SIMBA DAY: Simba ni taifa kubwa, mabingwa wa nchi

MABINGWA wa soka nchini, Simba inajiandaa kuadhimisha siku maalumu ya klabu hiyo maarufu kama Simba Day.
Tofauti na ilivyozoeleka, tamasha la msimu huu linafanyika Septemba 19 badala ya Agosti 8, likiwa ni maalumu kwa ajili ya utambulisho wa kikosi na jezi mpya za msimu kwa timu ya Simba, sambamba na kutoa tuzo kwa wadau wake.
Tamasha la mwaka huu ni la 13 tangu Simba Day ilipoanzishwa mwaka 2009 na uongozi wa enzi hizo chini ya Hassan Dalali ‘Field Marshal’ na Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda ‘Simba wa Yuda’ na wenzao ambao baadhi yao wametangulia mbele ya haki.
Kina Dalali waliasisi siku hiyo ili kukutanisha wanasimba wote bila kujali ni nani ili kupanga mikakati ya maendeleo kwa timu yao kabla ya kugeuzwa kuwa ni mahususi kutambulisha kikosi na jezi mpya za msimu ikiambatana na mechi maalumu ya kirafiki.
Mwaka huu tamasha hilo linafanyika kama ilivyo kwa misimu mingine litapambwa na burudani mbalimbali ikiwamo kumalizia kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Simba inalifanya tamasha hilo wiki moja tu kabla ya mchezo wao wa Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga ili kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ambao utakuwa wa 58 tangu ligi hiyo ilipoasisiwa mwaka 1965.
Wanasimba wakijiandaa kufanya tamasha hilo linaloenda sawia na miaka 85 tangu klabu yao iasisiwe rasmi mnamo mwaka 1936 Mwanaspoti inakuletea baadhi ya rekodi za kusisimua za klabu hiyo kongwe.
WAZEE WA KULIAMSHA
Achana na rekodi za kuwa klabu ya kwanza kuvaa jezi, viatu nchini ama kumiliki gari ama kuwazawadiwa nyota wake magari, Simba pia ina rekodi nyingine tamu ikiwamo ya kuwa timu yenye bahati ya kunyakua kila taji jipya likianzishwa.
Simba ndio klabu ya kwanza kubeba taji la Ligi ya Soka Tanzania (sasa Ligi Kuu Bara) ikifanya hivyo mwaka 1965. Klabu hiyo ilibeba bila kutoka jasho baada ya watani zao Yanga kususia mechi yao iliyovunjika dakika ya 80, huku wakiwa mbele kwa bao 1-0 na Chama cha Soka (FAT) kuamuru urudiwe na Vijana wa Jangwani kuingia mitini na Simba kupewa taji.
Simba ililitetea taji hilo kipindi hicho ikitumia jina la Sunderland kabla ya kubadilishwa jina na kuwa Simba mwaka 1971. Klabu sita pekee ndizo zilizoasisi Ligi Kuu ya sasa ambazo ni Tobacco au Sigara (Pwani), Young African, Coastal Union na Manchester United (Tanga), TPC (Moshi) na mabingwa Sunderland (Pwani).
Pia Simba ndio klabu ya kwanza kubeba taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame) ikifanya hivyo mwaka 1974.
Kama haitoshi imelibeba pia taji la Tusker lilioasisiwa mwaka 2001 na kulitetea kwa miaka mingine miwili mfululizo, kadhalika ilikuwa ya kwanza kubeba taji la michuano ya BancABCSuper8 iliyofanyika mara mmoja tu na kuzimika 2012.
Lakini pia hata Simba Day ndilo tamasha la kwanza kwa klabu za soka nchini, kabla ya Yanga na Azam nao kufuata mkumbo, mbali kuwa klabu ya kwanza kuingia mfumo wa Hisa ikiwapiga bao watani zao Yanga.
INATISHA KIMATAIFA
Licha ya Yanga kuwa klabu ya kwanza kushiriki michuano ya kimataifa kwa timu za Tanzania na kufika robo fainali kwa miaka miwili mfululizo 1969 na 1970, lakini Simba ndiyo yenye rekodi tamu katika mechi za kimataifa.
Simba ndio klabu ya kwanza Tanzania kufika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (enzi hizo Klabu Bingwa Afrika) 1974, pia ni klabu pekee ya Bongo kufika fainali za Afrika ikifanya hivyo kwenye Kombe la CAF 1993.
