Song asimulia safari yake hadi Arsenal
ACHANA na zile kazi alizozifanya akiwa na klabu za Ulaya hususani England, kiungo Alex Song ameamua kutundika rasmi daluga akiwa kwenye ardhi aliyozaliwa ya Afrika.
Ndio, Novemba 15 mwaka huu, nyota huyo wa zamani wa Arsenal, Barcelona na West Ham, Alexandre Dimitri Song Billong ‘Alex Song’ alitangaza kustaafu soka kupitia ukurasa wake wa Instagram akiwa na umri wa miaka 36 akiitumikia timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Djibouti, Arta Solar7.
Mcameruni huyo aliyezaliwa katika Mji wa Douala mwaka 1987, alihudumu kama kiungo mkabaji na hata beki wa kati katika soka, akicheza soka la kulipwa kwa takriban miaka 19 tangu 2004 ndani ya klabu tisa tofauti.
Alipita klabu za Bastia ya Ufaransa, Arsenal, Charlton Athletic, Barcelona, West Ham United, Rubin Kazan, Sion, Sion II kabla ya hivi karibuni kurudi Afrika na kujiunga na Arta Solar7 iliyowahi kuweka kambi mara kadhaa jijini Dar es Salaam.
“Ni kwa huzuni kubwa wakati umefika wa mimi kutundika buti zangu, Safari yangu ilianza Yaounde nikiwa mtoto, nikicheza bila buti, miguu wazi na kwenye changarawe ngumu, ilinipa nguvu na ujasiri wa kufaulu.”
“Nilifikiri nimepata miujiza nilipohamia Ufaransa nikiichezea Bastia, ila ulikuwa mwanzo wa safari yangu ikiendelea kwenda Arsenal na Barcelona klabu kubwa Duniani,” aliandika.
Hata hivyo, Song amewashukuru wote walifanikisha safari yake ya soka tangu alipoanza hadi kustaafu huku akiwataja mke, watoto na mawakala wake.
“Watu wengi wamenisaidia njiani mke wangu, watoto wangu, familia, marafiki, mawakala wangu, makocha na hata wachezaji wenzangu, mashabiki wote nitawashukuru na nitawathamini milele.”
Mwandishi wa makala haya aliwahi kufanya mahojiano na mkali huyo na hapa ni sehemu ya aliyofunguka kuhusu yeye na soka lake kwa jumla hadi alipostaafu mwezi huu.
MTU WA MFANO
Anasema alihamasishwa kucheza soka na binamu yake Ronny Song ambaye alikuwa akicheza soka akiwa Cameroon na baada ya kukua alitamani kuwa kama kina Patric Vieira na Claude Makelele.
“Niliishi kwa mjomba wangu ambaye mwanaye alikuwa akicheza soka, alinifanya nitamani kuwa mwanasoka na baadae nilitamani kuwa kama kina Viera na Makelele, walinivutia sana.”
SOKA NA KITABU
Haikuwa rahisi kwa wazazi kukubali nicheze soka na kukataa masomo, hii ni kawaida kwa jamii zetu za Afrika lakini nilikuwa na maono yaliyonifanya nipambane, namshukuru Mungu nilifanikiwa,” alisema huku akiwashauri vijana kuzingatia masomo licha ya kucheza soka.
“Natamani kuwaambia vijana wenzangu ni vizuri kucheza soka lakini ni muhimu kuzingatia masomo kwa sababu sio kila mtu ana bahati na soka, mfano ukazingatia mpira na kuacha kusoma alafu usije kufanikiwa kama ulivyotarajia nini utakifanya baadae?”
UGUMU KWENDA ARSENAL
Anasema haikuwa rahisi kwenda Arsenal licha ya kuhitaji huduma yake kwani alitakiwa na klabu nyingine kubwa tu ulaya.
“Haikuwa rahisi mimi kwenda Arsenal kwani nilikuwa mdogo sana (miaka 17) na kila kitu kwa Arsenal kilikuwa kikubwa kuanzia timu yenyewe hadi wachezaji lakini nilichagua hapo kwa kuwa Wenger alikuwa akizungumza kifaransa na alihusudu vijana licha ya kuhitajika na klabu zingine,” alisema huku akiweka wazi kusajiliwa kwake ni kama ndoto yake ilikuwa imetimia kwani alitamani kucheza na wachezaji wakubwa kama kina Steven Gerrard na David Beckham ambao alikuwa akiwaona tu kwenye TV.
AMSHUKURU WENGER
Anasema anamshukuru sana Wenger kwa kuwa alimsaidia kutambua nini afanye na kwa wakati gani kwani Wenger alimwambia hatamani kumuona akinunua vitu vya kifahari kama magari (Ferrari) wakati tu aliposaini Arsenal kwani alikuwa na umri mdogo miaka 17.”
