Simba kuendeleza moto kimataifa
Muktasari:
- Vijana hao wa Kocha Fadlu Davids, leo watakuwa wenyeji wa Bravos do Maquis katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika Kundi A utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Uwanjani hapo jana tulishuhudia wawakilishi wengine wa Tanzania, Yanga wakipambana na Al Hila ya Sudan katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika nao ukiwa wa Kundi A.
USHINDI wa mechi tano mfululizo zilizopita huku ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara sambamba na rekodi isiyovutia waliyokuwa nayo wapinzani wao, Bravos do Maquis kwa siku za karibuni, ni vitu vinavyoipa jeuri kubwa Simba kwenye mchezo wa leo.
Vijana hao wa Kocha Fadlu Davids, leo watakuwa wenyeji wa Bravos do Maquis katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika Kundi A utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Uwanjani hapo jana tulishuhudia wawakilishi wengine wa Tanzania, Yanga wakipambana na Al Hila ya Sudan katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika nao ukiwa wa Kundi A.
Simba tangu mara ya mwisho ipoteze mchezo wa Ligi Kuu Bara Oktoba 19 mwaka huu kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga, michezo mitano iliyofuatia imeshinda yote huku ikiwa haijaruhusu bao.
Mwenendo huo mzuri kwa Simba unadhihirisha wazi kikosi hicho kimejiimarisha katika maeneo yote ikiwemo ulinzi licha ya kwamba Kocha Fadlu amekuwa akifanya mabadiliko ya hapa na pale.
Awali safu ya ulinzi ya Simba ilikuwa ikiundwa na mabeki wa pembeni Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ huku Che Malone Fondoh na Abdulrazack Hamza wakiwa mabeki wa kati, golini anasimama Moussa Camara.
Kuumia kwa Abdulrazack Hamza, Fadlu akalazimika kumtumia Chamou Karaboue huku mara kadhaa akimpumzisha Tshabalala, nafasi yake akicheza Valentine Nouma. Hata hivyo, hakuna kilichobadilika zaidi ya ukuta kuwa imara.
Kwa sasa Hamza amepona na kurejea uwanjani, hivyo leo anaweza kurudi eneo lake kucheza na Che Malone na Tshabalala akichukua upande wake wa kushoto.
Safu hiyo ya ulinzi ndiyo ilifanya kazi kubwa ya kuwazuia Al Ahli Tripoli kwao wasifunge bao lakini walipokuja hapa nyumbani wakafanikiwa kupata moja ambalo halikutosha kwani wao walifunga matatu na kutupwa nje.
Ukiachana na ulinzi, katika mechi hizo tano Simba imefunga mabao kumi huku Jean Charles Ahoua akifunga matatu. Mengine yakifungwa na Leonel Ateba, Edwin Balua, Awesu Awesu, Steven Mukwala, Che Malone Fondoh, Debora Fernandes Mavambo na Shomari Kapombe.
Simba msimu huu katika michuano tofauti imecheza mechi 15 ikishinda 11, imepoteza 2 na sare 2. Katika ligi pekee, imefunga mabao 22 na kuruhusu matatu. Wakati Simba ikiwa hivyo, Bravos michezo mitano ya mwisho imeshinda 1, sare 3 na kupoteza 1 huku kwenye ligi yao ikishuka dimbani mara 12 ikiruhusu mabao 10 na kufunga 11. Ukiweka kando rekodi hizo, Simba imeonyesha kuwa hatari zaidi katika kipindi cha kwanza ambapo mechi tano za mwisho imefunga mabao sita muda huo huku manne yakipatikana kipindi cha pili.
Hii inaweza kuwa mbaya zaidi kwa Bravos ambayo inaonekana kuwa haipo imara katika kujilinda hasa kipindi cha pili, hivyo endapo kipindi cha kwanza itaruhusu angalau kufungwa kutokana na Simba muda huo kufosi sana, basi kipindi cha pili mvua ya mabao inaweza kuwaangukia.
Aina ya uchezaji wa Bravos, inaonekana ni timu ambayo ikipelekewa mashambulizi mfululizo inashindwa kuhimili kishindo na kuruhusu kufungwa kitu ambacho mshambuliaji wa Coastal Union, Mbaraka Yusuph amekibaini pindi walipokutana katika mchezo wa hatua ya awali msimu huu.
Coastal iliyofungwa mechi ya kwanza ugenini 3-0, nyumbani ikatoka 0-0 na kutupwa nje lakini Mbaraka anasema kama wangetumia vizuri udhaifu wa wapinzani wao basi pengine wasingetolewa.
