Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siku 32 ngumu kwa Yanga

Yanga Pict

Muktasari:

  • Bao hilo lilifungwa na Prince Dube katika dakika ya mwisho kati ya tano zilizoongezwa kabla ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi Ibrahim Kalilou Traore kutoka Ivory Coast kuhitimisha mchezo huo wa Kundi A, huku ubao wa matokeo ukisomeka 1-1.

YANGA juzi jioni ikiwa jijini Lubumbashi, DR Congo ilitumia sekunde chache kabla ya pambano lao dhidi ya TP Mazembe kumalizika, kufunga bao la kwanza lililowapa pointi moja katika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Bao hilo lilifungwa na Prince Dube katika dakika ya mwisho kati ya tano zilizoongezwa kabla ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi Ibrahim Kalilou Traore kutoka Ivory Coast kuhitimisha mchezo huo wa Kundi A, huku ubao wa matokeo ukisomeka 1-1.

Yanga ina kila sababu ya kujilaumu kutotoka na ushindi katika mchezo huo kutokana na kutawala sehemu kubwa hasa kipindi cha pili ambacho kiliongezwa kasi baada ya kocha Sead Ramovic kufanya mabadiliko ya wachezaji na kuifanya icheze kwa utulivu zaidi.

Kabla ya mechi hiyo ya juzi, Yanga ilikuwa imepoteza michezo miwili mfululizo ikianza kwa kugongwa mabao 2-0 na vinara wa kundi hilo, Al Hilal ya Sudan licha ya kucheza kwenye uwanja wa nyumbani, kisha ikakandikwa tena idadi kama hiyo ilipoenda ugenini jijini Algiers, Algeria ilipovaana na MC Alger.

Licha ya kuvuna pointi moja na bao moja lililowaepushia aibu kama ingepoteza tena mchezo wa tatu kutokana na ukweli katika ushiriki wake katika hatua ya makundi ya michuano ya CAF, Yanga ilikuwa haijawahi kupoteza michezo kwa idadi kama hiyo bila ya kufunga walau bao moja, lakini kazi ipo mbele yao.


Yanga 03

KWANINI?

Matokeo ya ushindi wa tatu mfululizo wa Al Hilal iliyoinyoa MC Alger usiku wa kuamkia jana kwa bao 1-0, una maana kwamba wababe hao wa Sudan tayari kimahesabu wamejihakikishia nafasi moja kutoka kundi hilo ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu barani humu.

Ushindi huo kwa Al Hilal umeifanya ifikishe pointi tisa na mabao matano, huku ikiruhusu moja tu katika mechi tatu ilizocheza hadi sasa, hivyo kuziachia msala MC Alger, TP Mazembe na Yanga katika kuwania nafasi moja iliyosalia ya kuungana nao katika robo fainali.

Yanga ina kazi ngumu zaidi kutokana na ukweli ina mechi moja ya ugenini dhidi ya wababe hao wa Sudan ambao rekodi zinaonyesha imekuwa ikiwatesa kila wanapokutana nao.

Ingawa Yanga ina michezo miwili ya nyumbani, ikianza kuikaribisha Mazembe mapema Januari, kisha kuifuata Al Hilal katika mechi itakayopigwa wiki moja baada ya mchezo huo dhidi ya Wakongomani na kumalizia ikiwa nyumbani dhidi ya mabingwa wa Algeria.

Yanga inahitaji kushinda mechi zote tatu ili kujiweka pazuri katika mbio za kufuzu kwa mara ya pili mfululizo hatua ya robo fainali, baada ya awali kufanya hivyo msimu uliopita kikosi kikiwa chini ya Miguel Gamondi.

Gamondi ndiye aliyeivusha pia makundi msimu huu, kabla ya kutemeshwa kibarua kumpisha Sead Ramovic baada ya Yanga kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam na Tabora United iliyowanyoa na kuwatibulia rekodi ya kuiongoza timu kucheza mechi nane mfululizo bila kuruhusu bao lolote.

Kama Yanga itashinda mechi zote tatu itamaanisha itafikisha pointi 10 ambazo haziwezi kufikiwa na Mazembe ama MC Alger, kwani itakuwa imezipunguza nguvu timu hizo na kuungana na mabingwa Sudan kupenya.

