Tanzania kuna cha kujifunza kwa Morocco?
Muktasari:
- Na katika hilo ni wazi kuwa Morocco imefanikiwa na imebeba matumaini makubwa ya kuwa mwenyeji mwenza wa fainali za Kombe la Dunia za 2030 kwa kushirikiana, Hispania na Ufaransa.
KUNA jambo moja lililoibua funzo kubwa kwa nchi yoyote inayotarajia kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya kimataifa, Morocco imeonyesha wazi kuwa AFCON haikuwa tu mashindano ya wiki chache, bali ilikuwa ni fursa ya taifa kujitangaza Afrika na dunia kwa ujumla.
Na katika hilo ni wazi kuwa Morocco imefanikiwa na imebeba matumaini makubwa ya kuwa mwenyeji mwenza wa fainali za Kombe la Dunia za 2030 kwa kushirikiana, Hispania na Ufaransa.
Hapo ndipo somo la kwanza, tukio kubwa kama AFCON ni fursa ya kuonesha uwezo wa taifa, dira yake, utamaduni, miundombinu na uwezo wa wananchi wake kushirikiana kwa pamoja.
Morocco haijakuchukulia AFCON kama mfululizo wa mechi za soka tu. Iliona huo kama mradi wa kitaifa wenye manufaa ya muda mrefu na kuwekeza kiasi kikubwa katika kila kipengele, kuanzia miundombinu, barabara, reli, viwanja vya ndege, usafiri wa umma, hoteli, uratibu wa mashindano, usalama na hasa ushirikiano na tabia ya wananchi wake.
Hili ndilo funzo la kwanza kwa Tanzania kuelekea AFCON ya 2027 ni kipimo cha taifa, kipimo cha ustawi wa wananchi na kipimo cha jinsi tunavyoweza kushirikiana kama taifa.
MOROCCO NA MAUA YAKE
Moja ya mambo ya kushangaza kuhusu Morocco ni jinsi ilivyofanya maandalizi ya AFCON kuwa mradi wa kitaifa unaoendelea kuzaa matunda hata baada ya mashindano kumalizika. Viwanja vyao vya michezo sio vya kisasa tu, bali ni vya mipango ya matumizi ya muda mrefu.
Barabara zimepangwa kwa njia ya kisasa, zikiwa na alama za usalama zinazoweza kueleweka kwa urahisi na mashabiki wa kimataifa. Hakukua msongamano mkubwa na uratibu wa trafiki umeonekana kuwa rahisi kufuatilia. Mfumo wa reli umeonganisha miji mikubwa kwa ufanisi, huku usafiri wa umma ukiruhusu mashabiki kusafiri bila matatizo ya kiusalama au kiufundi.
Viwanja vya ndege vimefanya kazi bila ucheleweshaji mkubwa. Mashabiki wa kimataifa wamepata urahisi wa kuingia na kutoka nchini. Hali hii imeifanya kuwa Morocco sio tu mahali pa michezo, bali pia mahali pa kuvutia utalii, biashara na uwekezaji. Wageni wanahisi urahisi wa kusafiri, kuona maeneo mapya na kushiriki kikamilifu katika fainali hizo.
Kwa Tanzania, funzo hili ni wazi kuwa miundombinu ya AFCON 2027 isijengwe kwa ajili ya mechi tu, bali iwe ni msingi wa maendeleo ya taifa kwa muda mrefu. Barabara, reli, viwanja vya ndege na hoteli lazima viwe vinavyotimiza mahitaji ya sasa na ya baadaye.
UTAMU ULIPO
Kuanzia unapowasili, mashabiki kutoka mataifa mbalimbali wanahisi wana ukaribu na watu wa Morocco. Hii haikuwa bahati au mpango wa muda mfupi ilikuwa ni matokeo ya mpango wa muda mrefu.
