Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba inavyolazimishwa kuanza upya

NONDO Pict


MASHABIKI wa soka nchini kwa sasa akili zao zipo Morocco kunakofanyika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 inayoanza Jumapili na kufikia tamati Januari 18 mwakani.


Tanzania ni moja ya nchi 24 shiriki za fainali hizo za 35 zilizosababisha kusimama kwa Ligi Kuu Bara hadi Januari 21 mwakani, siku chache baada ya AFCON kufikia tamati na bingwa kujulikana.


Lakini wakati wa mapumziko hayo ya Ligi Kuu kupisha michuano ya AFCON yamezipa fursa klabu za hapa nyumbani kufanya tathmini juu ya ushindani katika Ligi na hata michuano ya CAF wanayoshiriki kwa klabu nne za Yanga, Simba, Azam na Singida Black Stars.

Tathmini hiyo ni ya kujua wapi walipatia na wapi pa kurekebisha, huku ikichagizwa na kuwepo na kipindi kifupi cha kufunguliwa dirisha la usajili kwa ajili ya maboresho ya vikosi vyao.

Tunaweza kuitumia Simba kama mfano wa klabu hizo kutokana na ushindani iliyonayo kimataifa huku ikiwa na mabadiliko ya wakufunzi katika benchi la ufundi na kuilazimu sasa kutaka kutoa ajira mpya kwa kocha itakayekubali uwezo wake na kuona ana sifa za kuwafikisha katika malengo waliyojiwekea.

NOND 01

Katika ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa Kundi D, Simba inaburuza mkia kwa kutokuwa na pointi hata moja mbele ya Stade Malien ya Mali, Petro Atletico ya Angola na Esperance ya Tunisia, baada ya kupoteza mechi mbili za awali ikiwamo ya nyumbani dhidi ya klabu ya Angola na ile ya ugenini kule Bamako Mali mbele ya wenyeji Malien.

Kwa msimu uliopita, Simba ikiwa na kocha Fadlu Davids ilifanya makubwa na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, jambo lililoongeza shauku kwa mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kutaka kuona msimu huu inafanya makubwa katika Ligi ya Mabingwa.

Fadlu alitua Suimba wakati sahihi kwani timu iliamua kutengeneza kikosi upya na hata viongozi walijaribu kujiondolea presha kwa kuwaambia wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kwamba tunatengeneza timu tishio kwa baadaye na wakakubaliana mwalimu akaanza kazi.

NOND 02

Kitu cha kwanza Fadlu alianza kutengeneza tabia ya kushindana ndani ya timu kwa kutengeneza utaratibu mzuri wa timu kwenye kutafsiri matukio matano ya mchezo ambayo ni Simba chini ya kocha huyo ikiwa na mpira, bila ya mpira, inapopoteza mpira, inapopokonya mpira na matukio ya mipira ya kutenga kwenye kuzuia na kushambulia kulikuwa na tabia zake zilizoiwezesha timu kutengeneza tabia ya kushinda.

Ushindi huo ulitegemea msingi mzuri uliotengenezwa hasa kwenye matukio hasi ya timu bila mpira na tahadhari iliyokuwa imetengenezwa kwenye mabadiliko hasi yaani timu inapopoteza mpira.

Baada ya msimu kuisha na timu kuonekana imevuka malengo hasa kimataifa, fikra zikatoka tena kwenye kuendelea hatua ya pili ya ujenzi na kujikuta wanaruka na kujikuta wanataka kushindana, lakini kwa bahati mbaya Fadlu aliondoka na kuifanya timu ianze upya.

NOND 03

Fadlu alirudi Raja Casablanca ya Morocco baada ya kucheza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika raundi za awali dhidi ya Gaborone United ya Botswana na kumpa kazi aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kumalizia mechi ya marudiano na kuvuka raundi ya pili.

Katika raundi hiyo ilimbeba Dimitar Pantev aliyekuwa Gaborone United na kumtambulisha kama Meneja Mkuu, ingawa kiuhalisia alikuwa kocha mkuu na Seleman Matola akawa msaidizi wake na kweli timu ilipata matokeo mazuri na kuvuka kwenda makundi kwa kuing’oa Nsingizini Hotspurs ya eSwatini.

Bahati mbaya Pantev alishindwa kuipa matokeo mazuri Simba katika mechi mbili za awali za Kundi D na kuwa tiketi ya kuondolewa Msimbazi na timu kuachwa kwa Matola ambaye mashabiki wa Msimbazi bado hawamuamini kama ameiva kuachiwa timu jumla kama kocha mkuu.

Sio mashabiki na wapenzi wa Simba tu, bali hata mabosi wa klabu hiyo nayo hawamuamini ndio maana kwa sasa anaendelea na mchakato wa kusaka kocha mkuu mpya kukiwa na majina karibu 100 yaliyochujwa na kuelezwa yamebaki matano ambayo mmoja ndiye atakayepewa shavu na kuinoa timu.

Kwa yakini huu ni muda mzuri kwa Simba kujisuka upya na kuweka mambo sawa katika eneo zima la kikosi kuanzia kwa benchi la ufundi na hata kuongeza wachezaji inayowaamini wataibeba timu katika michuano inayoshiriki kuanza ile ya ndani hadi ya CAF kufikia malengo iliyojiwekea.

NOND 04

Kocha aliyekuja baada ya Fadlu alivutwa na rekodi tamu za Simba, lakini kwa bahati mbaya amekutana na hali tete, kwani hata ule msingi wao mkuu uliowapa sifa kupitia kwa Fadlu aliyeipa mafanikio umepotea ndani ya kiwanja, yaani Simba bila mpira au inapopoteza mpira imekua na udhaifu mwingi ki mbinu.

Kutokana na hilo Simba kwa sasa inahitaji kocha ambaye atakuwa anaamini kwenye uhalisia wa timu na sio daraja timu ilipo kwa mujibu wa msimamo wa CAF.

Simba inahitaji kujitengeneza upya na kuleta kocha ambaye atakuwa na kazi ya kuanza kutengeneza msingi mzuri wa uwiano wa timu katika vipindi viwili vya mchezo timu inapokuwa bila mpira na timu baada ya kupoteza mpira.

Kwa kuwaangalia wachezaji walioko kuna makundi mawili kama sio matatu, kuna wanaohitaji muda kukua na kufikia viwango vinavyohitajika na timu zenye wasifu kama Simba kwa mafanikio barani Afrika. 

Kundi la pili ni lile la wanaohitaji muda kuzoea mazingira na aina ya maisha nje ya uwanja kundi la tatu ni lile ambalo matarajio ni makubwa kwao, hivyo dirisha hili wawatazame wachezaji kwa kuzingatia hayo makundi ili waendelee na mpango wao wa kujenga timu.


Hakuna ubishi kikosi walichonacho hakina changamoto kubwa wako kwenye njia nzuri kuijenga timu, ila kinachowafanya wakati mwingine wasione hilo ni daraja walilolitengeneza mahasimu wao Yanga

Kila la kheri kwenye kipindi hiki cha kujiandaa na Ligi na michuano ya CAF itakaporejea kutofautiana kwa mitazamo kusiathiri maandalizi ya timu na kujua kuwa kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi, wayajenge na kuleta kocha atakayewavusha salama na kusahau kipindi hiki kigumu wanachopitia.