Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Yanga hii ndo nafasi yenu sasa

NONDO Pict


KUMALIZIKA kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) iliyokuwa ikifanyika Morocco na kushuhudiwa Senegal ikibeba ubingwa, kumetoa nafasi ya kurejea kwa michuano ya CAF ngazi ya klabu kwa hatua ya makundi iliyokuwa imesimama tangu Desemba mwaka jana.


Katika michuano hiyo ya CAF, Tanzania inawakilishwa na klabu nne za Simba, Yanga zilizopo Ligi ya Mabingwa, ilihali Azam FC na Singida Black Stars zikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika zikiwa makundi tofauti na kila moja ikiwa imepata matokeo tofauti kwa mechi za awali.


Kurejea kwa michuano hiyo kunazifanya klabu hizo kukaa mguu sawa kwa mechi za raundi ya tatu za makundi yao wikiendi hii, ikianza Yanga leo Ijumaa kisha kesho Jumamosi kuwa zamu ya Simba huku Azam na Singida zenyewe zitashuka uwanjani keshokutwa kusaka pointi muhimu.

Katika mechi za raundi mbili za awali Yanga ilishinda moja na nyingine kutoka sare na kuvuna pointi nne ikiwa Kundi B ikilingana na Al Ahly ya Misri wanaovaana nao jioni ya leo mjini Alexandria, wakati Simba iliyopo Kundi D ilipoteza mechi zote na kuifanya iburuze mkia katika kundi hilo.

Yenyewe itashuka uwanjani kesho kuvaana na Esperance ya Tunisia kusaka pointi tatu za kwanza kama ilivyo kwa Azam itakayokuwa pia ugenini Nairobi, Kenya dhidi ya Nairobi United, huku Singida yenye pointi moja katika Kundi C baada ya kutoka sare moja na kupoteza mechi moja itakuwa nyumbani Zanzibar kukabiliana na AS Otoho d’Oyo ya Congo.

NOND 01

Hizi ni mechi ngumu kwa timu zote nne za Tanzania bila kujali kama zipo ugenini au nyumbani, kutokana na ukweli matokeo mazuri kwa timu hizo wikiendi hii itakuwa na maana kubwa kwa zile za marudiano wiki ijayo kwani zitaumana na wapinzani wao hao hao.

Matokeo ya mechi za awali yamezifanya timu hizo za Tanzania kuwa katika mtataziko juu ya hatma ya kwenda robo fainali, lakini sasa zina nafasi ya kurekebisha makosa na kuthibitisha ubora ilizonazo, pia ubora wa Ligi Kuu Bara iliyo nafasi tano za juu Afrika.

Bahati nzuri ni klabu hizo zinarudi katika michuano hiyo kila moja ikiwa imetoka kuongeza nguvu vikosi hivyo kupitia dirisha dogo la usajili lililo wazi hadi Januari 30, Yanga ikitambulisha nyota mpya ikiwamo Allan Okello kutoka Uganda na Depu aliyekuwa akicheza Poland, japo ni raia wa Angola, mbali na kipa Hussein Masalanga, Mohamed Damaro na Emmanuel Mwanengo.

NOND 02

Kwa upande wa Simba yenyewe imesajili nyota wapya akiwamo kipa Tanja Djibrilla Kassali, Libasse Gueye, Ismael Toure, Nickson Kibabage na Clatous Chama, ilihali Azam ikiwa na Aimar Abubakar ‘Haaland’, huku Singida ikiwa na kina Steven Mboni, Abdallah Said ‘Lanzo’, Abdulmalik Zakaria na Abdallah Kheri ‘Sabo’.

Hii ina maana maingizo mapya yataongeza kitu kwa vikosi hivyo na huenda vikapata matokeo bora zaidi kuliko ya mechi mbili za awali, lakini hilo haliwezi kutokea kama wachezaji hawatashuka uwanjani kwa kucheza na nidhamu na kujituma zaidi.

Mechi mbili za Simba dhidi ya Esperance ni muhimu zaidi kwa wababe hao wa Tanzania wenye rekodi tamu katika michuano ya CAFD ili kufufua tumaini na kucheza tena robo fainali, lakini kurejesha furaha na amani kwa mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo.