Simba ilipoteza 2-0 nyumbani mbele ya Stella Abidjan baada ya suluhu ya mechi ya ugenini, Ivory Coast, pia ndio klabu pekee nchini kuwahi kumvua taji mtetezi wa Afrika ikifanya hivyo 2003 dhidi ya Zamalek ya Misri na kutinga makundi. Na miaka mitatu iliyopita imeweza kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili moja ikikwama mbele ya TP Mazembe ya DR Congo na nyingine dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Pia Simba ndio timu pekee ya Tanzania inayozitetemesha klabu za Ukanda wa Afrika ya Kaskazini maarufu kama Waarabu kwani imekuwa ikizinyanyasa hasa zikija Tanzania.
Klabu nyingine ikiwamo Yanga zimekuwa zikitaabika na miaka mingi kabla ya kujikomboa hivi karibuni ikiwa ni zaidi ya miaka 30 walipoidonyoa Al Ahly na kuendelea dhidi ya Mo Bejaiya na MC Alger za Algeria, japo ilichapika ilipoenda kupambana nao ugenini.
WAZEE WA DOZI
Ni kweli Yanga ndio klabu ya kwanza kutoa kipigo kikali katika mechi ya watani wa jadi nchini ikiisulubu Simba mabao 5-0 mnamo Juni 1, 1968, ila inateseka na kipigo cha paka mwizi.
Simba ililipa kisasi na kuandikisha rekodi inatowatesa Yanga kwa miaka zaidi ya 40 walipoitandika mabao 6-0 Julai 19, 1977 ikishuhudiwa King Abdallah Kibadeni akipiga hat trick. Hat trick pekee katika Kariakoo derby.
Kama haitoshi wakati Yanga ikipambana kutaka kufuta aibu hiyo wakati ikitimiza miaka 35, iliongezewa tena dozi kwa kukandikwa mabao 5-0 na Simba katika mechi ya Mei 6, 2012.
Kama unataka kuwakera Wanayanga wakumbushie vipigo hivyo vya paka mwizi ilivyopewa timu yao na wapinzani wao hao ambao misimu mitatu sasa wanaonekana kuwa moto kweli na kutwaa kombe la Ligi mara tatu.
Hata kwenye michuano mingine Simba imekuwa ikitoa dozi kwa watani wao, ikifanya kwenye Kombe la Tusker na Mapinduzi na hata mwaka jana katika Kombe la Shirikisho (ASFC) waliwanyoosha watani wao kwa mabao 4-1.
MATAJI KIBAO
Ukiondoa mataji 22 iliyonayo katika Ligi Kuu Bara ikiwa nyuma ya Yanga iliyotwaa mara 27, Simba pia ina mataji mengine lukuki yanayoifanya itishe kwa klabu za Tanzania.
Katika Ligi, Simba ilibeba mataji yake 22 katika misimu ya 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007 (Ligi Ndogo), 2009-10, 2011-12, 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2021.
Katika Kombe la Kagame Simba inashikilia rekodi ya kubeba mataji mengi ikifanya hivyo mara sita katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002.
Simba pia inashikilia rekodi ya kubeba Kombe la Tusker mara nyingi zaidi kwa klabu za Afrika Mashariki ikifanya hivyo mara nne 2001, 2002, 2003 na 2005.
Katika Ligi Kuu ya Muungano pia ilimenyakua jumla ya mataji sita ikifanya hivyo 1993, 1994, 1995, 2001 na 2002, huku katika Kombe la Nyerere (sasa FA) imenyakua mara sita miaka ya 1984, 1995, 2000, 2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021.
Jumla ya mataji hayo ni 43 hapo hayajawekwa ya Kombe la CCM ama lile la Kombe la Mapinduzi walilowahi kutwaa mara tatu wakiwa nyuma ya Azam ambao ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo. Pia wamebeba kombe la Super8ABC, Bima Cup, mbali na Ngao ya Jamii iliyotwaa mara 9.
Sasa kwa rekodi hizo tamu kwa nini Simba a.k.a Wekundu wa Msimbazi wasiitwe ‘Taifa Kubwa’ kwani Simba ipo #Another Level na kweli ni Mabingwa wa nchi!