Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya wamachinga viwanja vya soka Afrika

KIJIWE Pict
KIJIWE Pict

Muktasari:

  • Siku moja mwaka 1983 nikiwa kwangu Dar es Salam nilipata simu saa mbili usiku muda mfupi baada ya kufika kutoka ofisini na kumuaga mhariri mtendaji, Ulli Mwambulukutu na kuwaachia wasaidizi wangu Stephen Rweikiza na Willie Chiwango kumalizia ukurasa wa michezo.

KILA nikifika Dar es Salaam, Tanga au Morogoro hujaribu kukutana na wachezaji wa kandanda niliokuwa nao kuanzia mwisho wa miaka ya 1960 hadi katikati ya miaka ya 1980.

Tunakumbushana yaliyotokea nyumbani na nje nilipokuwa nao kama mwandishi au kiongozi wa msafara kutokana na kuwa mhariri wa michezo Daily News na mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Siku moja mwaka 1983 nikiwa kwangu Dar es Salam nilipata simu saa mbili usiku muda mfupi baada ya kufika kutoka ofisini na kumuaga mhariri mtendaji, Ulli Mwambulukutu na kuwaachia wasaidizi wangu Stephen Rweikiza na Willie Chiwango kumalizia ukurasa wa michezo.

Simu ilikuwa ya katibu wa BMT, hayati Victor Mkodo aliyeniambia Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hayati Daudi Mwakawago ananitafuta. Nilipouliza kulikuwa na nini aliniambia Mwalimu Julius Nyerere amepokea mwaliko kutoka kwa Rais Jean-Baptise Bagaza wa Burundi akitaka timu ya taifa ya kandanda iende Burundi kushiriki sherehe za mapinduzi.

Aliniambia BMT ilimshauri waziri na kukubali mimi niongoze msafara kama mjumbe wa BMT. Kutokana na muda wa safari kuwa chini ya saa 48 nilimwambia haiwezekani kwa sababu sio rahisi kuwakusanya wachezaji kwa saa chache kutokana na matatizo ya usafiri na mawasiliano wakati ule.

Nilimwambia Mohammed Chuma alikuwa Mtwara, kipa Omar Mahadhi na wenzake Omari Zimbwe na Mwabuda walikuwa Tanga na wachezaji wengine waliokuwepo Mwanza, Shinyanga, Morogoro na Zanzibar. Nilishauri iende Yanga iliyokuwa klabu bingwa kwa vile ni rahisi kupata wachezaji kwa kuwa walikuwepo Dar es Salaam na wamekuwa na mazoezi ya pamoja.

Tuliondoka na ndege ya Air Tanzania hadi Bujumbura ambapo mapigano yalikuwa nje ya mji mkuu wa nchi hiyo. Tulipofika ilikuwa tabu kuamini nchi ilikuwa katika vita na kwani hali ilikuwa ya kawaida katika mji mkuu. Baada ya mapumziko mafupi nilifanya mkutano na wachezaji na kuwaeleza nchi ilikuwa haina usalama kuwataka wachukue tahadhari na wasitoke usiku.

Msaidizi wangu wa msafara, Kenneth Mbeyela wa Iringa ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa FAT na kocha Ray Gama pia waliwaasa wachezaji kuwa waangalifu. Tulipanga kufanya mazoezi mepesi jioni na siku ya pili wacheze, lakini niliposhuka chini katika hoteli ili twende kwenye mazoezi nilipewa taarifa baadhi ya wachezaji hawapo.

KIJ 01

Baadaye walikuja wakiwa na mitumba ya nguo, viatu, sabuni za kuogea, dawa ya meno na vitu vingine. Wakati ule vitu hivyo ilikuwa tabu kupatikana nyumbani. Nilichoelewa baadaye ni kwamba walikuwepo wachezaji walioyajua maeneo yanayouzwa mitumba kwa vile walishafika Bujumbura kabla na walikuwa na marafiki.

Katika miaka ya karibuni nilipokwenda Bujumbura kufundisha waandishi wa habari masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki niligundua maeneo yaliyotumiwa kuuza mitumba yamejengwa maduka na kupewa vijana kufanyia biashara. Tulipokwenda kufanya mazoezi tulikuta wauza mitumba wanawasubiri wachezaji wa Yanga na nililazimika kuwaomba polisi kuwatimua ili kocha Gama aongoze mazoezi.

Kumbe makubwa - kuhusu mitumba ilikuwa inatungojea siku ya pili tulipocheza na Burundi. Mpaka mapumziko hakuna timu iliyoweza kutikisa wavu wa mwenzake. Filimbi ya mapumziko ilipopulizwa niliondoka jukwaa kuu na kwenda chumba cha wachezaji. Huko nilikuta makubwa kuliko niliyoyaona Togo na Ghana nilipokuwa mwandishi wa Daily News nikifanya kazi na gazeti la serikali la Daily Graphic mwaka 1975 na 1976.

