Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shalulile, mfalme wa mabao anayeishi kifahari

SHALULILE Pict

Muktasari:

  • Baada ya kuandika historia akiwa Mamelodi Sundowns, nyota huyo wa Namibia, 31, sasa analeta uzoefu wake Jangwani, huku akiwa miongoni mwa wachezaji waliolipwa vizuri zaidi katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL). Mafanikio yake yametokana na mshahara mkubwa, mikataba ya udhamini, biashara binafsi na uwekezaji alioufanya kwa miaka kadhaa.

MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Peter Shalulile amejiunga na mabingwa hao wa Tanzania akiwa na hadhi ya mmoja wa washambuliaji wakubwa kuwahi kutokea Afrika Kusini, si kwa mabao pekee bali pia kwa utajiri alioujenga ndani na nje ya uwanja.

Baada ya kuandika historia akiwa Mamelodi Sundowns, nyota huyo wa Namibia, 31, sasa analeta uzoefu wake Jangwani, huku akiwa miongoni mwa wachezaji waliolipwa vizuri zaidi katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL). Mafanikio yake yametokana na mshahara mkubwa, mikataba ya udhamini, biashara binafsi na uwekezaji alioufanya kwa miaka kadhaa.

Taarifa za usajili wake kutua Yanga, zimeripotiwa kwamba, Shalulile dau lake ni dola 700,000 (Sh1.9 bilioni)

SHALU 01

Utajiri wa kutosha

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, Shalulile anakadiriwa kuwa na utajiri wa takribani, kiasi kilichoongezeka kwa kasi tangu aliposajiliwa na Mamelodi Sundowns mwaka 2020.

Utajiri huo umetokana na mshahara wake, mikataba ya matangazo ya kibiashara, uwekezaji katika sekta ya hoteli, mali isiyohamishika (real estate), hisa pamoja na mapato anayopata kupitia shughuli mbalimbali za kimichezo na kijamii.


Mshahara mara mbili

Baada ya kuhamia Mamelodi Sundowns kutoka Highlands Park mwaka 2020, Shalulile alisaini mkataba wa miaka mitano uliokuja kuongezewa mwaka mmoja kuelekea msimu wa 2025/26.

Inaripotiwa mshambuliaji huyo alikuwa analipwa mshahara wa R400,000 (Sh65.2 milioni) kwa mwezi, mara mbili ya alichokuwa akilipwa Highlands Park ambako alikuwa akipokea takribani R200,000 (Sh32.6) kwa mwezi. Mbali na mshahara huo, alikuwa akipata bonasi mbalimbali kutokana na mafanikio ya timu na michuano aliyoshiriki.

SHALU 02

Mikataba minono ya udhamini

Umaarufu wa Shalulile umevutia makampuni makubwa duniani. Kwa sasa ni balozi wa Nike, huku akiwa aliwahi kufanya kampeni mbalimbali za Puma kati ya mwaka 2020 na 2021.

Mwaka 2022 alisaini makubaliano na Samsung kutangaza simu za Galaxy S22, dili linaloripotiwa kumuingizia takribani R10 milioni. Miaka miwili baadaye, mwaka 2024, aliteuliwa kuwa balozi wa chapa ya magari ya Volkswagen, hatua iliyoongeza zaidi thamani yake sokoni. Pia ameendelea kushirikiana na kampuni mbalimbali za Namibia na Afrika Kusini kupitia kampeni za matangazo.


Amewekeza kwenye biashara

Mbali na soka, Shalulile ameanza kujenga maisha ya baada ya kustaafu kwa kuwekeza katika sekta ya hoteli, biashara za mavazi, nyumba (real estate) pamoja na hisa. Ingawa hapendi kuweka wazi biashara zake, uwekezaji huo unatajwa kumuingizia mapato ya kudumu hata akiwa nje ya uwanja.

Aidha, amekuwa akialikwa mara kwa mara kwenye hafla na shughuli za kibiashara, huku baadhi ya taarifa zikieleza kuwa aliwahi kulipwa hadi R200,000 kwa mwonekano mmoja wa matangazo mwaka 2020, kiwango kinachoaminika kuongezeka kutokana na mafanikio yake ya hivi karibuni.

SHALU 03

Maisha ya kifahari

Shalulile pia anafurahia maisha ya kifahari nje ya uwanja. Anamiliki nyumba ya kisasa yenye thamani inayokadiriwa kufikia R20 milioni nchini Afrika Kusini, ikiwa na vyumba vitano vya kulala, bwawa la kuogelea, ukumbi mkubwa wa chakula, gym binafsi na maegesho mawili ya magari.

Pia anadaiwa kumiliki nyumba nyingine mjini Windhoek, Namibia.


Magari ya mamilioni

Kama ilivyo kwa mastaa wengi wa soka, Shalulile anapenda magari ya kifahari. Miongoni mwa magari anayomiliki ni Toyota Corolla, Hyundai Tucson na Hyundai Cresta yenye thamani ya takribani R408,500. Pia amewahi kuonekana akitumia Volkswagen TSI (2022) yenye thamani inayokadiriwa kufikia R479,900.


Safari yake hadi kuwa nyota

Shalulile alianza soka la ushindani akiwa Tura Magic FC nchini Namibia mwaka 2011 kabla ya kuhamia Highlands Park ya Afrika Kusini mwaka 2015.

Aliisaidia Highlands Park kupanda daraja hadi PSL mwaka 2016, kabla ya kumaliza msimu wa 2019/20 akiwa kinara wa mabao kwa kufunga mabao 16 sambamba na Gabadinho Mhango. Mwaka 2020 alisajiliwa na Mamelodi Sundowns kwa ada inayoripotiwa kufikia R30 milioni, hatua iliyobadilisha kabisa maisha yake ya soka na kumfanya kuwa mmoja wa washambuliaji hatari zaidi Afrika.

SHALU 04

Rekodi zinazomfanya kuwa miongoni mwa bora Afrika

Tangu ajiunge na Sundowns, Shalulile alifunga zaidi ya mabao 100 na kuisaidia klabu hiyo kutwaa mataji matano mfululizo ya PSL.

Katika kipindi hicho alitwaa ubingwa wa PSL mara tano, akawa Mfungaji Bora wa ligi mara tatu mfululizo (2020/21, 2021/22 na 2022/23), akanyakua tuzo ya Mchezaji Bora wa PSL 2020/21, Players' Player of the Year mara mbili, pamoja na kuwa Mfungaji Bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2023.

Aidha, alifikisha mabao 129, rekodi iliyomweka miongoni mwa wafungaji bora wa muda wote katika historia ya PSL.


Timu ya taifa

Kwa upande wa Namibia, Shalulile alicheza mechi yake ya kwanza mwaka 2014 na hadi sasa ameichezea nchi yake mara 67, akifunga mabao 17 huku akiwa nahodha wa Brave Warriors katika AFCON 2023.

Sasa akiwa Yanga, mashabiki wa mabingwa hao watakuwa na matumaini rekodi, uzoefu na makali aliyoyaonyesha kwa miaka mingi Afrika Kusini yatahamia pia kwenye Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa ya CAF.

Kwa Shalulile, mafanikio ya mchezaji wa kisasa hayapimwi kwa mabao pekee, bali pia namna anavyotumia umaarufu wake kujenga utajiri, kuwekeza na kujiandaa kwa maisha baada ya soka.


Mafanikio yake makubwa zaidi

Ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini mara tano

Mshindi wa Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu ya Afrika Kusini mara tatu

Mchezaji Bora wa Msimu wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini 2020-2021

Mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini