Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SPOTI MIKIKI: Ni nini kimewakuta vinara wa msimu uliopita?

Kimewakuta Pict

Muktasari:

  • Washindi wa tuzo za ubora za msimu uliopita wana hali mbaya sana hadi sasa kiasi kwamba akitokea mgeni na kuhadithiwa kwamba hiki anachokiona ndicho kilichokuwa bora kupita kawaida msimu uliopita, hawezi kuamini.

Tukiwa katika mzunguko wa 14 wa ligi kuu msimu wa 2024/25, mambo mengi yamekuwa kinyume sana na aidha matarajio au uhalisia kwa kulinganisha na msimu uliopita.

Washindi wa tuzo za ubora za msimu uliopita wana hali mbaya sana hadi sasa kiasi kwamba akitokea mgeni na kuhadithiwa kwamba hiki anachokiona ndicho kilichokuwa bora kupita kawaida msimu uliopita, hawezi kuamini.


1. MFUNGAJI BORA NA MCHEZAJI BORA

Stephane Aziz Ki ndiyo mfungaji bora wa msimu uliopita, na MVP. Alicheza dakika 2174 kwenye mechi 27 kati ya 30 ambazo timu yake ilicheza katika msimu mzima.

Alifunga mabao 21 na kutoa pasi 8 za mabao ikiwa na maana kwamba alihusika moja kwa moja katika mabao 29, katika ya 71 ambayo timu yake ilifunga. Hii ni sawa na asilimia 40.85.

Yanga 01

Aziz Ki akashinda tuzo ya mfungaji bora kwa mabao yake 21, na akashinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu kwa kiwango chake alichokionesha.

Lakini msimu huu hadi sasa hajaonyesha hata robo ya kiwango chake cha msimu uliopita.

 Ameshacheza dakika 760 kwenye mechi 11 huku akifunga bao moja pekee na kutoa pasi mbili tu za mabao.

Msimu uliopita katika mechi kama hizi, yaani 11, Aziz Ki alikuwa tayari ana mabao 7 na pasi mbili za mabao.

Lakini namba peke yake hazitoshi kuelezea ubora wa Aziz Ki msimu uliopita. Sanaa yake ya soka ilikuwa kubwa sana; ubunifu wa hali ya juu, uwezo binafsi na utengenezaji wa nafasi kubwa.

Yanga 02

Aziz Ki alikuwa na uwezo wa kupiga pasi yenye kufungua safu ya ulinzi ya wapinzani, hata kama hafungi bao au hatoi pasi ya kuzaa bao moja kwa moja.

Aliwatia hofu wapinzani na kulazimika kumfanyia madhambi mengi ambayo aidha yalichangia kadi zilizopunguza matumizi yao ya nguvu au mikwaju ya adhabu ndogo iliyopia faida Yanga.

Aziz Ki alikuwa anafanya mikimbio mingi katika eneo la hatari iliyowatawanya wapinzani na kusababisha akina Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli kupata nafasi za kufunga.

Lakini hayo yote msimu huu hakuna. Azzi Ki hakimbii tena uwanjani. Aziz Ki hana ubunifu na wala haleti hofu kwa wapinzani. Amekuwa mwepesi kukabika na kuzifanya safu za timu pinzani kucheza kwa uhuru mkubwa sana, nini kimebadilika kwake?


2. KIPA BORA

Ley Matampi Vumi wa Coastal Union ndiyo alikuwa kipa bora wa msimu uliopita. Raia huyo wa DRC na mshindi wa CHAN mwaka 2016, alicheza jumla ya mechi 24 kati ya 30 za timu yake, na kutoka na hati safi 15.

Aliruhusu mabao 11 tu kati ya mabao 19 ambayo timu yake ilifungwa kwa ujumla. Coastal Union ilimaliza ligi ikiwa imefungwa mabao machache zaidi kuliko timu mbili za juu yake, Simba (25) na Azam FC (21).

Yanga 03

Leyi Matampi aliisaidia Coastal Union kumaliza nafasi ya nne kwenye ligi, ambayo ni ya juu zaidi kwa timu hiyo tangu ishinde ubingwa wa bara mwaka 1988.

Matampi alikuwa bora sana, siyo tu kwa sababu ya hizi namba bali kazi yake uwanjani. Aliokoa michomo mingi sana ya wazi iliyoiweka salama timu yake katika mechi kadhaa na kuifanya ifuzu mashindano ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1989.

Coastal Union walishiriki Kombe la washindi mwaka 1989 baada ya kushika nafasi ya pili kwenye ligi ya Muungano.

