Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Magori asimulia Mo Dewji alivyoibadilisha Simba

MAGORI Pict

Muktasari:

  • Miaka 90 si safari fupi kwa klabu ya soka. Ni kipindi kilichobeba mafanikio, changamoto, mabadiliko na matukio mbalimbali yaliyoiweka Simba katika nafasi yake ya sasa.

SIMBA SC inapoelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 90 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1936, historia ya klabu hiyo inaendelea kufunguka kupitia viongozi wake waliokuwepo katika vipindi tofauti vya maendeleo.

Miaka 90 si safari fupi kwa klabu ya soka. Ni kipindi kilichobeba mafanikio, changamoto, mabadiliko na matukio mbalimbali yaliyoiweka Simba katika nafasi yake ya sasa.

Katika kuelekea Simba Day na kilele cha maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Crescentius Magori, anafunguka kuhusu safari ya klabu hiyo, mfumo mpya wa uendeshaji, mchango wa Mohammed Dewji ‘MO’, mipango ya kituo cha mafunzo Bunju, usajili uliowahi kuwa na ushindani mkubwa, malengo ya Afrika na mipango mingine ya klabu.

MAGO 09

MIAKA 90 YA SIMBA NI HISTORIA NDEFU

“Kusema ukweli, miaka 90 ya Simba ni historia ndefu sana. Simba imepita kwenye mabonde na milima, mafuriko ya ngazi, lakini Simba imeendelea kubakia ni klabu imara sana, ni klabu isiyoyumba na ni klabu halisi ya kuonyesha ni klabu ya Kitanzania.”

Magori anaendelea kueleza kuwa pamoja na historia hiyo ndefu, Simba bado haijafikia mwisho wa safari yake.

“Bado safari ya Simba ni ndefu. Hatujafikia malengo yetu makubwa ambayo ni kutawala pia soka la Afrika, tuchukue ubingwa wa Afrika na kutawala soka la Afrika.”

Kauli hiyo inaonyesha kuwa maadhimisho ya miaka 90 kwa Simba hayatazamwi kama kusherehekea yaliyopita pekee, bali pia kuweka msingi wa hatua zinazofuata.

MAGO 10

MABADILIKO YA MFUMO WA SIMBA

Moja ya mambo makubwa yanayoendelea ndani ya Simba ni mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu.

Magori anaeleza kuwa Simba ilikuwa klabu ya wanachama tangu ilipoanzishwa mwaka 1936, lakini mabadiliko ya soka duniani yalifanya klabu hiyo itafute njia mpya ya kujiimarisha.

“Simba ilikuwa ni klabu ya wanachama tangu ilivyoanzishwa mwaka 1936. Lakini tukaona kila tukienda tunakwama kwa sababu mpira duniani unabadilika kila siku.”

Anaeleza kuwa mabadiliko hayo hayajalenga kuwaondoa wanachama kwenye klabu, bali kuongeza uwezo wa kifedha na kiutendaji.

“Ndiyo maana tukatangaza tenda. Sisi tubakie na asilimi 51 na mwenzetu ambaye ana uwezo wa kuweka pesa abakie na asilimia 49.”

MAGO 07

MO DEWJI NA MABADILIKO YA SIMBA

Miongoni mwa watu waliotajwa katika safari ya mabadiliko ya Simba ni Mohammed Dewji, ambaye amekuwa sehemu ya klabu hiyo tangu mwaka 2017.

Magori anasema mabadiliko ya kifedha ndani ya Simba yanaonekana wazi ukilinganisha hali ya klabu wakati Dewji anaingia na hali ilivyo sasa.

“Imebadilika sana. Kama mnavyoona, wakati amekuja hata bajeti yetu ilikuwa ndogo sana, ilikuwa chini ya bilioni tatu, lakini sasa hivi tunazungumzia bajeti ya bilioni 26 hadi 27.”

Anasisitiza kuwa, MO Dewji hawezi kutazamwa kama mdhamini wa kawaida kwa sababu nafasi yake ndani ya Simba ni zaidi ya udhamini.

“Yeye sio mtu wa kutoka mdhamini anaweza kutoka, lakini pamoja kwamba ni mwekezaji, yeye ni sehemu ya umiliki wa Simba.”

Kwa upande wa fedha, Magori anaeleza kuwa MO Dewji amekuwa akichangia katika mambo mbalimbali ya klabu, ikiwemo usajili.

“Yeye anatoa kila mwaka hela ya usajili, kuna zingine anatoa tu hata hasemi, hizo hataki hata zihesabiwe za bonus. Anasema hazirekodi.”

Magori anaeleza pia msimamo wa Dewji kuhusu fedha hizo kwamba: “Anasema wazi, ‘hizi siwezi kudai Simba. Sasa nikidai Simba kwanza watalipa kutokana na nini na mimi mwenyewe ni sehemu ya Simba.’”

MAGO 08

BUNJU NA KITUO CHA KISASA CHA MAFUNZO

Katika mipango ya muda mrefu ya Simba, ujenzi wa miundombinu umepewa nafasi kubwa.

