Taifa Stars isibweteke, imepata kianzio cha 2027
Muktasari:
- Stars iliwasili asubuhi ya jana, ikiwa imetoka kuweka rekodi mpya ya kucheza hatua ya 16-Bora ya michuano hiyo ya 35 tangu ilipoasisiwa mwaka 1957 baada ya kufungwa na wenyeji Morocco kwa bao 1-0.
TIMU ya taifa ya soka, Taifa Stars imerejea nchini jana na kupokewa kwa bashasha ikitokea katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoendelea kule Morocco.
Stars iliwasili asubuhi ya jana, ikiwa imetoka kuweka rekodi mpya ya kucheza hatua ya 16-Bora ya michuano hiyo ya 35 tangu ilipoasisiwa mwaka 1957 baada ya kufungwa na wenyeji Morocco kwa bao 1-0.
Kwa walioliangalia pambano hilo ni wazi Stars ilistahili ushindi kutokana na ukweli ilipoteza nafasi mbili za wazi kwa kila kipindi moja ya Simon Msuva na nyingine ya Feisal Salum, achilia mbali kunyimwa penalti ya dhahiri na mwamuzi Boubou Traore aliyekataa hata kujishughulisha na V.A.R ili kujiridhisha.
Licha ya kutoka patupu kama ilivyokuwa katika fainali nyingine tatu za nyuma ikiwamo ya mwaka 1980 kule Nigeria, 2019 pale Misri na zile zilizopita za mwaka 2023 zilizofanyika Ivory Coast, mafanikio yaliyopatikana katika michuano hii ni makubwa ukizingatia historia ya ushiriki wa timu hiyo tangu ilipoanza kushiriki.
Zaidi ya matokeo, AFCON 2025 itaendelea kukumbukwa kwa alama kubwa iliyoachwa na kocha Miguel Gamondi pamoja na vijana wake. Gamondi ameonyesha wazi dira mpya ya Stars, akijenga timu yenye nidhamu, ushindani na ujasiri dhidi ya mataifa makubwa barani Afrika. Mbinu zake na imani aliyowawekea wachezaji zilidhihirika uwanjani, hali iliyorejesha matumaini mapya kwa Watanzania wengi waliokuwa wameanza kukata tamaa.
Kwa upande wa wachezaji, viongozi wa uwanjani kama Simon Msuva na Mbwana Samatta walibeba jukumu lao kikamilifu, wakionyesha uzoefu, kujituma na uzalendo mkubwa. Samatta, kama nahodha, alikuwa mfano wa kuigwa ndani na nje ya uwanja, huku Msuva akiendelea kuonyesha umuhimu wake katika timu kwa kasi, maarifa na ari ya ushindani. Feisal Salum naye aliendelea kudhihirisha ubora wake wa kiungo mbunifu, akionesha ukomavu mkubwa na uwezo wa kucheza katika presha katika michuano mikubwa.
Vijana kama Ibrahim Bacca walitumia jukwaa la AFCON kujitangaza na kuonyesha kuwa Stars ina hazina ya vipaji vinavyoweza kulihudumia taifa kwa miaka mingi ijayo. Aidha, kipa Hussein Masalanga alikuwa miongoni mwa wachezaji waliovutia wengi, akifanya kazi kubwa langoni na kuokoa hatari nyingi, jambo lililoipa timu ujasiri mkubwa wa kucheza kwa kujiamini.
Hapo ni mbali na kina Novatus Dismas, Alphonce Mabula, Charles M’Mombwa, Seleman Mwalimu, Tarryn Allarrakhia. Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Shomary Kapombe na wengine waliotumika katika michuano hiyo walivyoonyesha juhudi za kuipigania Stars.
Ndio maana sio ajabu timu hiyo kupokewa kishujaa hata kama haijarudi na taji lolote kama ilivyokuwa katika fainali nyingine tatu zilizopita, ila imejitofautisha.