Mchakato wa kupata viza umekuwa rahisi sana. Lugha nyingi zimekuwa zikitumika, ikiwemo Kifaransa, Kiarabu na Kiingereza, ili kuhakikisha hakuna kizuizi cha lugha kwa wageni. Watu wa kujitolea wameonakana kuwa wengi, wakiwa na mafunzo maalumu ya kuongoza mashabiki, kuwapa mwongozo na kuhakikisha wanahisi wanaheshimiwa.
Hali ya usalama pia imehakikisha mashabiki wanahisi kuwa salama. Polisi na maofisa wa usalama wamekuwa kila mahali, lakini walifanya kazi kwa weledi, urahisi na heshima bila kuonekana kama adui wa wageni.
Kwa Tanzania, somo hili ni muhimu sana AFCON 2027 italeta maelfu ya wageni, mashabiki, wanahabari na wawekezaji. Ukarimu wa taifa, usalama, maelekezo wazi na tabia nzuri za wananchi itaunda kumbukumbu ya muda mrefu kwa wageni. Tukishindwa katika hili, mashindano yanaweza kumalizika, lakini taswira ya taifa inaweza kuharibika.
MAANDALIZI YANAYOPASWA KUANZA
Morocco haikusubiri tukio liwe karibu kabla ya kuanza maandalizi. Mipango ilianza miaka kadhaa kabla na kila sekta ya taifa ilihusishwa serikali, sekta binafsi, halmashauri za miji, vyombo vya usafiri, sekta ya utalii, na wananchi wa kawaida.
Hii ilisababisha matokeo makubwa, ikiwemo kugundua changamoto mapema, matatizo ya kiufundi, ulinzi, usafiri na mawasiliano yalitambuliwa na kutatuliwa kabla ya mashindano. Ushirikiano wa wananchi, kila mtu alijua jukumu lake na hivyo kufanya mashindano kuwa na uratibu mzuri.
Kwa Tanzania, somo ni wazi kwamba maandalizi hayapaswi kuanzia siku chache kabla ya mashindano, bali sasa, ili kuhakikisha kila kitu kiko tayari, kuanzia miundombinu, ukarimu, usalama, utalii na mashabiki.
TUSHINDWE WENYEWE
Hii ni fursa ya kihistoria kwa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki. Fursa hii inaweza kuonesha uwezo wa kitaifa mbele ya dunia, kuendeleza utalii wa ndani na wa kimataifa, kuimarisha miundombinu ya muda mrefu, kutoa ajira na kukuza uchumi wa taifa na kuunda mshikamano wa kitaifa.
Morocco ilitumia AFCON kujiweka kwenye ramani ya dunia kama taifa lenye maono, lenye uwezo na linaloshirikiana kikamilifu. Tanzania inaweza kufanya vivyo hivyo ikiwa tutajaribu, tukiweka mpango wa muda mrefu, tukashirikisha wananchi na kuhakikisha kila sekta inashirikishwa.
WASIKIE WADAU
Mwandishi wa habari kutoka Nigeria, Samweli Areo ambaye yupo Morocco kwa ajili ya fainali hizo, anasema: “Nimepata uzoefu mkubwa. Wageni wanahudumiwa kwa heshima na uratibu unaovutia. Hakuna msongamano, hakuna kutoeleweka. Hii ni somo kubwa kwa nchi yoyote inayotarajia kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa.”
Kwa upande wake, Mnoga ambaye alikuwa nchini humo kwa ajili kumsapoti mtoto wake Haji aliyekuwa akiichezea timu ya taifa la Tanzania, anasema Morocco imeonyesha uwezo wa Afrika katika kuandaa mashindano makubwa kuanzia mapokezi hadi miundombinu.
Unaweza mtu kukataa ukiambiwa Morocco ipo Afrika, jambo zuri na kubwa kwa nchi yangu ni kuchukua mazuri ambayo tumeyaona na kujaribu kuyafanyia kazi tunayo nafasi ya kufanya mashindano hayo kuwa na mvuto, tulianza na CHAN naamini hata haya pia inawezekana,” anasema.