Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kayange: Kilichonikuta Sauzi kimenifunza mengi

KAYANGE Pict

Muktasari:

  • Egine Kayange, bondia wa ngumi za kulipwa nchini kutoka mkoani Mbeya ambaye kwa sasa anaishi Mabibo Mwembeni, Dar es Salaam, ni mwanamke aliyethibitisha kuwa mchezo wa ngumi haujaumbwa kwa ajili ya wanaume pekee.

UKIMUONA mtaani au ukisikia sauti yake nyororo wakati anazungumza ni vigumu kuamini kuwa mikono yake imebeba uzito wa makonde yanayoweza kumuangusha mtu chini kwa pigo moja la ‘knockout’ (KO).

Egine Kayange, bondia wa ngumi za kulipwa nchini kutoka mkoani Mbeya ambaye kwa sasa anaishi Mabibo Mwembeni, Dar es Salaam, ni mwanamke aliyethibitisha kuwa mchezo wa ngumi haujaumbwa kwa ajili ya wanaume pekee.

Egine si bondia wa kawaida; ni mwanamichezo aliyevuka vikwazo vingi vya kimaisha na kimfumo ili kujenga jina lake katika ulingo wa ngumi za kulipwa nchini na kimataifa.

Mwanaspoti lilifanya mahojiano maalumu na mwanadada huyo anayesimamiwa na kocha Master Kinyogoli ambapo alifunguka kuhusu safari yake, changamoto alizokutana nazo, na maono yake katika mchezo huo.


KAYA 04

MUZIKI HADI NGUMI

Kabla ya kuvaa glavu na kuingia ulingoni kuonyeshana kazi na mabondia wengine,  Kayange alikuwa akijishughulisha na sanaa ya muziki wa Bongo Fleva, Michiriku, na ngoma za asili.

 Alikuwa na sauti nzuri na kipaji cha uimbaji ambacho kilimfanya kufanya kazi na watayarishaji mbalimbali wa muziki.

“Kabla ya kuja Dar nilikuwa naishi Bagamoyo ambapo ndio kuna makundi mengi ya vipaji kwahiyo nilikuwa naimba kwenye hivyo vikundi lakini kwa sasa nimeacha ila wenzangu huwa wananisihi sana kurudi kwenye muziki lakini maisha hayo magumu,” anasema Kayange.


KAYA 08

ALIINGIAJE KWENYE NGUMI

Bondia huyo anasema alikuwa anapenda kufanya mazoezi kabla hata hajaingia kwenye ngumi lakini kocha Sharifu Muhsini alimshawishi na kuanza kumfundisha na kumpa pambano la kwanza dhidi ya mdogo wake Habiba Pengo.

“Mimi nilikuwa napenda sana mazoezi tangu kitambo. Sharifu aliponiona nafanya mazoezi bichi, aliniambia anaona kitu ndani yangu na kunishawishi nianze kwenda gym kwake,” anasimulia Kayange.

Kati ya mwaka 2015 na 2017,  Kayange alianza kupata mafunzo rasmi ya ngumi na kupata pambano lake la kwanza dhidi ya Habiba Pengo, pambano aliloshinda na kuanza rasmi safari yake katika mchezo wa ngumi za kulipwa.

Ingawa wazazi na baadhi ya watu wa karibu walikuwa na hofu kuhusu maamuzi yake ya kuingia kwenye mchezo huo hatari, Kayange aliamua kuweka pembeni muziki na kujikita ulingoni.


KAYA 07

AFRIKA KUSINI NA FUNZO

Moja ya matukio yaliyowahi kutikisa kazi ya Kayange ni safari yake ya Afrika Kusini mwaka 2024 akiwa na bondia mwenzake Jesca Mfinanga.

Safari hiyo iliyojaa matumaini iligeuka kuwa mtihani mkubwa baada ya kukumbana na changamoto za uzito, mazingira magumu ya pambano, na kucheleweshewa malipo yao.

Egine anaeleza kuwa changamoto hiyo ilitokana na mratibu wa pambano (matchmaker) aliyewapeleka huko bila kuhakikisha maslahi na mikataba yao inalindwa kikamilifu kabla ya kuingia ulingoni.

KAYA 05

“Ilinifundisha somo kubwa sana. Nimejifunza kwamba katika nchi za nje au michezo ya kimataifa, huwezi kumwamini kila mtu. Lazima uhakikishe mikataba yako imenyooka kabisa. Tunamshukuru Balozi wetu wa Tanzania  nchini Afrika Kusini, James Bwana wakati huo, na serikali ya Awamu ya sasa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuingilia kati hadi tukapata haki zetu,” anasema Kayange.