“Bravos ni timu nzuri, lakini wana udhaifu wa kuhimili presha hasa wanapocheza ugenini. Simba wanapaswa kutumia nafasi hiyo kwa kushambulia kwa kasi ni vile tu tulishindwa kutumia nafasi ambazo tulizitengeneza katika mchezo wetu wa marudiano,” alisema mashambuliaji huyo.
Ukiachana na udhaifu huo, Bravos si timu ya kuibeza kwani licha ya kutofanya vizuri nyumbani, lakini kimataifa haipo kinyonge kutokana na matokeo yake inapokuwa ugenini.
Katika mechi mbili za hatua ya awali, imeshinda moja na sare moja, haijapoteza huku ikiruhusu bao moja pekee kitu ambacho Simba wanapaswa kuwa makini nacho leo. Ukiangalia wakati ikipambana kutinga makundi, Bravos iliifunga St Eloi Lupopo ya DR Congo nje ndani kwa matokeo ya jumla mabao 3-1.
Simba ya Fadlu katika kugunga mabao hayo, inaonekana kuwa hatari inapopeleka mashambulizi huku ikiwatumia zaidi watu wa pembeni kwa maana ya mabeki na mawinga, pia wanapopoteza mpira huwalazimisha wapinzani kufanya makosa.
Ukiangalia katika mchezo ambao waliifunga Al Ahli Tripoli mabao 3-1, Leonel Ateba alifunga baada ya mpinzani kurudisha mpira nyuma ulionaswa na mfungaji, huku pia Edwin Balua akifunga kwa shambulizi la kushtukiza baada ya Walibya hao kwenda kusaka bao la kusawazisha. Pia Kibu Denis alifunga kutokana na pasi ya pembeni.
Inavyocheza Simba, wakati mabeki wa pembeni (Kapombe na Tshabalala) wakipandisha mashambulizi, mawinga (Kibu Denis, Joshua Mutale, Edwin Balua au Ladack Chasambi) na mshambuliaji wa mwisho (Leonel Ateba au Steven Mukwala) wanakuwa ndani ya boksi la mpinzani, huku Jean Charles Ahoua ambaye mara nyingi hucheza kama namba 10, anatoke nje kidogo wakati huohuo Fernandes Mavambo akiwa nyuma yake akijaribu kukaa bila ya mpinzani.
Hii imewasaidia sana Simba katika kuhakikisha mpira inayotua ndani ya boksi hata kama ikiokolewa, inarudishwa kwa haraka hivyo ni ngumu shambulizi lao kufa kirahisi.
Hata hivyo, tahadhari kubwa imetolewa kwa Simba juu ya kiungo wa Bravos, Francisco Matoco ambapo taarifa zinabainisha ndiye mchezaji hatari zaidi wa kikosi hicho.
“Ni mchezaji mzuri sana ambaye Simba wanapaswa kuhakikisha wanamlinda ili asiweze kuwaletea madhara, ni hatari na anajua kusoma wapinzani uwanjani kwa haraka na kuunganisha timu hivyo, wawe makini naye,” alisema mmoja wa watu kutokea Angola.
Akizungumzia mchezo wa kesho, Fadlu amesema: “Maandalizi yetu yamekwenda vizuri, tumekuwa na siku nne za kujiandaa baada ya kutoka kucheza mechi ya ligi Mwanza, lakini kipindi cha mapumziko ya Kalenda ya Fifa tulijiandaa na mchezo huu. Tupo tayari kupambana kwenye kundi hili gumu huku tukienda kukutana na timu ngumu katika mechi ya kwanza.
“Tumewaangalia wapinzani wetu ni wazuri, wagumu, wana wachezaji warefu hasa eneo la mbele, hivyo tumejiandaa kutofanya makosa ya kuwaruhusu watuadhibu,” alisema Fadlu.
Hii ni mara ya sita Simba inacheza hatua ya makundi katika michuano ya Caf ndani ya misimu nane mfululizo tangu 2018/2019 hadi 2024/2025. Mara zote hizo ilipotinga makundi, imeishia robo fainali ambapo ilikuwa 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024 upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika na moja Kombe la Shirikisho msimu wa 2021/2022, huku misimu miwili ya 2019-2020 na 2021-2022 ikishindwa kufika makundi.
Katika misimu yote hiyo ambayo Simba imecheza hatua ya makundi, imefanikiwa kuvuka kwenda hadi robo fainali ndiyo inapogotea. Msimu huu itakuwaje huku mikakati iliyopo ni kucheza nusu fainali ya michuano hiyo? Fadlu na vijana wake wana kazi ya kufanya.
Mbali na mchezo huo, pia Kundi hilo itashuhudiwa CS Sfaxien kutoka Tunisia leo itakuwa mwenyeji wa CS Constantine ya Algeria, mechi ikichezwa saa 1 usiku kwenye Uwanja wa Hammadi Agrebi uliopo Radès, Tunisia.