Simulizi ya kusisimua bondia mwanamke aliyestaafu majuzi
Muktasari:
- Na hivi karibuni msichana akiwa na miaka 40, bingwa wa dunia mara tano wa ngumi upande wa wanawake, mshindi wa medali ya dhahabu ya Olimpiki na bingwa wa dunia asiye na mpinzani katika uzito wa lightweight na super-lightweight alishuka uwanjani Croke Park, Ireland kwa ajili ya pambano la mwisho la maisha yake ya ndondi, huku watu 82,000 wakishuhudia.
COUNTY WICKLOW, IRELAND: Kuna jambo la kuvutia sana kuhusu namna simulizi ya bondia maarufu wa Ireland, Katie Taylor ilivyofikia mwisho, kwani miaka 30 iliyopita akiwa msichana mdogo kutoka Bray alilazimika kuficha nywele zake chini ya kinga ya kichwa na kujifanya mvulana ili tu aweze kushiriki mchezo alioupenda.
Na hivi karibuni msichana akiwa na miaka 40, bingwa wa dunia mara tano wa ngumi upande wa wanawake, mshindi wa medali ya dhahabu ya Olimpiki na bingwa wa dunia asiye na mpinzani katika uzito wa lightweight na super-lightweight alishuka uwanjani Croke Park, Ireland kwa ajili ya pambano la mwisho la maisha yake ya ndondi, huku watu 82,000 wakishuhudia.
MWISHO WA SAFARI?
Taylor anakiri kwamba huo ndio mwisho ambao alikuwa akiota siku zote na hapa anasema: “Kwa kweli, baada ya pambano la mwisho dhidi ya Serrano nilisema hakuna kitu kinachoweza kuwa kikubwa kuliko MSG, hivyo nilifikiri nitaweka tu glovu zangu pembeni. Kitu pekee ambacho kingeweza kuwa kikubwa kuliko MSG ni Croke Park, lakini hilo lilionekana kuwa jambo lisilowezekana.
“Kwa hiyo nilipopigiwa simu na kuambiwa kwamba kweli pambano hilo lingefanyika, sikuamini. Nilifurahi sana na niliguswa sana. Huu ndio ukweli wa mwisho wa hadithi nzuri niliokuwa nikiutafuta.”
ALIANZA ANZAJE?
Taylor ametumia maisha yake yote kufuatilia mambo yaliyoonekana kutowezekana, akiwa na miaka 10 alianza ndondi pamoja na baba yake Peter, bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu Ireland, lakini wasichana hawakuruhusiwa kushindana. Hivyo akatafuta njia tofauti.
Na katika hilo aliamua kujifanya mvulana na kupigana kila mahali alipoweza. Wakati ndondi za wanawake ziliporuhusiwa rasmi nchini Ireland, Taylor aliandika historia kwa kushiriki pambano la kwanza la wanawake lililotambuliwa rasmi nchini humo 2001.
Kilichofuata kilikuwa zaidi ya ndoto ambazo hata yule msichana mdogo mwenye msimamo mkali asingeweza kufikiria; medali ya dhahabu ya Olimpiki London 2012, mataji matano ya dunia, mataji sita ya Ulaya, ubingwa usio na mpinzani katika uzito wa lightweight na super-lightweight pamoja na usiku wa kihistoria katika Ukumbi Madison Square Garden, Marekani ambako mabondia wengi hutamani kupigana hapo.
Hata hivyo, chini ya furaha hiyo ukweli ni kwamba huu ni mwisho, na alipoulizwa kuhusu kutembea mara ya mwisho kwenda ulingoni, kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo kwa mara ya mwisho na kujua kwamba hakutakuwa tena na kambi nyingine ya maandalizi ya pambano, Taylor aliguswa kihisia.
“Unanifanya niwe hisia sana,” anacheka huku akijaribu kuzuia machozi. “Ndiyo, ni... ninajaribu kutokuwa na hisia sana, lakini hata kuzungumzia tu jambo hili naanza kubanwa koo. Kila kitu sasa kinaanza kuwa halisi, kwa kweli. Nipe dakika moja tu.”