“Nilipofika arsenal niliwakuta wenzangu ni wakubwa na sikuwa nimeuzoea mji, Wenger aliniambia hatamani kuniona nanunua vitu vya bei ghali (ferarri) nikifuata maisha wanayoishi wenzangu bila kuchanganua mambo nitajikuta napoteza malengo, alikuwa kama baba kwangu,” alisema Song ambaye alihudumu Arsenal kwa miaka sita na alifanikiwa kushika nafasi ya pili katika mashindano ya EFL kwa sasa Carabao 2010-2011.
MAISHA YA BARCA
Anasema alijiunga na Barcelona 2012- 2016 kwanza kwa ajili ya pesa, pia kutamani kukidhi hamu yake ya kucheza kwenye klabu kubwa, licha ya kukidhi haja ya moyo wake maisha yake hayakuwa mazuri na ya muda mrefu kwenye kikosi hicho na alidumu kwa miaka miwii hadi kutolewa kwa mkopo kwenda West Ham 2014 na alitwaa ubingwa wa La liga msimu wa 2012-2013.
“Tunacheza kwa ajili ya kupata pesa, lakini kwenda Barcelona ilikuwa ni kukidhi haja ya moyo wangu ya kucheza vilabu vikubwa barani Ulaya, yalikuwa maisha mazuri lakini ya muda mfupi.”
“Licha ya mimi kwenda Barcelona mke wangu pamoja na wanangu hawakupendezwa kwa sababu tulienda kuanza maisha mapya nje ya London, lugha ilikuwa changamoto kwao hivyo hawakufurahishwa, siwezi kufanya vizuri kama familia yangu haina furaha, ndipo nilichukua uamuzi wa kwenda kwa mkopo West Ham ili familia ifurahi.”
ASICHOSAHAU
Licha ya kufanya vizuri huko Ufaransa na kujiunga Arsenal anasema hawezi kusahau mchezo wake wa kwanza akiwa na uzi wa Arsenal wa Ligi Kuu dhidi ya Fulham kwani hakuwa na mchezo mzuri na mashabiki hawakupendezwa naye siku hiyo.
“Sintasahau siku ya kwanza naanza kwenye kikosi cha Arsenal mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Fulham, sikufanya vizuri kwani sikutegemea kama ningeanza kwenye kikosi cha kwanza, hivyo nilikuwa na hofu sana, sikufanya vizuri na mashabiki hawakufurahishwa na mimi lakini kocha (Wenger) aliweka deni kwangu kwani aliwaambia mashabiki mnayemzomea leo atakuja kuwa bora zaidi mbeleni, Namshukuru Mungu ilikuwa kama alivyosema.”
Ameongeza hawezi kusahau mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona Februari 16, 2011 ambao walishinda 2-1 kwani hakuwahi kucheza mchezo wenye mashabiki wengi namna ile.
JEZI NAMBA 17
“Nilipendelea kuvaa jezi namba 17 licha ya kuwa kuna wakati haikuwezekana kwa sababu mbalimbali, lakini namba 17 ina maana sana kwangu, huwa inanikumbusha kuhusu familia yangu, kwetu tupo 28 lakini nina dada 17,” alisema Alex Song ambaye anakiri ni shabiki wa Arsenal maisha yake yote.
HATAMANI UKOCHA
Anasema yeye ni tofauti na malijendi wengi ambao wakimaliza soka hugeuka kuwa makocha, anatamani kuwasaidia vijana wadogo wenye malengo na soka licha ya hivyo tayari amenza kuwekeza katika majengo kwani anaamini katika hilo.
“Siwezi kuwa kocha ila nitaendelea kuhudumu kwenye soka kwa kuwasaidia vijana wadogo wenye malengo na mpira, hata hivyo wanangu ni wanasoka, nitawaelekeza wapi pa kupita, naamini pia katika uwekezaji wa majengo na tayari ninamiliki hoteli kwenye baadhi ya maeneo Afrika, nitasimamia hapo zaidi, alisema Song ambaye ana mke mmoja na ni baba wa watoto wawili, wa kiume Nolan na Kaylian.
Song katika ngazi ya timu ya taifa ya Cameroon ‘Simba Wasiofugika’ ameitumikia tangu akiwa na umri wa miaka 17, akicheza mechi tatu za U17, U23 amecheza tatu huku akicheza mechi 49 katika timu kubwa bila kufunga bao lolote, lakini akiweka rekodi mbalimbali, huku akicheza jumla ya mechi 331 kwa ngazi za klabu na kufunga mabao 12 hadi alipostaafu mwezi huu.