Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba v Yanga miaka 60 ya Uhuru

Simba v Yanga miaka 60 ya Uhuru

KAMA utani vile. Tanzania Bara imetimiza Miaka 60. Ndio, juzi Alhamisi ilikuwa kilele cha Miaka 60 tangu Tanganyika kupata uhuru wake kutoka kwa Wakoloni. Tanganyika ilipata uhuru wake Desemba 9, 1961 kutoka kwa Uingereza kisha mwaka mmoja baadaye ikawa Jamhuri na Aprili 26, 1964 iliungana na Zanzibar na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tanganyika ikawa Tanzania Bara ya leo.

Miaka 60 ni mingi kwelikweli. Kwa maisha ya binadamu, miaka 60 ni umri mkubwa kiasi cha mtu kuitwa mzee.

Achana na shamrashamra na shughuli mbalimbali zilizofanyika katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru, kwa upande wa soka, mchezo unaopendwa kwa asilimia kubwa na Watanzania uhuru huo una maana kubwa kwao.

Soka limehusika kwa kiwango kikubwa katika mafanikio ya Tanganyika kupata uhuru wake. Utabisha nini, wakati Simba na Yanga zimehusika kwa kiwango kikubwa kuupigania uhuru huo?

Kama hujui, ni kwamba wakati Tanganyika (Tanzania Bara ya sasa) ikipata Uhuru wake, Simba na Yanga zilikuwa tayari zina umri wa miaka kati ya 25 na 26, Wekundu wa Msimbazi klabu yao ikizaliwa 1936 na wakati wa Uhuru ilikuwa ikitimiza miaka 25.

Kwa watani wao, Yanga, ilikuwa ikitimiza miaka 26, kwani klabu hii ilianzishwa 1935, japo inadaiwa ilizaliwa mapema zaidi (1929) ila ilisajiliwa na kutambulika mwaka huo.

Pia zipo klabu nyingine kongwe nchini zilizoasisiwa kabla ya Uhuru wa Tanganyika, ikiwamo Coastal Union (1948) na African Sports (1936) zote za jijini Tanga ukiachilia klabu nyingine kadhaa zilizotapakaa kuanzia jijini Dar es Salaam hadi mikoani.

Hata hivyo, Simba na Yanga, klabu pinzani na watani wa jadi wa soka la Tanzania ya leo zimekuwa zikitajwa kuhusika kwa kiasi kikubwa kushiriki katika harakati za Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara ya sasa).

Mwanaspoti linakuletea historia na baadhi ya mafanikio sambamba na matukio mengine ya kusisimua yaliyojiri ndani ya klabu hizo katika safari yao nzima ndani ya kipindi miaka 60 ya Uhuru huo wa Tanganyika (Tanzania Bara). Endelea...!


WAASISI WA LIGI

Simba na Yanga ndizo klabu sita za kwanza kuasisi Ligi ya Bara, ambayo kwa sasa ni maarufu kama Ligi Kuu Bara inayodhaminiwa na Azam Media, GSM, TBC na NBC.

Ligi ya Bara iliasisiwa mwaka 1965 ikifahamika kama Ligi ya Taifa na ilishirikisha klabu sita tu.

Yapo madai mengine kuwa ligi hiyo iliasisiwa mwaka 1963 kabla ya kutambuliwa rasmi miaka miwili baadaye yaani 1965 kwa kushirikisha timu hizo sita, zikiwa pia ndizo klabu zilioasisi Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam (Mzizima) iliyoanza mwaka 1944.

Mbali na Simba na Yanga nyingine zilikuwa ni Tobacco au Sigara (Pwani), Coastal Union na Manchester United (Tanga) na TPC (Moshi).

Simba na Yanga ndizo timu pekee ambazo zimedumu muda mrefu kwenye ligi hiyo bila kuwahi kusuka daraja. Tangu zilipoasisiwa zimekuwa zikishiriki ligi hiyo iliyobadilishwa na kuwa Ligi Daraja la Kwanza miaka ya 1970 kisha mwaka 1997 kubadilishwa tena na Ligi Kuu Bara baada ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kuingia kuidhamini.


