Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba na Warundi ni damudamu!

NI ukweli usiopingika, soka la Tanzania limekuwa kivutio kwa nyota wa kigeni tangu miaka ya 1970 hadi leo, ikishuhudiwa mastaa mbalimbali kutoka mataifa tofauti wakimiminika kuja kucheza nchini.
Utabisha nini, wakati Fredy Mayaula Mayoni kutoka Zaire (DR Congo ya sasa) alikipiga Yanga 1970 na kubahatika kufunga mara mbili kwenye pambano la Kariakoo Derby  alipoizamisha Simba kwa 2-1.
Huyu ndiye mchezaji wa kwanza wa kigeni kucheza soka la kulipwa nchini, kabla ya kugeukia muziki na kupata umaarufu mkubwa duniani. Kwa sasa ni marehemu.
Makocha wakubwa wa kigeni kutoka barani Ulaya, Latin America sambamba na wa nchi za Kiafrika wamekuwa wakiingia na kutoka nchini tangu miaka hiyo hadi leo kwa ajili ya kufundisha klabu mbalimbali na timu za taifa, kuthibitisha soka la Tanzania linaeleweka nje ya mipaka.
Profesa Victor Stansleascu kutoka Romania, Tambwe Leya kutoka Zaire (sasa DR Congo) na Nabi Kamala (Guinea) walikuja kufundisha Simba na Yanga miaka ya 1970 kisha kutuatiwa na wengine, huku pia ikishuhudiwa wachezaji mahiri kutoka nje wakimimbika zaidi miaka ya 1990.
Utasema nini, wakati kuna majina makubwa yalipita nchini kama kina Nonda Shaaban 'Papii', Ngandou Ramadhani, Constantine Kimanda, William Fahnbulleh, Kipre Tchetche na wakali wengine walipita kabla ya sasa Fiston Mayele, Prince Dube, Saido Ntibazonkiza, Jean Baleke, Idris Mbombo, Bruno Gomes na Djigui Diarra kukimbiza katika Ligi Kuu Bara.
Rekodi zinaonyesha, Yanga imekuwa na zali na nyota wa kigeni na hata makocha kutoka DR Congo, ilihali kwa upande wa Simba imekuwa na kismati na wachezaji kutoka Burundi.
Simba ni moja ya klabu iliyowahi kukimbiliwa na wachezaji Warundi, licha ya kwamba kwa miaka ya karibuni imekuwa ikibadilisha kwa kusajili nyota kutoka mataifa mengine yakiwamo ya Zimbabwe, Ghana, Zambia, Kenya, Uganda na hata DR Congo.
Hapa chini ni orodha ya kikosi na makocha waliowahi kutua au waliopo Msimbazi kutoka Burundi, hata kama baadhi yao hawakupata mafanikio makubwa kulinganisha na nyota wenzao wa Kikongo waliopita au waliopo Jangwani. Ieleweke hata Yanga imekuwa ikikimbiliwa na wachezaji wa kutoka taifa hilo la Burundi, lakini kimafanikio halingani na ile ya watani wao.
Mmoja ya nyota wa mwanzo kabisa kusajiliwa na Simba kutoka Burundi alikuwa ni, Damian Morisho Kimti aliyetua miaka ya 1990 na kuwa sehemu ya mastaa walioisaidia timu hiyo kucheza fainali ya michuano ya Kombe la CAF 1993, japo baadaye ilikuja kuelezwa alikuwa ni mzawa na kuzima zile kelele mshambuliaji huyo mfupi aliyefariki dunia Machi, 2020 alikuwa ni Mrundi. Endelea nayo....!


