Afcon 2025 Morocco sawa, ila ni kama tumeisahau ya 2027
KOCHA wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Miguel Gamondi ametangaza na kuondoka na kikosi cha mwisho cha wachezaji kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya ushiriki wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025.
Michuano hiyo ya 35 tangu ilipoasisiwa mwaka 1957 inatarajiwa kuanza rasmi Desemba 21 na kufika tamati Januari 18 mwakani na Tanzania ni kati ya nchi 24 zitakazoshiriki fainali hizo ikiwa imepangwa Kundi C sambamba na Uganda, Nigeria na Tunisia.
Kabla ya uteuzi wa wachezaji hao 28, kocha Gamondi aliteua kikosi cha awali kilichokuwa na mastaa 53, kisha juzi amewachuja na kusaliwa na 28 aliokwenda nao Misri kwa ajili ya mechi kadhaa za kirafiki za kujipima nguvu kabla ya kujisogeza Morocco.
Ukitazama kikosi kilivyoitwa unaona ni dhahiri lengo la benchi la ufundi ni kwenda kushindana kutokana na majina yaliyomo.
Kifupi, huoni kama kuna mawazo hata kidogo yanayowakilisha mustakabali wa Afcon 2027 ambayo Tanzania itakuwa ni wenyeji sambamba na majirani zetu wa Kenya na Uganda.
Ndiyo, hakuna wachezaji vijana waliochukuliwa ili kwenda kupata uzoefu kwa maandalizi ya fainali hizo zijazo.
Sitaki kuingilia kazi ya Kocha Gamondi, lakini bado inashangaza kwa wachezaji vijana ambao hii ilikuwa ni fursa yao ya kwenda kupata uzoefu mkubwa katika fainali za Morocco kabla ya kuwa wenyeji wa Afcon ijayo.
Kwa vile sisi ndio wenyeji wa fainali hizo zijazo, ilikuwa ni vyema kuona vijana wakipewa nafasi ya kukua kutokana na michuano hiyo ya Morocco.
Sikatai tunaweza kubahatisha na kufanya vizuri kama yalivyowahi kufanya mataifa mengine, lakini hatuwezi kufika mbali kwa sababu ya kushindwa kuandaa vikosi vya miaka ya mbele.
Nalisema hili kwa kurejea yaliyowahi kuyakuta mataifa mengine yaliyobahatisha katika fainali za Afcon miaka ya nyuma na baada ya hapo hakuna wanaowajadili tena kwa sababu ilikuwa ni kama turufu tu na sio mikakati maalumu ya kufanya vizuri kwa miaka nenda rudi.
Sisi tukibaki katika uhalisia wa mambo tunapaswa kufikiria zaidi fainali ambazo tutakua wenyeji na kuanza kujiandaa uwanjani kutokana na michuano hii kuliko kufikiria kuweka historia Morocco.
Historia ambazo haziendani na uhalisia wa kikosi, kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wachezaji ambao huenda wasiwe sehemu ya kikosi kitakachopeperusha bendera kama wenyeji mwaka 2027.
Swali langu kama mmoja ya wadau wakubwa wa soka, je baada ya michuano hii ndiyo tunaanza kujiandaa na Afcon 2027 au inakuwaje?
Nauliza hivyo kwa kufahamu wazi hata benchi la ufundi lililokwenda Morocco halina uhakika kama litaandaa timu kwa ajili ya michuano inayofuata au inategemea matokeo ya michuano hii kuamua kama wanapewa jukumu la kuiongoza Stars ya fainali za 2027.
Gamondi kwa sasa ni kocha wa mpito baada ya Hemed Suleiman 'Morocco' aliyetupeleka katika fainali hizo za Morocco kung'olewa hivi karibuni akitoka pia kutufikisha robo fainali ya michuano ya Ubingwa kwa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2024 zilizofanyika Agosti mwaka huu kwa uenyeji wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Kwa kuangalia tu, unaona tulianza kukwama kwa benchi kudaiwa matokeo ili kuonyesha kama linastahili kuendelea. Ni nani anaweza kufikiria kesho na kutoa uzoefu badala ya kushindana?
Hapa wenye mamlaka hawawezi kukwepa lawama kwa kushindwa kufikiria kesho yetu ambayo tutakua nyumbani.
Kama wanaona mwaka 2027 ni mbali tuwakumbushe hadi michuano inaisha itakuwa ni Januari mwakani hapo tutakua na miezi 10 kama siyo 12 kabla ya michuano kuanza.
Hivyo, tunapaswa kuanza kuchagua vita vya kupigana, siyo kila vilivyopo mbele yetu tunataka kushindana navyo.
Kipaumbele chetu kinapaswa kuwa Afcon 2027 zitakazochezwa katika ardhi yetu wenyewe na hizi za Morocco zingetumika kama sehemu ya maandalizi na mikakati ya kujiweka tayari kwa vita.
Hata hivyo, kwa vile limeshafanyika, tutumie kosa hili kama somo kwa siku zijazo ili kutimiza malengo ya muda mrefu ya kuandaa jeshi la kuja kutubeba katika michuano mikubwa kwa sababu kina Simon Msuva, Mbwana Samatta, Shomary Kapombe na wengine umri umeanza kuwatupa mkono, hivyo kama hatuandai nyota wapya wa kuja kuziba nafasi zao, tutachemsha mbele ya safari.
Ndiyo maana nakumbuka tu, tuliifikiria zaidi Morocco 2025 na kusahau kama tuna Afcon 2027, tena tukiwa nyumbani kama ilivyokuwa fainali za CHAN 2024 na kuweka heshima ya kufika robo fainali.