili waendelee kuwa salama hata baada ya kumaliza maisha yao ya ulingoni," anasema Dk. Semunyo.