TFF na Yanga wanavyoliana taimingi

Jumamosi, Mei 8, Taifa liliingia katika taharuki baada ya kushindwa kufanyika kwa mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga uliopangwa kuchezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Sababu kubwa ya mchezo huo kutofanyika ni kitendo cha Yanga kugomea mabadiliko ya ghafla ya muda wa mchezo kutoka saa 11 iliyopangwa awali hadi saa 1 usiku yaliyotangazwa saa tatu kabla ya kuanza kwa mchezo huo. Yanga iliamua kupeleka timu uwanjani katika muda uliopangwa awali wa saa 11, tofauti na ule uliotangazwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) ikidai ilikuwa ni kinyume na kanuni ya 15 (10).

“Mabadiliko yoyote ya muda wa kuanza mchezo yatajulishwa ipasavyo kwa pande zote husika za mchezo angalau saa 24 kabla ya muda wa awali,” inafafanua kanuni hiyo.

Hilo lilipelekea mchezo huo kutofanyika na kufanya serikali iingilie kati ambapo mwanzoni mwa wiki hii, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa maagizo kwa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kushauriana na TFF na TPLB na kutoa majibu ya lini mechi hiyo itachezwa na hatima ya viingilio kwa mashabiki walioenda uwanjani.

Mara baada ya kukutana, wizara ilibaini kutokuwepo kwa maelewano mazuri baina ya Yanga, TFF na TPLB na ilitoa agizo la kukutanisha Yanga na mamlaka hizo za soka ili kutafuta suluhu ya utofauti.

Hilo lilikuwa ni kama ushindi kwa Yanga ambayo tangu mwaka huu ulipoanza imekuwa ikitunishiana msuli na mamlaka za soka nchini.

Mwanaspoti inakuletea orodha ya matukio ya Yanga kuzivimbia TFF na TPLB na mara kadhaa kuibuka mshindi ndani ya mwaka huu.


KUFUNGIWA NA KUSHINDWA RUFAA BUMBULI

Januari 27 mwaka huu Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alifungiwa miaka mitatu kutojihusisha na soka nje na ndani ya Tanzania kwa kosa kutolipa kwa wakati faini ya milioni tano aliyopaswa kulipwa mwaka jana baada ya kukutwa na hatia ya kutoa maneno yasiofaa kwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuhusu sakata la mchezaji Bernard Morrison kwenye kesi yake ya kimkataba dhidi ya klabu yake ya zamani, Yanga.

Hata hivyo, Yanga na Bumbuli hawakuridhishwa na uamuzi huo na kuamua kukata rufaa ambapo Februari 27, mwezi mmoja baadaye, Kamati ya Rufaa ya Nidhamu ilitangaza kutengua adhabu yake na kumuachia huru.


TISHIO LA KUJITOA KWENYE LIGI

Februari 19 mwaka huu, uongozi wa Yanga kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake, Fredricjk Mwakalebela ulitishia kujitoa kwenye Ligi Kuu kwa kile ilichokidai kutotendewa haki na mamlaka za soka pamoja na waamuzi.

“Yanga tumeona kwamba hatutendewi haki na vyombo vinavyosimamia mpira kwa maana ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, Bodi ya Ligi na Kamati ya Saa 72 pamoja na Kamati ya Waamuzi,” alinukuliwa Mwakalebela.

Mwakalebela alisema malalamiko yao hayatofanyiwa kazi, wanafikiria kujitoa katika ligi.

Hilo lilisababisha Kamati ya Maadili ya TFF kumpiga rungu la kumfungia muda wa miaka mitano na adhabu ya Sh5 milioni baada ya kumkuta na hatia ya kuvunja kanuni za kimaadili.


YAIPIGA BAO TFF SERIKALINI

Sakata la Mwakalabela liliibua tetesi za kuwepo kwa maandamano ya mashabiki na wapenzi wa Yanga kuonyesha kutofurahishwa na uamuzi wa kufungiwa kwa makamu mwenyekiti wao.

Taarifa hizo za maandamano hata hivyo uongozi wa Yanga uliyakana, zilisababisha Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa kukutana na uongozi wa Yanga na ule wa TFF kutafuta namna ya kusuluhisha pande hizo Aprili 8.

Huo ulikuwa ni kama ushindi kwa Yanga ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikilalamika kutopata nafasi ya kusikilizwa.


MALALAMIKO MECHI YA NAMUNGO

Wakati upepo wa kuahirishwa kwa mechi yake dhidi ya Simba ukiwa haujatulia, Yanga hivi karibuni ilikiri kuwasilisha maombi ya kutocheza dhidi ya Namungo Jumamosi hii hadi pale wapinzani hao watakapocheza angalau mechi moja dhidi ya Simba. Simba na Namungo bado hazijacheza mechi mbili za Ligi Kuu baina yao hivyo Yanga inaamini kuwa hilo linaweza kupelekea upangaji wa matokeo baina yao. TFF baadaye ikaweka wazi kwamba wanafahamu hilo na ratiba inapangwa kwa wakati.