Prime
Dirisha dogo ni mtego, msisajili kwa mihemko
KLABU mbalimbali za soka nchini zipo bize kwa ajili ya kuliwahi dirisha dogo la usajili lililo wazi tangu Januari Mosi na likitarajiwa kufungwa mwishoni mwa mwezi huu.
Dirisha hilo limepangwa kufungwa Januari 30, wakati mechi za michuano mbalimbali ikiendelea na klabu zikiwa zinataka kulitumia kuimarisha vikosi vyao baada ya awali kubaini dosari katika mechi kadhaa zilizochezwa tangu msimu ulipozinduliwa Septemba mwaka jana.
Dirisha hili la usajili la Januari ni makhsusi kwa ajili ya kutumiwa na klabu kujiimarisha kutokana na upungufu uliojitokeza katika dirisha kubwa la Julai na hii ni baada ya kufanya tathmini kulingana na malengo yaliyokuwepo kabla ya kuanza msimu mpya.
Kitaalamu hili siyo dirisha la kujenga timu kutokana na muda uliopo kimashindano ni kipindi cha maboresho ya kikosi na hapo ndipo benchi la ufundi na mabosi wa klabu wanapopaswa kutumia akili za ziada kufanya usajili badala ya kuendeshwa na mihemko na kutafuta sifa tu.
Ukitazama kitaalamu usajili wa dirisha kubwa ambalo huwa kati ya Julai na Agosti huwa ndilo la kujenga timu na ndilo linalobeba malengo ya timu kwa msimu mpya kutokana na muda unaopatikana.
Klabu hususan makocha hupata muda wa maandalizi (pre season) zinazowapa nafasi kujua cha kufanya kwa kuijenga timu katika maeneo yote matano kuanzia utimamu wa mwili, utimamu wa akili, kimbinu, ufundi na kijamii.
Katika dirisha hili lenye muda mrefu wa maandalizi na mipango ya msimu mpya, ikitokea timu ikishindwa kufanikiwa mipango yake, ndipo sasa hutumia dirisha dogo la Januari kutatua changamoto zao.
Baadhi ya klabu sajili mpya za dirisha kubwa zimeshindwa kufikia matarajio, hivyo kulazimika kurudi sokoni kipindi hiki ili kufukia mashimo kwa mapengo waliyoyabaini tangu msimu kuanza kwa timu kucheza mechi za mashindano mbalimbali ikiwamo Ligi Kuu.
Tumeona usajili uliofanywa na Yanga dirisha kubwa ambao walikuwa wanakiimarisha kikosi hicho kwa kujazia baadhi ya nafasi walizoachwa wazi kwa kuondoka wachezaji kama Stephane Aziz Ki, Khalid Aucho, Clatous Chama na kadhalika.
Ndipo tuliposhuhudia ujio wa kina Mohamed Doumbia, Moussa Balla Conte, Andy Boyeli na wengine ambao hata hivyo umeshindwa kufikia matarajio na kujikuta ikiendelea kukitegemea kikosi walichomaliza nacho msimu uliopita.
Faida kwa Yanga ni walikuwa na timu bora iliyohitaji kuongezewa ubora kwa kiasi kidogo kulinganisha na baadhi ya klabu nyingine, japo kuna baadhi ya wachezaji sasa wanalazimika kupelekwa timu zingine kuboresha viwango vyao.
Kama wataonekana wanafanya vizuri kinachowafanya waonekane kawaida ni madaraja walioweka wachezaji kwenye kikosi hicho, wanaweza kurudishwa tena klabuni hapo.
Sio Yanga tu, hata Simba na Azam FC nazo zilifanya usajili dirisha kubwa na bado kuna walioshindwa kwenda na kasi na mipango ya timu na mabosi pamoja na benchi la ufundi limeamua kurudi tena sokoni ili kuboresha maeneo yaliyolegalega mambo yaendelee kunyooka.
Nakumbuka tulikuwa na mjadala kuhusu usajili mpya na tija katika baadhi ya klabu za Ligi Kuu baada ya kuviona vikosi vyao hasa wale wanaogombea ubingwa.
Wengi waliamini Simba imefanikiwa dirisha hilo kulinganisha na klabu nyingine, lakini kwa mtazamo wangu niliona tofauti na kuwaambia, ndiyo inavyoonekana hivyo kwa sababu Simba nafasi ziko wazi na timu iko katika kujengwa.
Ila ni usajili wa kawaida kama utachukua wachezaji hao na kuwafanya wachezaji wa Yanga na hata hawa wanaoonekana Yanga wanacheza kawaida, lakini kama wakienda Simba wanaweza kuonekana tofauti kutokana na uhitaji.
Kuna tofauti ya uhitaji katika kujenga timu na kuongeza ubora, hata ukiwatazama Azam FC, kuna namna unaona bado iko vilevile kutokana na maingizo mapya kushindwa kuongeza ubora kwa kikosi kilichomaliza msimu uliopita hasa wachezaji wa kigeni.
Ndiyo maana nazikumbusha klabu hizo, ni lazima zitumie vizuri dirisha hili kuboresha vikosi vyao. Siyo dirisha la kuongeza tu idadi ya wachezaji na kufanya majaribio bali ni la kutatua changamoto.
Viongozi na hasa wanaosimamia usajili wakishirikiana na makocha au benchi la ufundi ni lazima wafanye usajili huu kwa faida na malengo na sio mihemko au kutafuta sifa, kwani kosa lolote litakalofanywa litakula kwao mazima kwa vile dirisha hili ni la kuboresha tu!
Pia, lazima wajue hili siyo dirisha la kujenga timu, pia ni ngumu kupata mchezaji wa kutumika moja kwa moja kuleta faida kama hakuna umakini na uangalifu wa kiwango cha juu. Hakuna muda wa kumsubiri mchezaji azoee wakati mechi za mashindano zikiendelea. Kazi kwenu!