Hakika, mapokezi ya timu yaliyofanyika jana yanapaswa kuwa ya heshima na pongezi, kwani wachezaji hawa na benchi la ufundi wameonyesha kwamba Taifa Stars ina uwezo wa kushindana na yeyote Afrika.
Walichoacha AFCON 2025 sio tu kumbukumbu ya matokeo, bali ni msingi wa matumaini mapya, umoja wa kitaifa na imani kwamba Tanzania inaelekea mahali pazuri zaidi katika soka la Afrika.
Kutolewa kwa Stars katika fainali hizo za Morocco kunapaswa kuwa chachu ya maandalizi kuelekea AFCON 2027, ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Kama taifa, tunapaswa kujipongeza kwa kile tulichokifanya kwenye mashindano haya, pia kutambua bado tuna kazi kubwa sana ya kufanya, hususan kama wenyeji wa michuano ijayo.
Ujumbe tulioutoa katika AFCON 2025 ni kwamba Stars imepiga hatua. Imani mpya imejengwa kwa mashabiki kutokana na kiwango cha ushindani kilichoonyeshwa na timu dhidi ya wapinzani wakubwa. Ni ukweli usiopingika kwamba kadri timu inavyofanya vizuri, ndivyo matarajio na deni kwa mashabiki yanavyozidi kuongezeka. Hili linatupatia wajibu mkubwa zaidi wa kujiandaa kwa umakini na mipango madhubuti.
Ukiangalia kikosi kilichoshiriki AFCON 2025, utaona mchanganyiko mzuri wa wachezaji wenye uzoefu na vijana. Endapo vijana hawa wataendelea kuaminiwa, kulelewa na kujengwa vizuri, wanaweza kuwa msaada mkubwa kwa taifa kwa muda mrefu.
Hii itasaidia kupunguza mzigo kwa wachezaji waliolitumikia taifa kwa miaka mingi, ambao bado wanahitajika ndani ya kikosi lakini si kubeba mzigo wote. Badala yake, watakuwa viongozi ndani na nje ya uwanja, wakitoa uzoefu na mwongozo kwa kizazi kipya.
Ni muhimu kutambua kuwa hatuna muda wa kutosha kufanya mabadiliko makubwa ya kikosi. Hivyo basi, tunapaswa kuboresha tulichonacho kwa njia sahihi. Moja ya njia hizo ni kuwalinda wachezaji wetu wachache tulionao kwa kuwasaidia kisaikolojia, hasa pale wanapopitia nyakati ngumu kwenye klabu zao. Hatuna wingi wa wachezaji wa kuchagua kiasi cha kuwaacha wengine na kuanza upya; muda hauturuhusu hilo.
Ni kweli kwamba wachezaji wanalelewa na klabu zao, lakini taifa pia lina malengo yake, kama ambavyo klabu zina malengo yao binafsi. Hivyo, kila mdau anapaswa kutimiza wajibu wake kuhakikisha mchezaji anakuwa tayari kulitumikia taifa. Iwapo klabu haitoi fursa ya kutosha kwa mchezaji, jukumu la taifa ni kumsaidia ndani na nje ya uwanja ili tusipoteze wapiganaji wetu.
Vilevile, mashabiki wana jukumu kubwa. Wanapaswa kuwafahamu wachezaji wa timu ya taifa, kuwapa heshima, upendo na sapoti itakayowafanya wajivunie kuitumikia nchi yao. Mchezaji wa Taifa Stars anapaswa kujiona mwenye fahari sawa na anavyojivunia kuichezea klabu kubwa nchini au nje ya nchi.
Kwa ujumla, AFCON 2025 ni kama kianzio kwa Taifa Stars na Tanzania kwa ujumla kwa ajili ya msingi na mwanzo wa safari mpya ya fainali za mwaka 2027.
Mafanikio ya baadaye yataamuliwa na maandalizi ya leo.