Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwa hili la Taifa Stars, kuna mazuri zaidi yanakuja 2027

NONDO Pict


HISTORIA imeandikwa. Haijalishi imeandikwaje, lakini ni kwamba Tanzania imeandika historia ya kufuzu hatua ya 16 Bora kwa mara ya kwanza katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).


Ndio, tulianza kushiriki fainali za kwanza mwaka 1980 zilizofanyikia Nigeria, ambapo tulipoteza mechi mbili za awali mbele ya wenyeji waliokuja kubeba taji lao la kwanza mwaka huo kwa kutufunga mabao 3-1 kabla ya Misri kutuadhibu kwa mabao 2-1 kisha tukatoka sare ya 1-1 na Ivory Coast.


Fainali za pili tulizisubiri baada ya miaka 39 tukaenda Misri na pale tulitia aibu kwa kupoteza mechi zote tatu kwa kufungwa 2-0 na Senegal kisha kulala 3-2 kwa majirani zetu wa Kenya na kumalizika kwa kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Algeria waliolibeba taji hilo kwa kuifunga Senegal. Hii ilimaanisha Stars tulipangwa na wababe kwelikweli.

Mwaka 2023 fainali zilipofanyikia Ivory Coast angalau tulionyesha dalili za kuimarika kwa kupoteza mechi moja tu mbele ya Morocco kwa mabao 3-0 kisha tukatoka sre ya 1-1 na Zambia baada ya kushindwa kushikilia bomba, kwani tuliongoza kwa muda mrefu kabla ya Clatous Chama kututibulia na mwisho tulitoka suluhu na DR Congo.

NOND 01

Hata hivyo, msimu huu ukiwa ni wa 35 tangu michuano hiyo ya AFCON ilipoasisiwa mwaka 1957, tumeonyesha tofauti. Tulianza kwa kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Nigeria, kisha tukalazimishwa sare na Uganda baada ya kuwaongoza kwa muda mrefu na mwishowe tukaibana Tunisia na kutoka nayo sare ya bao 1-1.

Yalikuwa ni matokeo bora kwa Tanzania tangu tuanze kushiriki michuaano hiyo kwani ilitufanya tuvune pointi mbili na mabao matatu licha ya kufungwa manne, ikiwa ni tofauti na msimu uliopita tulipovuna pia pointi mbili, lakini tulifunga bao moja tu na kufungwa manne, ilihali Misri tulitoka kapa bila pointi na kufunga mabao mawili tu na kufungwa manane huku 1980 tulipata pointi moja na kufunga mabao matatu na kufungwa sita.

Matokeo hayo yametupa nafasi ya kutinga hatua ya 16 Bora kupitia washindwa bora tukiwapiku Angola ambao wamefunga mabao mawili, sisi tukifunga matatu na hivyo kupangwa sasa kukutana na wenyeji Morocco Jumapili hii.

NOND 02

Binafsi niwapongeze wachezaji kwa jinsi walivyopambana uwanjani kwa dakika zote 270, pia niliponngeze benchi la ufundi chini ya kocha Miguel Gamondi kwa kazi kubwa waliyofanya kimbinu kuweza kupata matokeo hayo na kuandika historia hiyo kwa mara ya kwanza barani Afrika.

Haya ni mafanikio makubwa baada ya awali Taifa Stars chini ya Hemed Suleiman ‘Morocco’ kuifikisha Tanzania hatua ya robo fainali ya Ubingwa wa nchi za Afrika (CHAN) 2024 zilizofanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ikiwa ni rekodi nyingine itakayoendelea kutambua mchango wa kocha huyo mzawa aliyeivusha pia timu hiyo kwenda katika fainali za AFCON 2025 kabla ya kuondolewa na kuteuliwa kwa Gamondi.

Hakuna shaka kwamba hii ni hatua kubwa na kuonyesha namna Tanzania tunazidi kukua kisoka, kwani tumetoka kuwa taifa linalopambana kupata nafasi ya kushiriki fainali hizo na sasa tunashindana, kwani tumerudi Morocco tukiwa kifua mbele tukiitazama michuano inayofuata kama sehemu ya mkakati wa kuonyesha kukua kwetu.