Wauza mitumba waliingia katika chumba cha wachezaji wa Yanga kuuza bidhaa na Gama alikuwa na tabu ya kuwataka waondoke. Ilibidi kuwaomba polisi na wanajeshi kusaidia. Wachezaji wawili waliniomba niwahifadhie mitumba waliyonunua mpaka mwisho wa mchezo. Niliwaambia hilo haliwezekani kwa sababu watu wasingeelewa kumuona kiongozi wa msafara anarudi kwenye jukwaa na mitumba mkononi.

Mchezo ulimalizika tukiwa tumeshinda mabao 2-1 na aliyekuwa balozi wetu Burundi, Hussein Makwaiya alifurahi sana.

KIJ 02

Kwangu furaha ya ushindi na sare tuliporudiana na Burundi na ushindi wa michezo miwili ya kirafiki na klabu iligubikwa na burudani ya kuona biashara ya mitumba ikifanywa chumba cha wachezaji.

Hili hulikumbuka ninaposimulia enzi za michezo za miaka iliyopita na ninapokutana na wachezaji wa Yanga waliokuwa katika ule msafara kicheko hutawala mazungumzo. Hadi leo najiuliza je itafika siku wamachinga hapa kwetu wataingia vyumba vya wachezaji na waamuzi kuuza mitumba, vyerahani na majokufu au wamachinga kwenda kwenye jukwaa la waheshimiwa kuwauzia mitumba?

Nimezungumzia vyerahani na majokufu kwa sababu nilipokuwa Afrika Magharibi niliona makubwa. Ghana niliona biashara za barabarani zinazoendeshwa na vijana waliotumwa na kinamama wanaoitwa Makola Women yaani wanawake wa Soko la Makola na wageni, hasa Walebanoni na Wafaransa zikiwa na maajabu yake.

Vijana walihangaika jua lilipochomoza hadi saa sita usiku wakitembeza bidhaa mikononi na kichwani na wachache walitumia baiskeli na mkokoteni. Wasichana walitembea mitaani na masufuria na sinia za chakula kichwani, hasa ugali wa mahindi (banku), mchanganyiko wa viazi vikuu, ndizi na mihogo (fufuu) na wali.

Wakati ule biashara aina hii ilikuwa haijashamiri nyumbani, bali walikuwepo Waarabu wa kabila la Wamahara waliouza nguo na vitambaa kwa kupita majumbani hasa Upanga, Kariakoo na Jangwani jijini Dar es Salaam. Wiki chache baada ya kufika Ghana nilikwenda Lome mji mkuu wa Togo - kama kilomita 80 kutoka Accra. Kilichonipeleka ni kuandika habari za mchezo wa Klabu Bingwa Afrika kati ya Hafia ya Guinea na klabu moja ya hapo.

Mwamuzi alikuwa kaka ambaye kwa miaka mingi niliishi naye jirani Zanzibar, Musa Bakari. Washika vibendera walikuwa Abdul Kawambwa wa Morogoro na Kulwa Nassor wa Jeshi la Polisi. Nilipokwenda uwanjani nilivamiwa na 'wamachinga' waliotaka kuniuzia kitambaa cha kufutia jasho, nguo mpya na mitumba na mmoja alikuwa amebeba cherehani kichwani na miengine jokofu dogo begani.

Nilipowaangalia aliyebeba jokofu aliniambia: "You go want to buy. It is cheap. I swear this is gift from God" (unataka kununua. Ni rahisi. Ninaapa hii ni zawadi kutoka kwa Mungu). Wakati wa mapumziko nilimwita anayeuza jokofu na kwenda naye chumba cha waamuzi na kumwambia Musa alinunue na ningemsaidia kulipeleka Zanzibar kama zawadi.

Musa ambaye alikuwa mwingi wa utani aliniambia: "Salim wewe ni mwendawazimu au hashashi (mvuta bangi). Kama hao jamaa wanaobeba jokofu na cherehani na kuuza katika viwanja vya mpira." Nilimpa yule 'machinga' cedi (fedha za Ghana) mbili  kununua soda na kumwambia bahati mbaya rafiki yangu alikuwa hana uwezo wa kulinunua. Kijana aliondoka akitabasamu na kuniambia Mekhsi (ahsante kwa lugha ya Kifaransa). Nimesimulia haya kuonyesha wamachinga katika nchi nyingine wanavyochukulia viwanja vya kandanda kama eneo la biashara.