WABABE KILA KONA

Katika kipindi cha miaka 56 tangu kuasisiwa kwa ligi hiyo ya Bara, Simba na Yanga zimekuwa ndio wababe kwa kulibeba taji mara nyingi zaidi kuliko klabu nyingine.

Simba, inayoshikilia rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kubeba ubingwa wa ligi hiyo kwa kufanya hivyo 1965 na kutetea tena mwaka 1966 imetwaa jumla ya mataji 22, yakiwamo manne iliyoyabeba mfululizo mbele ya watani wao.

Taji la kwanza la Simba ilitwaa bila kutokwa jasho kwani Yanga iliugomea mchezo kabla mwamuzi hajaumaliza katika dakika ya 80 kwa madai ya kuwepo kwa giza, huku vijana wa Jangwani wakiongoza kwa bao 1-0.

Simba v Yanga miaka 60 ya Uhuru

Chama cha Soka nchini kipindi hicho, FAT (sasa Shirikisho la Soka (TFF), kiliagiza mchezo huo urudiwe upya ili kupata bingwa na Yanga waliendelea kugoma wakitaka wapewe ubingwa kwa vile ulivunjika wakiongoza, lakini FAT ikawapa Simba ubingwa.

Licha ya Simba kuwa mabingwa wa kwanza na kutetea taji mwaka 1966, lakini rekodi zinaonyesha kuwa, Yanga ndio baba lao kwenye Ligi ya Bara, kwani katika kipindi chote cha Uhuru wa Tanzania Bara, klabu hiyo imebeba jumla ya mataji 27.

Yanga imebeba mataji yake katika misimu ya mwaka 1968, 1969,1970, 1971, 1972,1974, 1981, 1983,1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2007-2008, 2008-2009, 2010-2011, 2012-2013, 2014-2015, 2015-2016 na 2016-2017.

Watani zao, yaani Simba mataji yake 22 iliyabeba katika misimu ya 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004 na 2007 (Ligi Ndogo).

Pia ilifanya hivyo katika misimu ya mwaka 2010, 2012, 2017-2018, 2018-2019, 2019-2021, 2020-2021.


ZENYEWE KWA ZENYEWE

Ukiacha ubabe wao katika Ligi Kuu Bara, Simba na Yanga ndani ya miaka 60 ya Uhuru na Miaka 56 ya ligi hiyo zimekutana mara 106, huku Yanga ikiwa kinara wa kugawa dozi kwa wapinzani wao.

Katika mechi hizo 106, Yanga imeshinda mara 38, huku Simba ikishinda mara 31 na mechi nyingine zikimalizika kwa sare mbalimbali zikiwamo zile za kusisimua za mwaka 1996 zilipofungana mabao 4-4 jijini Arusha na 2013 zilipotoka mabao 3-3.

Yanga ndio ilikuwa klabu ya kwanza kugawa dozi nene kwa watani wao Simba kwa kuwafumua mabao 5-0 katika mechi iliyopigwa Juni 1, 1968, lakini wakajibiwa mapigo kwa kusambaratishwa kwa mabao 6-0 Julai 19, 1977, kipigo kilichoshuhudiwa ikifungwa hat trick ya kwanza na ya pekee baina ya timu hiyo katika Kariakoo Derby.

Hat trick hiyo iliyofungwa na Abdallah ‘King’ Kibadeni, kisha Simba ikaja kuitesa tena Yanga katika mechi ya msimu wa 2011-2012 walipoilaza kwa mabao 5-0 katika mechi ya ovyo kuwahi kupigwa baina yao iliyochezwa Mei 6, 2012.

Katika mechi zote za watani, pambano la mwaka 1974 lililopigwa kwenye Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza na Yanga kushinda kwa mabao 2-1 ndilo linalotajwa la kusisimua zaidi kwa namna soka lililopigwa na matukio ya kustaajabisha yaliyojiri.