MACKENZIE RAMADHANI
Huyu ni mmoja wa makipa tegemeo waliowahi kukipiga Msimbazi kwa mafanikio makubwa. Kipa huyu aliyekuwa mashoto, alisajiliwa na Simba miaka ya 1990 na kuungana na makipa wengine hodari wa Kitanzania akiwamo Idd Pazi 'Father' na kuifanya timu hiyo iwe na machaguo mengi kwenye nafasi ya kulinda milingoti mitatu.
Hadi anaondoka Simba, Mackenzie alikuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichobeba mataji kadhaa yakiwamo ya Ligi Kuu Bara 1990, Ligi ya Muungano na Kombe la Kagame, japo alipoteza umaarufu baada ya kusajiliwa kwa Mohammed Mwameja kutoka Coastal Union aliyepishana na Pazi aliyeenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na baadaye akatemwa.


EMERY NIMUBONA
Beki huyu wa kulia aliyesajiliwa na msimu wa 2015-2016 akitokea Vital'O ya Burundi na alikuwa mmoja ya mabeki waliotengeneza ukuta wa Wekundu wa Msimbazi iliyokuwa chini ya Kocha Muingereza, Dylan Kerr, japo majeraha yalimnyima raha kikosini.
Baada ya Kerr kutimuliwa na kuletwa kwa kocha mwingine kikosini Nimubona naye alipoteza namba kabla ya kutemwa na kurudi kwao na msimu huu amerejea tena nchini akikipiga Coastal Union iliyopo Ligi Kuu Bara akiwa ni mmoja wa wachezaji wa kikosi cha kwanza.


RAMADHAN WASSO
Utasema nini juu ya beki huyo wa kushoto aliyetamba na Wekundu wa Msimbazi miaka ya 2000 akishikilia shavu la kushoto la kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Alikuwa kwenye kikosi kilichobeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2001 na 2003, sambamba na taji la Kombe la Kagame 2002, lililokuwa la mwisho kwa timu hiyo kwenye michuano hiyo. Kumbuka mwaka 2003 Simba iliandika historia ya kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kumvua taji Zamalek ya Misri, Wasso naye alikuwa mmoja ya nyota waliounda kikosi hicho.
Beki huyo alikuwa na uwezo mkubwa wa kukaba na kupandisha mashambulizi, kiasi cha kujijengea jina kubwa, kabla ya kuipiga chenga Simba wakati akiwa moto na anayetegemewa kwa kuzuga amepata timu ya kucheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji kisha kuibukia Jangwani.
Bahati mbaya hakupata mafanikio makubwa akiwa na Yanga, hivyo kulazimika kurudi tena Msimbazi, kisha kukimbilia Coastal Union kabla ya kustaafu soka la ushindani miaka ya 2010.


GILBERT KAZZE
Beki wa kati aliyesajiliwa na Simba mwaka 2013 sambamba na straika Amissi Tambwe wote wakitokea Vital'O ya Burundi iliyokuwa imetoka kubeba ubingwa wa Kombe la Kagame michuano iliyofanyika Sudan, na timu za Simba na Yanga kususa kushiriki kwa hofu ya usalama uliokuwapo nchini humo.
Ni mmoja ya mabeki waliokuwa wakicheza kwa akili na utulivu mkubwa katika kulinda makipa wa timu yake, lakini kuanzisha mashambulizi akishirikiana na nyota wengine wa eneo la kiungo.
Anakumbukwa zaidi kwa bao alililofunga dakika ya 83 na kuiokoa Simba isipate aibu mbele ya watani wao, Yanga katika Kariakoo Debry liliyopigwa Oktoba 20, 2013 na kumalizika kwa sare ya 3-3.
Katika pambano hilo, Yanga ilionekana ilikuwa ikirejesha kipigo cha aibu cha mabao 5-0 iliyopiwa msimu mmoja uliopita, kwa kufunga mabao matatu ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, kabla ya kocha Abdallah Kibadeni kufanya mabadiliko na kuchomoa bao zote hizo, kupitia Betram Mwombeki, Joseph Owino na Mrundi huyo kufunga la kusawazisha na kuiduwaza Wanajangwani.