Hata hivyo, Magori anaweka wazi kuwa uwanja si lazima uwe jambo la kwanza kufanyika.

“Kuhusu kujenga uwanja ameniambia jana hasubiri hata mchakato wa mabadiliko.”

Anaeleza kuwa kipaumbele cha kwanza ni kujenga kituo cha kisasa cha mafunzo.

“Kabla ya uwanja anachofikiria ni kujenga the best training facility pale Bunju kwa sababu anasema uwanja unaweza ukaenda kucheza ukakodisha.”

Anataja huduma zinazotarajiwa kuwepo katika kituo hicho.

“Cha kwanza training facility ya kisasa, hicho ndiyo first and foremost. Kutakuwa na recovery center, swimming pool, five star hostels kwa ajili ya senior team, kwa ajili ya women, kwa ajili ya youth.”

Magori anasisitiza kuwa lengo si kujenga kituo cha kawaida, bali kituo chenye viwango vya kimataifa.

“Itakuwa ni kama vile European standards training facility.”

MAGO 05

MAGORI NA SAFARI YAKE NDANI YA SIMBA

Magori anafunguka pia kuhusu uhusiano wake na Simba na namna alivyoingia kwenye uongozi wa klabu hiyo.

“Baba yangu marehemu Chief Johanes Magongwe Chacha alikuwa ni Simba na kwenye familia yetu nafikiri wote ni Simba.”

Anaeleza kuwa mwaka 1999 ndipo alipoanza rasmi kushiriki shughuli za Simba kupitia Friends of Simba.

“Mwaka 1999 ndiyo tulianza rasmi pale kutenda Simba kwa vitendo, nafikiri kundi la Friends of Simba.”

“Mimi niko ndani ya Simba, lakini kwa kiongozi kabisa kwa Simba ni mwaka 2018 kama CEO na baadaye mjumbe wa bodi na mwaka jana Septemba nikawa Mwenyekiti.”

MAGO 06

TUHUMA ZA FEDHA KWENYE USAJILI

Suala la fedha katika usajili ni miongoni mwa mambo ambayo Magori anaweka wazi msimamo wake.

Anasema jambo linalomkera ni pale mchezaji anaposajiliwa halafu baadaye kuwepo kwa madai kwamba kuna kiongozi aliyepata fedha.

“Mimi kitu kinachonikera katika uongozi wangu ni kwamba mchezaji akisajiliwa akiwa mbovu unaambiwa umechukua hela.”

Anaweka msimamo wake kuhusu tuhuma hizo akisema: “Sijawahi kuchukua hela ya mtu hata siku moja.”

“Na hili nalisema, naomba mlirudie. Kama kuna mchezaji aliambiwa katika pesa yake lazima kiongozi apate kiasi fulani na kama kiongozi huyo ni Magori, wachezaji hao wanapaswa waende kuwadai mawakala wao hiyo pesa wamefanya nini? Wamewaibia au wamekula kwa kutumia jina langu.”

MAGO 04

VICTOR COSTA NA VITA YA USAJILI

Magori anafichua moja ya simulizi zilizowahi kutokea katika usajili wa Victor Costa, akieleza namna Simba ilivyohusika katika mchakato huo.

“Tuliambiwa Victor Costa amesaini Yanga, wamempeleka Zanzibar. Tukamchukua mimi na rafiki yangu Musleh Ruhwey, tukapindua meza.”

Anaeleza pia kuwa wakati huo yeye binafsi alikuwa na mashaka kuhusu nafasi ya mchezaji huyo.

“Mimi nikamwambia, katika center half siwezi kumkubali. Naye mchezaji mwenyewe akasema roho yangu haitaki kwenda Yanga.

“Tukaenda naye Polisi. Kule habari zikawa zimeshafika kwa waandishi wote.”

“Mazoezi ya Yanga yakavunjika kwamba Victor Costa nyie mnamsubiri hapa, Victor Costa yuko Kijitonyama na Simba.”

MAGO 03

KIBU DENIS NA INONGA

Katika usajili mwingine, Magori anataja Kibu Denis na Henock Inonga kama mifano ya wachezaji ambao usajili wao ulikuwa na ushindani mkubwa.

“Hakuna usajili nilioufanya siku za karibuni mgumu na wa ajabu kama tulivyomsajili Kibu Denis kutoka Mbeya City.”

Anasema mchakato huo ulikuwa na ushindani mkubwa kati ya Simba na Yanga.

“Kulikuwa na vita na Yanga, vita ya ajabu sana.”

Kwa upande wa Inonga, anafichua namna Simba ilivyofanikiwa kuingilia mchakato wakati mchezaji akiwa njiani.

“Inonga alikuwa anaenda airport kupanda na ndege ya Kinshasa. Mimi nikampora, nikamrudisha. Kesho nimkampandisha ndege na kumshusha Zanzibar.”

MAGO 02

SIMBA NA MALENGO YA AFRIKA

Kwa upande wa mashindano ya Afrika, Magori anaweka wazi lengo la Simba.