Baada ya kujikusanya anaendelea: “Ni lazima bila shaka nidhibiti hisia zangu kwa sababu nina kazi muhimu sana ya kufanya. Na ninajaribu kutotafakari sana safari yote kwa sababu kweli lazima niingie ulingoni na kufanya kazi yangu, na jambo muhimu zaidi ni kwamba mkono wangu uinuliwe.
“Lakini mara kwa mara huwa nafikiria kuhusu hilo na huwa ninaguswa kihisia. Nimetoa maisha yangu yote kwa mchezo huu na ndio kila kitu nachokijua na nachokipenda, hivyo wazo la kutofanya tena linaumiza, lakini lazima nijikite katika kutofikiria sana. Pia ni mchezo hatari sana kupeleka mwili wako ulingoni huku moyo wako ukiwa nje... ukifikiria kuhusu kustaafu.
“Na kiakili, nadhani maisha ya mwanamichezo ni maisha yaliyojaa kujitoa, na mara nyingi kinachopotea kutokana na kujitoa huko ni mahusiano. Siyo mara zote huwa hivyo, lakini kwangu ilikuwa hivyo. Niliona ni vigumu kuzingatia mahusiano wakati nilikuwa katikati ya nyakati hizi ngumu na za kushangaza katika maisha yangu ya kikazi.
Kwa hiyo nadhani huu ndio wakati sahihi wa kuondoka. Sasa nitapata nafasi ya kuwekeza katika ndoa, kuelekeza nguvu huko na kufurahia matunda ya kazi yangu. Kisha anatoa utani wake wa kawaida akisema: “Pia nitasubiri kwa hamu kutopigwa tena usoni. Haifanyi mambo kuwa rahisi kwamba sijui kabisa jinsi ya kupigana na kusogea.”
NINI KINAFUATA?
Lakini urithi mkubwa wa Taylor hautapimwa kwa mikanda aliyoshinda. Anapotazama nyuma, anakumbuka waliomsaidia kutengeneza njia kina Laila Ali, Christy Martin, Lucia Rijker, Ann Wolfe na shujaa wake wa utotoni, Deirdre Gogarty, lakini pia anaelewa maana ya safari yake mwenyewe.
“Nataka nikumbukwe kama bondia mkubwa, lakini pia nadhani jambo moja ambalo nataka nikumbukwe nalo ni kwamba niliuacha mchezo wangu ukiwa katika hali bora kuliko nilivyoukuta,” anasema.
“Nadhani hiyo ndiyo labda fahari kubwa zaidi katika maisha yangu yote ya kikazi, kuhamasisha kizazi kipya cha mabondia wanawake vijana, na kuona kila ukumbi wa ndondi nchini ukiwa umejaa mabondia wanawake ambao hawapiti katika changamoto zilezile au vikwazo vilevile nilivyopitia mimi.”
Taylor hajui hasa nini kitafuata baada ya hapo, ingawa hawezi kufikiria kujitenga kabisa na ndondi. “Nimekuwa nikihusika na ndondi kwa miaka 30 ya maisha yangu, hivyo nadhani itakuwa jambo la ajabu kuondoka tu na kutokuwa na nafasi yoyote ya kushiriki,” anasema.
“Naupenda mchezo wangu, na napenda mazingira ya ukumbi wa ndondi. Na nadhani hilo ni jambo ambalo nitaendelea kuhusika nalo siku zote, lakini kwa sasa natazamia kufurahia tu maisha yangu.
“Nimekuwa nikicheza ndondi tangu nilipokuwa na miaka 10 au 11. Imekuwa safari ngumu na yenye kuchosha. Imekuwa safari ya ajabu, lakini pia imekuwa ngumu sana. Na natazamia kutohisi tena presha ya mapambano, presha ya matarajio na kutolazimika tena kujiandaa kwa mapambano haya makali, bali kufurahia tu maisha kwa mabadiliko.
“Imekuwa mzigo pia kwa familia yangu. Hata maisha ya ndugu zangu yalipangwa kulingana na ratiba yangu ya mazoezi nilipokuwa nikikua kutokana na ndoto yangu ya Olimpiki. Napotazama nyuma naona jinsi walivyokuwa na msaada mkubwa na wa ajabu. Kama ningekuwa katika nafasi yao ningekuwa na uchungu kwa sababu maisha yao yalinizunguka mimi na ratiba yangu. Kwa hiyo, itakuwa vizuri sasa kufurahia maisha pamoja.”