Taifa Stars kupata kivuno Afcon 2023?
UHONDO wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 unaendelea baada ya kipyenga cha mwanzo kupulizwa tangu wikiendi iliyopita katika nchi ya Ivory Coast au Cote d’Ivoire, kama inavyopenda kujiita kwa Kifaransa.
Wenyeji hao jana usiku walikuwa wakirudi tena uwanjani kuvaana na majirani zao wa Nigeria, baada ya awali kuanza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Guinea Bissau. Mbali na mechi hiyo jana pia ilipigwa mechi kali ya Masri na Ghana ambazo hazikuanza kwa kishindo fainali hizi tofauti na zilivyozoeleka. Misri ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na Msumbiji, wakati Ghana ilichapwa mabao 2-1 na Cape Verde.
Haya ni mashindano makubwa kabisa barani Afrika yakishirikisha mataifa 24 wanachama wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Inakadiriwa kwamba watu milioni 800 watashuhudia michuano hii kwa njia mbalimbali zikiwamo televisheni na mitandao.
Historia ya mashindano haya inarudi nyuma hadi mwaka 1957 yalipofanyika Sudan kwa kushirikisha nchi tatu za Misri, wenyeji Sudan na Ethiopia, huku Misri ikinyakua ubingwa. Mashindano haya kwa kiasi kikubwa yametawaliwa na taifa la Misri likinyakua mataji saba hadi sasa.
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ni moja ya mataifa yanayoshiriki fainali hizo za Ivory Coast ikiwa ni mara yake ya tatu baada ya mwaka 1980 zilipofanyikia Nigeria ikishirikisha jumla ya nchi nane na mwaka 2019.
Ikumbukwe kwamba 1980, Taifa Stars ilifuzu ushindani ukiwa mkubwa sana kwani fainali zilishirikisha timu nane tu, tofauti na sasa ambapo mashindano yamepanuliwa na kuruhusu karibu nusu ya mataifa yote barani Afrika kushiriki fainali moja.
Binafsi naiona Taifa Stars ya 1980 kama timu bora ya taifa ya kandanda kwa Tanzania upande wa wanaume kwani ilifuzu katika mazingira magumu.
Mchezo wa mwisho wa kufuzu kwa michuano ya Nigeria 1980, Taifa Stars ilishinda ugenini dhidi ya wababe ‘KK Eleven’, timu ya Taifa ya Zambia kwa bao pekee la Augustino Peter ‘Tino’.
Katika mashindano ya mwaka 1980, Taifa Stars ilipangwa kundi moja na wenyeji Nigeria, Ivory Coast na Misri. Stars ilipoteza michezo dhidi ya wenyeji Nigeria (3-1), Misri (2-1 ) na kisha kutoka sare na Ivory Coast ya bao 1-1.
Pamoja na kushika mkia katika kundi lake ikiwa na pointi 1 tu, Taifa Stars ilifunga bao katika kila mchezo na hivyo kumaliza ikiwa na mabao matatu ikiwa imeziona nyavu za kila mpinzani waliyekutana naye pia wakiokota wavuni katika kila mchezo.
Katika fainali za mwaka 2019 ziizofanyika Misri, Stars ilikuwa miongoni mwa timu 24 zilizofuzu kucheza fainali za Afcon. Katika mchezo wa mwisho wa kufuzu iliifunga Uganda ambayo tayari ilikuwa imefuzu, hivyo kufuzu ikiwa nafasi ya pili.
Stars ilicheza fainali hizo dhidi ya Algeria, Senegal na Kenya na ilipoteza michezo yote yaani dhidi ya Senegal (2-0), Kenya (3-2) na Algeria (3-0), hivyo kuondoka mashindanoni ikiwa haina pointi lakini ikifanikiwa kuziona nyavu za Kenya pekee.
Mazingira ya kufuzu kwa Stars hii iliyoko Ivory Coast hayana tofauti sana na yale ya mwaka 2019 kwani imefuzu katika timu 24, huku ikicheza mchezo muhimu wa kufuzu dhidi ya Algeria waliokuwa wanaongoza kundi na wamefuzu tayari na kuweza kutoka nao suluhu.
Huo ndio mchezo uliowazuia Uganda kuifikia Taifa Stars. Stars katika kundi F iko na Morocco waliyocheza nayo juzi usiku na kufungwa mabao 3-0, Zambia na DR Congo zilizotoka sare ya 1-1.
Katika ubashiri wake, mtandao wa kitakwimu wa Opta unaipa Morocco nafasi ya 3 ya uwezekano wa kunyakua Kombe la Afcon 2023, huku DR Congo inapewa nafasi ya 11 na mtandao huo wa Opta, wakati Zambia ikipewa nafasi ya 15.
Mtandao huo haujaijumuisha Tanzania na mataifa mengine 7 katika timu 16 zenye uwezekano wa kubeba Kombe la Afcon kwa mwaka huu. Ubashiri wa mtandao huo unakwenda mbali kwa kuibashiria Tanzania kutocheza vizuri, ingawa inaweza kupata matokeo kupitia jeuri za klabu za Yanga na Simba na ligi inayofanya vizuri barani Afrika. Taifa Stars haina wachezaji wengi wanaocheza ughaibuni kama ilivyo wapinzani wake hasa Morocco na Congo DR.
Hata Zambia inayofundishwa na Avram Grant, kocha Muisraeli aliyewahi kuifundisha Chelsea ya England bado wana kikosi bora sana kulinganisha na kile cha Taifa Stars. Nafasi yetu ya kuchukua ubingwa wa Afcon inakaribia tundu la sindano analoshindwa ngamia kupita, labda inayokuja hapa nyumbani 2027.
Mwandishi wa Makala hii ni mzoefu katika miradi ya maendeleo, utawala na Biashara katika michezo na nyanja nyingine. Ametumikia nyadhifa mbalimbali katika klabu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), CAF na FIFA. Unaweza kumtumia maoni yako kuptia simu yake hapo juu.