“Sisi malengo yetu sasa hivi robo fainali tushaitoa. Sisi malengo yetu ni kufika nusu fainali. Naamini tuna kikosi kizuri.”

Anasisitiza kuwa ubora wa kikosi unatokana na uwepo wa wachezaji wenye uwezo wa kuamua mchezo mmoja mmoja.

“Trust me, the brilliance ya hii timu ya hawa wachezaji, ni quality ya juu sana.”

Anaendelea kuwataja baadhi ya wachezaji anaowaona kuwa na uwezo huo.

“Mpanzu anaweza akaamua mechi pekee yake, Anicet Oura anaweza akaamua mechi pekee yake, Clatous Chama anaweza kuamua mechi pekee yake, yule Keletso anaweza akaamua mechi pekee yake.”

MAGO 01
MAGO 01

KADI MPYA ZA WANACHAMA

Katika mipango ya kibiashara na huduma kwa wanachama, Simba inatarajia kuja na mfumo mpya wa kadi.

“Very soon tutatoa kadi za wanachama ambazo zitakuwa ni Visa Card kupitia benki zote.

“Tutaanza nafikiri na CRDB, NMB, NBC, TCB. Kadi ya kwanza itakuwa ni ya kawaida ya Simba, halafu kadi ya pili itakuwa ni Tanzanite ambayo itakuwa ni ya katikati na ya mwisho itakuwa ni Simba King.”

Anaeleza kuwa: “Kadi hizo zitakuwa na faida mbalimbali kwa wanachama vingi sana vya faida.”


KOCHA NA UJENZI WA TIMU

Kwa upande wa benchi la ufundi, Magori anasisitiza umuhimu wa kuwa na utulivu.

“Steve Barker sio tu kocha, ni kiongozi, sisi tunataka kukaa naye muda mrefu zaidi. Kama atakubali kubaki basi kama uongozi tuko tayari ingawa timu kubwa zimeanza kumfuatilia.”


UDHAMINI WA JAYRUTTY

Magori pia anazungumzia namna Simba inaweza kuongeza thamani ya udhamini na kutumia nembo yake kwenye bidhaa nyingi zaidi.

Anasema fedha ambazo Jayrutty ametoa kwa klabu ni kubwa na si jambo la kuchukuliwa kawaida.

“Pesa ambayo Jayrutty ametoa kwa klabu si utani. Hata hivyo, nimemshauri udhamini usibaki kwenye jezi pekee ana nafasi ya kujitanua zaidi.”

Badala yake, anaona nembo ya Simba inaweza kuonekana kwenye bidhaa mbalimbali.

“Auze na vitu vingine, aweke nembo ya Simba. Ni merchandise: taulo, kofia, vikombe, kalamu.”


SIMBA BAADA YA MIAKA 90

Miaka 90 ya Simba imekuwa safari ndefu yenye historia, mafanikio na changamoto. Lakini kwa Magori, historia hiyo haimaanishi kuwa klabu imefika mwisho wa safari akisema: “Bado safari ya Simba ni ndefu.”

“Hatujafikia malengo yetu makubwa ambayo ni kutawala pia soka la Afrika, tuchukue ubingwa wa Afrika na kutawala soka la Afrika.”


RATIBA NGUMU YAMTIA WASIWASI

Ingawa Simba inaingia kwenye msimu ikiwa na malengo makubwa ya kutwaa ubingwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Crescentius Magori, anasema ratiba ngumu ya mashindano inaweza kuwa changamoto kubwa kwa timu hiyo.

Magori anasema baadhi ya ratiba zimekuwa na safari ndefu ndani ya muda mfupi, hali ambayo inaweza kuwachosha wachezaji na kuathiri maandalizi ya timu kabla ya mechi zinazofuata.

Akitoa mfano wa ratiba ya mechi za mwisho, Magori anasema Simba inaweza kujikuta ikitoka Mbeya kwenda Geita, eneo la Bukombe, kabla ya kusafiri tena kwenda Kigoma ndani ya siku chache.

“Ratiba hii ambayo tunayo sasa hivi ni ngumu sana,” anasema Magori.

Anasema changamoto si kucheza mechi pekee, bali pia namna timu itakavyosafiri kutoka eneo moja kwenda jingine kwa muda mfupi.

“Unaweza ukatoka Mbeya, ukaenda Geita, Bukombe, halafu ndani ya siku chache unatakiwa uwe Kigoma,” anasema.

Magori anasema hali hiyo inakuwa ngumu zaidi kutokana na changamoto ya usafiri wa anga kati ya maeneo hayo.

“Tatizo kubwa ni usafiri. Hakuna usafiri wa uhakika wa ndege kutoka sehemu hizi kwenda nyingine,” anasema.

“Tunataka ubingwa, lakini ratiba kama hizi zinaweza kuwa mitego.”

Magori anasema pamoja na changamoto hizo, Simba haiwezi kutumia ratiba kama kisingizio cha kushindwa kutimiza malengo yake.

“Lazima tukabiliane nazo, kwa sababu malengo yetu ni makubwa,” anasema.