Simulizi ya Pendeza: Ndoto ya Jeshi Ilivyomuingiza Kwenye Ngumi
Muktasari:
- Kwenye ngumi za kulipwa, Pendeza alicheza mapambano kadhaa ya ushindani mkubwa, akisafiri na kupambana, huku akionyesha uwezo mkubwa wa kiufundi. Changamoto za kifedha, uchache wa mapromota, na ukosefu wa bima kwa wakati huo zilimfanya yeye na wenzake kupitia mazingira magumu ya kimaisha na kimichezo.
KATIKA mchezo wa ngumi nchini majina yanakuja na kuondoka, lakini yapo yanayobaki kwenye kumbukumbu kutokana na mchango wake katika kukuza mchezo huo na kuandaa mabondia wa kizazi kipya. Miongoni mwa watu waliochagua kuendeleza safari yao katika ngumi hata baada ya kuachana na maisha ya kupanda ulingoni ni Kocha Athuman Pendeza, ambaye historia yake inaunganisha maisha ya ubondia na jukumu la kulea vipaji.
ALIPOANZIA
Safari ya Pendeza ilianza miaka ya 1990, wakati alipoingia katika ngumi za ridhaa, maarufu kama amacha. Katika kipindi hicho, alikuwa akijifunza misingi ya mchezo huo akijenga uwezo wa kupambana na kujitengenezea uzoefu ambao baadaye ungekuwa msingi wa safari yake ya ukocha.
Hii ni simulizi ya safari ya Kocha Athuman Pendeza, kuanzia miaka yake ya ubondia wa ridhaa hadi kuingia kwenye ukocha.
Ni historia inayofungua ukurasa wa mchango wake katika ngumi za Tanzania, uzoefu alioubeba kutoka ulingoni na nafasi anayocheza katika kuendeleza kizazi kipya cha mabondia kupitia Boca Boxing Club.
Alianza kujifunza misingi ya mchezo huo kwa kumaanisha. Haikuwa rahisi katika kipindi hicho, kwani miaka ya 1995 hadi 1997 ilikuwa ni kipindi ambacho ngumi za amacha zilikuwa na ushindani mkubwa, zikiwa na changamoto za kiuchumi na ukosefu wa miundombinu rafiki ya mazoezi.
Mwaka 1997, akiwa na kiu ya mafanikio, alifanikiwa kuingia rasmi kushiriki mashindano ya ridhaa (amacha). Katika mashindano hayo, alipambana vikali na kufanikiwa kucheza michezo mingi, kufika fainali, na hata kushinda medali za dhahabu, jambo lililomjengea msingi imara wa kisaikolojia na kiufundi.
“Safari yangu ya ngumi ilianza mwaka 1995 ndio nilianza ngumi rasmi kujifunza na mwaka 1997 rasmi niliingia kushiriki mashindano ya ridhaa, nikimaanisha mashindano ya amacha,” anasimulia Kocha Pendeza.
Lengo kuu la Pendeza wakati huo halikuwa tu kupigana burudani, bali ilikuwa ni njia ya kupata fursa ya kujiunga na jeshi kupitia michezo lengo ambalo lilikuwa ndoto ya vijana wengi waliokuwa wakishiriki ngumi za amacha. Ingawa haikuwa rahisi, alitumia ngumi kama ngazi ya kujitangaza na kutafuta mustakabali wake wa maisha.
MITIHANI YA ULINGONI
Baada ya kupambana kwenye ngumi za ridhaa kwa mafanikio, hatua iliyofuata ilikuwa ni kuvuka mpaka na kuingia kwenye ngumi za kulipwa. Hata hivyo, kama ilivyo kwa mabondia wengi wa zamani, kipindi hicho kilikuwa na changamoto nyingi za kimaslahi na kukosekana kwa usimamizi mzuri wa kazi zao.
Kwenye ngumi za kulipwa, Pendeza alicheza mapambano kadhaa ya ushindani mkubwa, akisafiri na kupambana, huku akionyesha uwezo mkubwa wa kiufundi. Changamoto za kifedha, uchache wa mapromota, na ukosefu wa bima kwa wakati huo zilimfanya yeye na wenzake kupitia mazingira magumu ya kimaisha na kimichezo.
“Wakati sisi tunacheza hakukuwa na fedha nyingi kama sasa ambayvo bondia anaweza kuondoka hadi na Milioni 30, wakati ule ili utoboe ilibidi ujiunge na jeshi ndio maana mabondia wengi wa zamani walikuwa wanajeshi,” anasema Pendeza
KUHAMIA KWENYE UKOCHA
Baada ya kupitia ulingoni na kushuhudia changamoto zinazowakumba vijana wengi wanaochipuka, Pendeza aliamua kuchukua uamuzi wa kuingia kwenye fani ya ukocha. Akiwa na mwenzake, Kocha Salum Lusasi, walianzisha mfumo imara wa kuwasimamia, kuwalea, na kuwafundisha vijana wadogo wanaotaka kuingia kwenye ulimwengu wa ngumi kupitia klabu yao ya Boca Boxing Club.
Kocha Pendeza anaweka wazi kuwa makocha wa sasa wanapaswa kutambua tofauti kubwa iliyopo kati ya ngumi za zamani na za sasa, ambapo kwa sasa mabondia wanahitaji zaidi nidhamu ya kisaikolojia, elimu ya mchezo, na usimamizi wa karibu.
“Mimi na mwenzangu Salum Lusasi tuliangalia usawa wa sasa hivi na usawa wa zamani ni tofauti jinsi ambavyo sisi tulivyokuwa tunafundishwa, tulivyokuwa tunajisimamia, hatuwezi kuenda kipindi ambacho tulikuwa tunachofanya sisi na kipindi ambacho wanafunzi wa sasa hivi,” anasema.
MAFANIKIO NA URITHI
Chini ya mikono ya Pendeza na Kocha Salum Lusasi, Boca Boxing Club imeweza kuibua na kulea mabondia wengi wakubwa ambao wamefanya vizuri ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, akiwemo hayati Chibumburi, Mustafa Mpasi, Miss Maya, Frank Nyisian, na Shomari Pendeza.
Pendeza anasisitiza kuwa mafanikio ya bondia hayawezi kupatikana bila kuwa na usimamizi mzuri wa klabu, nidhamu ya hali ya juu, na uwepo wa mifumo ya kisheria kama vile bima za afya zinazotolewa na Chama cha Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) ili kuwalinda mabondia wanapopata majeraha au wanapostaafu.
“Changamoto kubwa ya mabondia ni bima ya afya kwa sababu hutaweza kukimbia masuala ya kupimwa na ngumi ni vitu vinavyoendana, hivyo ikisimamiwa vizuri tunaweza kuzalisha mabondia wengi wazuri na wenye afya,” anasema.
Pendeza anaendelea kusimama kama nguzo kuu ya mafanikio katika ngumi za Tanzania, akitumia uzoefu wake wa miongo kadhaa kuunda mabondia watakaopeperusha bendera ya nchi kimataifa.