Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Stars ikikaza kidogo tu, Uganda inakaa

Muktasari:

  • Ndio, Stars iko katika michuano hiyo inayoshiriki kwa mara ya nne baada ya awali kucheza zile za 1980 zilipofanyikia Nigeria, kisha 2019 kule Misri na msimu uliopita 2023 kule Ivory Coast na kote huko haikufanya vizuri.

NI kweli Taifa Stars imeanza vibaya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa kupoteza mbele ya Nigeria. Ni kweli imeendeleza rekodi isiyovutia ya kutopata ushindi katika mechi za kwanza za michuano hiyo, lakini bado mashabiki wamekuwa na matumaini makubwa nayo.

Ndio, Stars iko katika michuano hiyo inayoshiriki kwa mara ya nne baada ya awali kucheza zile za 1980 zilipofanyikia Nigeria, kisha 2019 kule Misri na msimu uliopita 2023 kule Ivory Coast na kote huko haikufanya vizuri.

Mwaka 1980 ilianza na mguu mbaya kwa kufumuliwa mabao 3-1 na wenyeji Nigeria, kisha zile za Misri ilikumbana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Senegal na fainali zilizopita ilianza kwa kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Morocco kabla ya msimu huu kufungwa mabao 2-1 na Nigeria.

Kwa waliolifuatilia pambano hilo la Kundi C watakubaliana nami kwamba Stars ilicheza vizuri na kwa nidhamu ya hali ya juu, licha ya kushindwa kucheza kwa kasi na kutengeneza mashambulizi ambayo yangeweza kuwasumbua mabeki wa Nigeria.

Pengo la kiungo mshambuliaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi ya njano aliyopewa katika michuano iliyopita, lilikuwa wazi licha ya nyota wengine waliopewa nafasi na kocha Miguel Gamondi kupambana kadri ya uwezo wao na kuifanya Nigeria isiamini ilichokutana nacho.

Kama sio umakini mdogo hasa katika kipindi cha pili kwa wachezaji wa Stars kupoteza nafasi mbili za wazi za kupata mabao, huenda leo tungezungumza mengine.

Mbinu alizoingia nazo kocha Gamondi, ilikuwa ni silaha iliyoisaidia Stars kuepuka kipigo kizito kutoka kwa Nigeria na pongezi nyingi ziende kwa safu ya ulinzi kuanzi kipa Zuberi Foba, mabeki wa kati Bakar Mwamnyeto na Ibrahim Bacca, sambamba na wale wa pembeni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomary Kapombe pamoja na viungo Dismas Novatus na Alphonce Mabula.

Kila mmoja alicheza kwa nidhamu ya hali ya juu na umakini mkubwa hata kwa wale walioingia baadaye kuwapokea wenzao katika eneo hilo, lakini namna Stars nzima ilivyocheza kwa nidhamu, mbinu na kujituma imetoa picha kwamba bado ina nafasi kubwa ya kufanya maajabu katika fainali hizi.

Ni kweli Stars haijawahi kupata ushindi wowote katika michuano ya AFCON tangu 1980, lakini kwa jinsi timu ilivyotuonyesha soka mbele ya Nigeria na kupata bao kupitia kwa Charles M’Mombwa ni matumaini ya wengi kwamba kama itacheza hivyo hata kesho mbele ya Uganda mambo yatakuwa mazuri.

Uganda ambayo ilianza vibaya kwa kupoteza mabao 3-1 mbele ya Tunisia, sio timu nyepesi hata kama ilianza na kipigo hicho kizito.

Rekodi zinaonyesha ni moja ya timu zinazotusumbua kila mara tunapokutana nao katika mashindano tofauti, hivyo Stars ni lazima ishuke uwanjani kesho ikiwa na nidhamu ile ile iliyokuwa nayo mbele ua Nigeria ili iweke hai tumaini la kusonga mbele katika fainali hizo.

Hofu yangu ni kwamba isije ikatokea Stars iliyocheza kwa kujituma na nidhamu ya hali ya juu ikaingia kesho kwa kuichukulia poa Uganda kwa vile ni majirani zetu na kule kupoteza kwao mbele ya Tunisia kisha aibu ikatukuta.

Kwa wanaokumbuka fainali za Misri, Stars ilipotoka kufungwa 2-0 na Senegal iliingia kwa kuichukulia poa Kenya na kujikuta tukipoteza 3-2 na kutung’oa mapema michuanoni kabla hata hatujakutana na kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa waliokuja kuwa mabingwa wa fainali hizo, yaani Algeria.

Mbinu, nidhamu na upambanaji ule ule uliotumika mbele yua Super Eagles ndio unaopaswa kutumika pia kwa The Cranes kesho ili mambo yawe mepesi na kuweka historia mpya katika ushiriki wa Stars kawenye fainali za AFCON tangu zilipoasisiwa mwaka 1957.

Fainali zilizopita licha ya kufungwa mabao 3-0 na Morocco ambao safari hii ndio wenyeji, Stars ilijitutumua na kutoka sare mbili katika mechi mbili za mwisho kundini, tukipata sare ya 1-1 kwa Zambia kisha suluhu kwa DR Congo na kuvuna pointi mbili kwa mara ya kwanza michuanoni.

Hayo yalikuwa ni mafanikio makubwa baada ya fainali za Misri kushindwa kuambulia japo pointi moja kwa kupoteza mechi zote tatu, tofauti na fainali za kwanza kule Nigeria ambapo tulipoteza mbili mfululizo mbele ya Nigeria na Misri, lakini tikapata sare ya 1-1 kwa Ivory Coast.

Matokeo ya mechi za fainali zilizopita zitumike kama kichocheo cha kuhakikisha tunawabana Uganda kabla ya kumalizana na Tunisia katika mechi ya mwisho wiki ijayo na kuamua hatima ya kucheza 16-Bora Kama wachezaji wa Stars watazingatia kuwa, Watanzania wote wameweka matumaini yao kwao ni wazi watapambana na kutumia kila nafasi watakayotengeneza mbele ya Uganda ili kuwapa furaha na kuandika historia mpya AFCON kwa kupata ushindi wa kwanza michuanoni.

Kama iliweza katika Fainali za Kombe la Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 iliyofanyika kati ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kwa kushinda na kufika hadi robo fainali, sioni kwanini isiwezekane katika mechi zilizosalia huko Morocco. Kila kitu kinawezekana. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Taifa Stars. Aluta Continua.