SAID KOKOO
Beki mwingine wa kati kukipiga Msimbazi kutoka Burundi akiwa ameacha alama ya kuwa mmoja wa mabeki waliokuwa wakicheza na akili na nguvu wakati mwingine kuilinda timu hiyo.
Kokoo alisajiliwa mapema zaidi kuliko Kazze, kwani alitua Mzimbazi miaka ya katikati ya 2000 akiunda ukuta mgumu sambamba na kina Wasso, Said Sued, Boniface Pawasa na wakali wengine.
Beki huyo aliyestaafu kucheza soka la ushindani miaka ya mwishoni mwa 2010, licha ya kwamba bado yupo Tanzania akionekana kwenye michezo ya mabonanza, lakini akiendelea kukumbukwa kama mmoja ya mabeki wa kati bora waliowahi kucheza nchini.


PIERRE KWIZERA
Kiungo huyu mkabaji, alisajiliwa na Simba mwaka 2014 sambamba na Mkenya Patrick Kiongera, ikiwa ni moja ya sajili zilizokuwa na mbwembwe, lakini zilizoshindwa kuleta tija kutokana na kila mmoja kuchemsha kivyake. Kiongera alikwamba kutamba Msimbazi kutokana na majeraha yaliyomuandama mara kwa mara, wakati Kwizera alishindwa kuaminiwa na Kocha Patrick Phiri aliyekuwa amerejea tena Msimbazi na kuishia kumchomesha mahindi benchini na kumpa nafasi kubwa chipukizi Jonas Mkude.
Muda mfupi baadaye Simba ilimtema japo ilikuwa imempa mkataba wa miaka miwili, akakimbilia Rayon Sports ya Rwanda na cha ajabu akiwa huko alifanya kweli kwa kufunga mabao ya kutosha na kunyakua tuzo ya Mchezaji Bora kwa misimu miwili mfululizo  katika Ligi Kuu ya nchini humo.


RAJAB MWINYI
Mmoja ya viungo mahiri waliowahi kuzua mzozo baina ya Simba na Yanga kama ilivyokuwa kwa Ramadhani Wasso. Simba iliamua kulipa kisasi mwaka 2003 ya kuporwa Wasso kwa kumsajili Mwinyi aliyeng'ara na Vijana wa Jangwani akitoka kutwaa tuzo ya Kiungo Bora wa VPL 2002.
Uwezo wake wa kukaba, kumiliki mpira na kutengeneza mashambulizi la kuwatengenezea wenzake vyumba pia akifunga vilimfanya Mrundi huyo kuwa kipenzi cha Yanga, hivyo alipotimkia Simba iliwatia simanzi mashabiki wa timu hiyo, japo majeraha ya mara kwa mara yalimnyima nafasi ya kuendeleza moto, ingawa alipokuwa yupo fiti aliliamsha vya kutosha dimba la kati la Msimbazi kabla ya kuibukia Moro United, moja ya klabu iliyowahi kuwika kwa kishindo kabla ya kufa kifo cha kawaida na kupotea kabisa.


SAIDO NTIBAZONKIZA
Kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine wa Kirundi waliobahatika kukipiga Simba na Yanga kwa mafanikio, Saido Ntibazonkiza naye anaingia kwenye orodha hiyo.
Huyu bado anakipiga Msimbazi akiwa amesajiliwa kwenye dirisha dogo la msimu huu akitokea Geita Gold aliyojiunga nayo mwanzoni mwa msimu baada ya kutibuana na Yanga msimu uliopita na kutemwa juu kwa juu kabla ya mechi ya nusu fainali ya Kombe la ASFC iliyopigwa Mwanza.
Saido aliachwa na Yanga kwa kuhisiwa amekwisha, lakini tangu atue Msimbazi, jamaa amekuwa na balaa kwani ameshaifungia timu hiyo mabao matano ikiwamo hat trick moja, mbalimbali na kuasisti mara tatu, akiwa miongoni mwa walioifikisha Simba katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