Uzoefu huo ulimfanya bondia huyo kuwa makini zaidi na sasa mara nyingi huchagua kusafiri na kusimamia mambo yake mwenyewe au kuhakikisha mikataba ipo wazi kabla ya kupanda ulingoni.


KAYA 06

REKODI

Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la Ngumi la WPF na rekodi za kimataifa, Kayange ana rekodi ya mapambano 12 ya ushindi, mapambano 9 ya kupoteza, na ushindi wa KO 8. Licha ya rekodi hiyo nzuri, Kayange bado anahisi ana deni kubwa kwenye mchezo huo.

Moja ya mapambano yaliyomuumiza zaidi ni pambano lake la kuwania mkanda wa WPF huko Dubai dhidi ya Angelina Lucas kutoka Kazakhstan, ambapo alipoteza kwa KO.

Kayange anaeleza kuwa alipoteza pambano hilo kutokana na changamoto za kiafya alizozipata mara baada ya kukata uzito kabla ya pambano.

KAYA 09

“Nilipofika kule, mazingira ya chakula na maji yaliniletea shida ya tumbo. Nilianza kuharisha na kuumwa ghafla baada ya kukata uzito. Nilitaka nisicheze, lakini mazingira yalinilazimu kupanda ulingoni. Iliniumiza sana kwa sababu nilikuwa nimejiandaa vyema,” anafunguka.

Hata hivyo, anaeleza kuwa deni lake kubwa la taaluma ni kuja kurudiana (rematch) na bondia yeyote aliyewahi kumfunga nchini Tanzania au kimataifa.


KAYA 05

THAMANI MABONDIA WANAWAKE

Kayange anasema kuna tofauti ya kimaslahi na kithamani kati ya mabondia wa kiume na wa kike nchini Tanzania. Anafichua kuwa ingawa ngumi za wanawake zimeanza kupata mashabiki na mwamko mkubwa, bado kuna pengo kubwa la kifedha.

“Mabondia wa kiume wanaweza kucheza pambano la raundi 10 wakalipwa Sh20 milioni au zaidi. Lakini bondia wa kike anayecheza raundi hizo hizo 10 anaweza kupewa milioni 2 au milioni 3. Hiyo inatuvunja moyo sana kwa sababu sote tunavuja jasho na kufanya mazoezi magumu,” anasema Kayange.

“Promota akitaka kukulipa kidogo ukikataa, anachukua bondia mwingine anayekubali fedha ndogo kwa sababu hana msimamo lakini letu lingekuwa moja wasingekuwa wanatupa pesa kidogo kiasi hiko,” anasisitiza.

KAYA 03

Anatoa wito kwa waandaaji wa mapambano (promoters) na mashirikisho ya ngumi kuweka usawa na kutoa fursa kwa mapambano ya wanawake kupewa kipaumbele kama mechi kuu (main card) badala ya kuwekwa kama mechi za utangulizi tu.


KAYA 02

MAISHA NJE YA ULINGO

Nje ya ulingo wa ngumi, Kayange ni mama wa mtoto mmoja wa kiume na pia ni mjasiriamali anayejishughulisha na ushonaji wa nguo za kike na za kiume baada ya kusomea ufundi chokaa na ushonaji. Anaishi maisha ya kawaida na ya amani na majirani zake katika mtaa wa Mabibo tofauti na watu wanavyomfikiria.

Akizungumzia mitazamo ya jamii kwamba mabondia wanawake ni wakorofi au hawana tabia njema, Kayange alipinga jambo hilo.  “Mchezaji aliyeiva vizuri katika ngumi hawezi kupigana mtaani. Sisi ni wapole sana uraiani. Nidhamu ndiyo nguzo kuu ya mchezo wetu. Huko ulingoni ni kazi yetu, lakini uraiani sisi ni wanawake, akina mama, na walezi katika jamii,” anasema.

Kayange ana imani kuwa kwa sapoti inayoongezeka kutoka kwa serikali, wadau, na mashabiki, ngumi za wanawake nchini Tanzania zitafika mbali na kuleta mikanda mingi zaidi ya dunia.

Katika mafanikio makubwa aliyoyapata, Kayange anasema amepigana nchi tofauti na pesa aliyoipata kwenye mapambano hayo imemsaidia kujenga nyumba yake iliyopo Gongo la Mboto na anamiliki viwanja zaidi ya viwili.