Kabla ya pambano hilo timu zote zilienda kuweka kambi zao nje ya Tanzania, Simba ikijichimbia Poland na Yanga ikienda Brazil na kubahatika kuonana na Pele, nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Brazili na klabu ya Santos.

Hilo ndilo pambano pekee lililochezwa kwa dakika 120 na matokeo yakaipa Yanga ubingwa kwa ushindi wa 2-1, pia katika pambano hilo kipa wa Yanga, Elias Michael na mshambuliaji wa Simba, Willy Mwaijibe waligongana na wote kuwahishwa hospitali ya Bugando.

Baadhi ya waliohudhuria pambano hilo ambalo mgeni rasmi alikuwa Meja Jenerali S.H. Sarakikya wanadai lilikuwa na watazamaji takribani 50, huku eneo ambalo mchezaji wa Simba, Saad Ali alianguka na kupoteza fahamu inaelezwa kuliota kichuguu.

Saad alizirai kwa kupigwa na kombora zito la mpira uliopigwa na Gibson Sembuli mfungaji wa bao la kusawazisha katika mchezo huo baada ya Adam Sabu kuitanguliza Simba na bao la ushindi likafungwa na Sunday Manara dakika saba ya awali ya muda wa nyongeza wa dakika 30.

Simba na Yanga pia zimewahi kukimbiana uwanjani mara kadhaa katika mechi za ligi, huku Msimbazi wakiwa vinara kwa kuwakacha Yanga mara nyingi.


MAKOMBE MENGINE

Katika kipindi cha Miaka 60 ya Uhuru, Simba na Yanga mbali na kugawana taji la Ligi Kuu Bara, lakini wamekuwa wakikimbiza hata kwenye michuano mingine mbali na ligi, ikiwamo Ligi Kuu ya Muungano iliyofutika kwa sasa, Kombe la FA (sasa ASFC), Kombe la Nyerere, Kombe la Mapinduzi, Kombe la Hedex na Kombe la Tusker.

Katika Ligi Kuu ya Muungano iliyokufa rasmi 2004 baada ya Zanzibar kutambuliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Yanga ndio baba lao kwa kutwaa mara nyingi taji hilo, ikifanya hivyo mara sita ikibeba mwaka 1983, 1987, 1991, 1996, 1997 na 2000.

Simba ililibeba taji hilo mara tano, ikishika nafasi ya pili nyuma ya Yanga na ikifanya hivyo mwaka 1993, 1994, 1995, 2001 na 2002.

Kwa upande wa Kombe la Nyerere, Simba imebeba mara tatu 1984, 1995 na 2000, wakati Yanga pia imelitwaa mara tatu 1975, 1994 na 1999 na kwa Kombe la FA, Yanga imelibeba mara tano, ikiwa kinara ikifuatiwa na Simba iliyobeba mara nne, 1995, 2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021.

Katika Kombe la Tusker Simba ndio vinara wakilibeba mara nne, 2001, 2002, 2003 na 2005, huku Yanga ikifuatia ikibeba mara mbili 2007 na 2009.

Klabu hizo pia zimegawana pia Ngao za Jamii, Kombe la Hedex, Kombe la AICC na Mapinduzi Cup linaloshikiliwa kwa sasa na Yanga baada ya Januari 13 mwaka huu kuifumua Simba kwa mikwaju ya penalti mjini Unguja, Zanzibar.

Kifupi ni kwamba Simba na Yanga kwenye ishu ya mataji, zimekuwa zikishindana kubeba kadri wanapopata nafasi, kwani wakiingia kwenye michuano huwa hawaachi kitu, japo kwa mara tatu walikwama kubeba Kombe la Sportpesa Super Cup.

Inaendelea kesho.

Kwa maoni tuandikie SMS au WHATSAPP kupitia namba:

0658 376 417