Japo walishinda ubingwa wa bara mwaka 1988, lakini Coastal Union hawakufuzu moja kwa moja  mashindano ya Afrika kwa sababu wakati huo ligi ya bara haikuwa ligi rasmi.

Ligi rasmi ilikuwa ya Muungano ambao watani wao wa jadi, African Sports walishinda. Bingwa wa Ligi ya Muungano alishiriki klabu bingwa Afrika, mshindi wa pili alishiriki Kombe la Washindi, ndiyo ilivyokuwa kwa Coastal Union.

Yanga 01 (1)

Kwa hiyo okozi za mikono ya Matampi zikairudisha Coastal Union kwenye mashindano ya Afrika.

Lakini msimu huu mambo yamebadilika, Matampi siyo yule wa msimu uliopita na haishangazi klabu kuamua kuachana naye, kwa mujibu wa taarifa ya klabu iliyotolewa Desemba 10.

Hadi anaondoka, Matampi ametumia dakika 630 kusimama katikati ya milingoti miwili na chini ya mwamba mmoja wa lango la Coastal Union, zilizopatikana kwenye mechi 7.

Katika muda huo, ameruhusu mabao 7. Msimu uliopita alicheza mechi 24 na kuruhusu mabao 11, msimu huu ana mechi 7 na ameruhusu mabao 7, jionee tofauti!

Na siyo tu kuruhusu mabao, bali hafanyi tena zile okozi kama za msimu uliopita. Matampi amekuwa rahisi sana kufungika.


3. YANGA SC

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Bara ambao msimu uliopita walikuwa bora katika kila eneo la uwanja.

Walitwaa ubingwa kwa kuvuna jumla ya alama 80, ambazo ni nyingi zaidi kwa misimu ya ligi 16, tangu ianze msimu wa 2021/22.

Yanga 05

Kumpata bingwa aliyefikisha alama kama hizi inabidi urudi hadi msimu wa 2020/21, ambapo Simba walifikisha alama 83. Hata hivyo, wakati ule ligi ilikuwa na timu 18, siyo 16 kama sasa.

Kabla ya timu kuongezeka hadi 20 msimu wa 2017/18, mara ya mwisho ligi kuwa na timu 20 ilikuwa msimu wa 2016/17 ambapo bingwa aliishia alama 68 ambaye alikuwa Yanga.

Ligi yetu imekuwa na kawaida ya kuongeza au kupunguza idadi ya timu kwa miaka yote.

Lakini katika nyakati zote, hakuna bingwa aliyefikisha alama 80 kwenye msimu wa timu 16 ni Yanga tu msimu wa 2023/24.

Unaweza kuona Yanga walikuwa bora kiasi gani. Walifunga jumla ya mabao 71 ambayo ni mengi zaidi tangu ligi iwe na timu 16.

Yanga 06

Kumpata bingwa aliyefunga mabao mengi zaidi ya hayo inabidi urudi hadi msimu wa 2020/21 wakati ligi ilipokuwa na timu 18 ambapo Simba walifunga mabao 78.

Hakuna msimu wowote wenye timu 16, ambapo timu moja ilifunga mabao zaidi ya 70. Ni Yanga haohao ndiyo walifikisha mabao 70, msimu wa 2015/16, wakati wa ubora wa Amissi Tambwe ambaye alifunga maba 21 kama Aziz Ki msimu uliopita.


Unaweza kuona Yanga ya msimu uliopita ilivyokuwa.

Iliruhusu mabao 14 tu. Mara ya mwisho Yanga kuruhusu mabao machache zaidi ya haya ilikuwa msimu 2021/22, ilipookota kwenye nyavu mara 8 pekee.

Msimu mzima wa 2023/24 Yanga ilipoteza mechi mbili pekee,  zote za ugenini.

Lakini msimu huu mambo yamekuwa tofauti. Hadi sasa ikiwa imecheza mechi 11, imeshapoteza mbili na zote nyumbani, huku ikiruhusu mabao matano.

Tayari Yanga imeshafukuza kocha na bado haijaipata ile fomu yake. Kocha mpya Sead Ramovic amelalamika kwamba wachezaji hawako timamu kimwili.

Yaani ile Yanga iliyoonekana nondo msimu uliopita, Yanga ambayo kipindi cha pili ilikuwa ndo kama inaanza mechi…sasa hivi haina utimamu wa mwili, nini kimeikuta? Ama kwa hakika maisha hubadilika!