AMISSI TAMBWE
Moja ya washambuliaji hodari kutoka Burundi waliowahi kukipiga nchini, akisajiliwa na Simba mwaka 2013 akitokea Vital'O alipotwaa nao Kombe la Kagame huku akiwa Mfungaji Bora wa michuano hiyo iliyofanyikia Sudan.
Alipotua Simba aliandika rekodi katika msimu wake wa kwanza kwa kutwaa tuzo ya Mfungaji Bora akifunga mabao 19 yakiwa ni mabao mengi kuwahi kufungwa na nyota wa kigeni katika Ligi Kuu msimu huu, kisha msimu uliofuata akaachwa kitatanishi kwenye dirisha dogo na kuibukia Yanga.
Akiwa Yanga alibeba nao ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili huku akitwaa tuzo nyingine ya Mfungaji Bora akifunga mabao 21 akiboresha zaidi rekodi yake ambayo hata hivyo ilikujwa kuvunjwa na Meddie Kagere ambaye kwa sasa wanacheza pamoja ndani ya timu ya Singida Big Stars.


SELEMAN NDIKUMANA
Mshambuliaji aliyejaliwa mwili mkubwa na ambaye aliibeba Simba ilipomsajili mwaka 2006 akitokea Inter Stars ya kwao Burundi na kuichezea kwa mafanikio, japo hakutwaa nao ubingwa wowote kabla ya kutimkia Molde FK ya Norway.
Anakumbukwa na mashabiki kwa uwezo wake wa kumiliki mpira, kupiga chenga na kuwatoka mabeki mbali na kufunga kwa mashuti makali aliondoka nchini kabla ya misimu miwili iliyopita kuibukia Azam FC kisha KMC, akiwa amepungua makali aliyokuwa nayo.


LAUDIT MAVUGO
Utasema nini juu ya straika huyo aliyesajiliwa Simba pia kutoka Vital'O mwaka 2016 na kuanza kuonyesha makeke yake kwenye Tamasha la Simba Day kwa kufunga bao moja kati ya manne yaliyoizamisha AFC Leopards ya Kenya kwa 4-1.
Usajili huo ndio uliokuwa gumzo kubwa msimu huo kutokana namna straika huyo alivyokuwa akitamba nchini kwao, kwani misimu miwili mfululizo nyuma kabla a kutua Msimbazi alikuwa ndiye Mfungaji Bora akifunga mabao 32 kila msimu.
Hata hivyo hakuwa na bahati ndani ya timu hiyo, akipoteza makali na kuachwa msimu wa 2018-2019 na kitu cha ajabu aliporejea tena uwanjani katika timu ya Napsa United ya Zambia aliibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya nchini humo mwaka 2019.


KOCHA MKUU
Nzoyisaba Tauzany 'Bundes', huyu ni mmoja wa makocha kutoka Burundi waliowahi kuzinoa timu za soka nchini, ikiwamo Yanga aliyotwaa nao ubingwa wa Kombe la Kagame 1993 kabla ya kwenda Majimaji Songea na kutwaa nao Kombe la Ligi Kuu ya Muungano 1998 kisha kunyakuliwa na Simba na kuinoa kwa misimu miwili mfululizo 1999 na 2000, japo akiwa na kikosi hicho hakutwaa taji lolote kwani ubingwa wa Bara ulibebwa na Mtibwa Sugar yote miwili.
Nzoyisaba ambaye kwa sasa ni marehemu anakumbukwa kwa soka lake maridadi alilofundisha na kuifanya Simba itishe kwa pasi za kampa... kampa tena na japo aliondoka Msimbazi bila kuwapa taji lolote, lakini heshima yake imesalia kikosini, mbali na mafanikio aliyoyapata na Yanga na Majimaji.
Kocha huyo anaingia kwenye kikosi hicho cha Warundi akisaidiwa na Masoud Djuma na Theiry Hitimana waliwahi kuwa makocha wasaidizi wa Simba na kisha kukaimu ukocha mkuu kwa muda kabla ya kutemwa kwa kushindwa kufanya maajabu.
Djuma amewahi kurejea nchini na kuinoa Dodoma Jiji, huku Hitimana aliyeibuka na Biashara United kisha Namungo na kuipandisha Ligi Kuu mwaka 2020 hivi karibuni alikuwa KMC aliyotemana nao.