NOND 03

Ukiitazama timu kuanzia fainali za 33 hadi za sasa za 35, Stars imeonekana kukua kwa kila kitu kuanzia kimbinu na hata uchezaji wake, ndio maana kiasi cha ushindani ndani ya kiwanja kimekua na tofauti ukilinganisha mara zote tatu tulizoshiriki safari hii tunaweka historia ya kwenda hatua ya mtoano.

Kwangu mimi ni mapema ukilinganisha na ushiriki wetu na timu nyingine, kwani bado tulipaswa kufanya makubwa zaidi kwa namna mechi zote tatu tulivyocheza mbele ya Nigeria, Uganda na hata Tunisia.

Kama kungekuwa na utulivu mkubwa na kutumia nafasi tulizotengeneza sambamba na kuepuka makosa ya kizembe leo tungekuwa tunazungumza mengine. Stars imetuheshimisha.

Hata kama kuna watakaobeza kwamba tumefuzu kibahati, kwa kundi tulilokuwa na ushindani uliopo AFCON 2025 tuna haki ya kujisifia kwa tulichovuna.

NOND 04

Ni kweli kabisa, hatuna wachezaji wenye madaraja ya juu kulinganisha na mataifa mengine makubwa kisoka, lakini utaona kila siku ule umbali wa viwango vya kushindana uwanjani unapungua na hii inaletwa na kuimarika kimbinu kwa wachezaji wetu na benchi kwa ujumla.

Miaka ya nyuma makocha wenye maarifa walikuwa wanapata kazi kubwa kuwasiliana na wachezaji kimbinu  ukizingatia katika makuzi ya wachezaji wengi hawakuwa wanafundishwa zaidi ya kusimamiwa kufanya kile walichonacho.

Hakuna siri wachezaji wengi walikuwa wakifundishwa na makocha wahamasishaji zaidi bila kutoa maelekezo ya kina kuhusiana na mbinu kuuendea mchezo husika.

Hongera kwa Kurungenzi ya Ufundi ya Shirikisho la Soka (TFF) chini ya Oscar Mirambo kwa kuwekeza katika elimu kwa makocha wetu ambao ndio wanaishi na vijana muda mwingi, huku makocha wa timu ya taifa wakipata muda mchache na pia hata ule ugeni wa maelezo kimbinu umetoweka kwa kiasi kikubwa kutokana na maboresho hayo bila kusahau chachu ya makocha wa kigeni katika soka la Tanzania kwa ujumla kusaidia kuimarisha soka letu.

NOND 05

Leo hii ukiitazama Taifa Stars unaiona ikiwa na ufahamu mzuri na wakiwa na majibu ya maswali yanayoletwa na mchezo... namaanisha vile vipindi vitano vya mchezo kuna uelewa wa kutosha bila kujali daraja la mtekelezaji.

Nikisema vipindi vitano namaanisha timu ikiwa na mpira wachezaji wanaelewa majukumu na mahali wanapopaswa kuwepo ili kurahisisha timu iweze kucheza, lakini pia timu bila mpira kila mmoja anajua jukumu na mahali anapopaswa kuwapo kwa wakati husika.

Halafu kuna timu inapopoteza mpira utaona uharaka wa kila mmoja kufika anapopaswa kuwapo na timu inapopokonya mpira unaona kila mmoja akiwa anajua kinachofuata na anapopaswa kuwapo na tukio la mwisho ni mipira ya kutenga katika kushambulia na kuzuia.

Haya ndio maswali matano yanayoulizwa na mchezo kwa muda wote wa mchezo na hapa naona tumeimarika sana bila kujali ubora wa utekelezaji kinachotia moyo ni uwezo wa timu kuelewa swali na kujaribu kulijibu.

Inatia moyo kuziendea fainali zinazofuata ambazo sisi tutakuwa wenyeji sambamba na Kenya na Uganda kwani tayari tuna sehemu ya kuanzia nayo ni kufuzu hatua ya mtoano ya 16 Bora na kuendelea kama nafasi itakuwapo lakini hatutaenda tena kushiriki bali kushindana kutokana na uzoefu wa mara tatu mfululizo. Bravo Stars!