NOND 03

Msimu huu Simba imekuwa tofauti na hata katika matokeo ya mechi za raundi ya awali kulinganisha na mafanikio iliyo nayo katika michuano, hali inayonyong’onyesha wanasimba waliozoea raha, kwani katika tatu za awali za nyumbani timu hiyo haijashinda.

Ilitoka sare ya 1-1 na Gaborone United katika raundi ya kwanza, kisha kutoka suluhu na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini raundi ya pili kabla ya kupoteza 1-0 mbele ya Petro Atletico ya Angola hatuia ya makundi.

Hii ni tofauti na misimu kadhaa nyuma ambapo wapinzani walikuwa wkaihofia kuja kucheza na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwani ilikuwa ikitumika ile slogani ya ‘Kwa Mkapa hatoki mtu’ na wapinzani walifia Kwa Mkapa katika mechi za CAF.

Kuna mambo yaliyochangia hali hiyo, ikiwamo mabadiliko ya wachezaji na benchi la ufundi mara kwa mara ni sehemu nyingine ya udhaifu inayopunguza imani kwa mashabiki na wanachama japo mpira unatoa nafasi sawa kwa timu zote uwanjani. Hapo ndipo yalipo matumaini pekee ya Simba kusonga mbele na umuhimu wa mechi hizo mbili zijazo.

NOND 04

Kwa Yanga yenyewe ina hadithi tofauti, kwani ushindi wa 1-0 nyumbani dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco kisha kutoka suluhu ugenini mbele ya JS Kabylie ya Algeria imewapa morali hata wachezaji wakiamini wataendeleza rekodi nzuri dhidi ya Al Ahly.

Yanga kama zilivyo timu nyingine za Tanzania haijawahi kupata ushindi dhidi ya Al Ahly ikiwa kwao, lakini kwa aina ya matokeo na kikosi ilichonacho ni wakati muafaka leo kuthibitisha ubora mbele ya wababe hao wa soka la Afrika.

Matokeo mazuri leo huko Alexandria na ile ya marudio itaiweka Yanga pazuri katika mbio za kuisaka robo fainali nyingine ya michuano hiyo baada ya msimu uliopita kuchemsha na kuishia tu makundi.

Kwa Azam na Singida nazo zina kazi kubwa ya kuibeba Tanzania katika Kombe la Shirikisho kama ilivyo kwa Simba na Yanga zilizopo Ligi ya Mabingwa, kwani matokeo mazuri kwao yatafufua nafasi ya kuandika historia nyingine katika michuano hiyo.

Azam na Singida iunacheza makundi kwa mara ya kwanza, lakini kuvuna pointi dhidi ya AS Otoho na Nairobi United kupitia mechi mbili za nyumbani na ugenini kisha kupambana kupata matokeo mazuri kwa wapinzani wao wengine itakuwa na maana kubwa kwa klabu hizo.

Sio kuongeza pointi katika makundi waliyopo, lakini itathibitisha Tanzania kuingiza timu nne kwa mpigo hakukuwa kwa bahati mbaya, ila ni ubiorta na uwezo wa klabu hizo na ubora wa Ligi Kuu Bara.

Hivyo, kila timu ikijiandaa kushuka uwanjani wikiendi hii ni lazima ijue kuwa ina kazi kubwa ya kupeperusha bendera ya Tanzania, lakini kuthibitisha kuwa soka letu kwa sasa limepita hatua na sio lile lililokuwa la kusindikiza mataifa mengine.

Imani yangu ni makocha wa timu zote pamoja na wachezaji wameshamaliza kazi katika kupeana mbinu na mipango dhidi ya wapinzani wao hao, lakini timu zitacheza kwa kujua zikiteleza kuanzia sasa zitajiweka pabaya tofauti na tumaini la walio wengi.

Wachezaji wajue kabisa huu ni wakati wa kuonyesha uwezo wa vipaji vyao kwa kupambana kwa jasho na damu na kujituma kutafuta matokeo mazuri bila kujali timu hizo zinacheza wapi, pia hata wao wenyewe watakuwa wanajiweka sokoni mbele ya maskauti wa nje.

Watanzania wapo pamoja na timu hizo na kuziombea kila la kheri wikiendi hii na hata wiki ijayo zitakaporudiana na wapinzani wao hao, ili kuhakikisha zote zinapata matokeo mazuri na kujiweka pazuri kutoboa kwenda robo, kwani hilo linawezekana. Kazi kwao!