Hata hivyo, ni bahati mbaya kwamba Yanga ya Ramovic sio kama ile ya Gamondi. Yanga hii ya sasa haichezi kwa kasi kubwa na kukabia juu. Hii inapoteza mipira mingi na nyota wa kikosi hicho ni kama hawajiamini kabisa, wanacheza kichovu na kukosa umakini katika eneo la mwisho la umaliziaji.

Hata katika mechi ya juzi ilicheza hovyo kipindi cha kwanza kabla ya kuzinduka kipindi cha pili baada ya mabadiliko ya wachezaji walioanzia benchini akiwamo Clatous Chama, Prince Dube, Clement Mzize, Stephane Aziz KI waliochukua nafasi za Maxi Nzengeli, Kennedy Musonda, Mudathir Yahya na Duke Abuya, ukiacha ile ya kipa Diarra Djigui aliyempisha Abubakar Khomeiny.


Yanga 01 (1)

NAMBA HAZIONGOPI

Katika mechi mbili za hatua ya awali ya michuano hiyo, Yanga ya Gamondi ilizifunga Vital’O ya Burundi na CBE ya Ethiopia kwa vipigo vikubwa. Yanga iliing’oa Vital’O kwa jumla ya mabao 10, kisha ikashinda 7-0 kwa Wahabeshi.

Hata kama ni kweli mechi za mtoano na hizi za makundi ni tofauti katika ushindani wake, lakini bado Yanga ya Ramovic ina kila sababu ya kuboresha kikosi hicho kama kweli anataka kufuata nyayo za Gamondi za kuivusha timu kwenda robo fainali.

Kwa msimu uliopita katika hatua hiyo ya makundi, Yanga ya Gamondi ilicheza mechi sita za makundi ikivuna jumla ya pointi nane na mabao tisa ikiwa vinara wa Kundi D kwa timu zilizofunga mabao mengi ikiwapita Al Ahly ya Misri waliokuwa watetezi na walioshika namba moja katika kundi hilo kwani yenyewe ilifunga mabao sita tu.

Pia ukuta wa Yanga ya Gamondi, uliruhusu mabao sita, yaliyochangiwa na kipigo cha 3-0 ilichopewa ugenini na CR Belouizdad ya Algeria  na sare ya bao 1-1 dhidi ya Medeama ya Ghana na kipigo cha bao 1-0 ikiwa ugenini dhidi ya watetezi wa taji hilo ambao walilitwaa katika fainali dhidi ya Esperance ya Tunisia.

Kutokana na ukweli siku Yanga ikirudiana na Mazembe, pia MC Alger itakuwa inaipokea Al Hilal jijini Algiers, hivyo Yanga kuombea mchezo huo uwe na matokeo kama ya juzi kwa maana Al Hilal washinde na kufuzu moja kwa moja na kuwazuia MC Alger wasiongeze pointi zaidi na walizonazo, wakati yenyewe ikishinda Kwa Mkapa, kwani itafikisha pointi nne na kulingana na wababe hao wa Algeria.

Mechi dhidi ya MC Alger itakayochezwa kati ya Januari 17, Yanga itahitajika kushinda na kulipa kisasi na kuifanya ifikishe pointi saba hapo ikiwa imeshatoka kuvaana na Al Hilal huko Mauritania ambao washafuzu robo.

Matokeo ya Al Hilal na Mazembe hayataisumbua sana Yanga, kwani hata kama Wakongomani wakishinda itaifanya ifikishe pointi nne tu, hivyo mechi wa mwisho ya ugenini dhidi ya Wababe wa Sudan itakuwa kama fainali, kwani itapaswa pia kushinda kabla ya ile ya kufungia hesabu ikiwa nyumbani ili kujihakikisha kufuzu, lakini hata sare inaweza kuwa na faida, kwani itaifanya ifikishe pointi nane zitakazowavusha kama ilivyokuwa msimu uliopita.


Yanga 05

TATIZO LIPO HAPA

Yanga inaweza kukutana na ugumu zaidi kama itapoteza mechi yoyote kati ya hizo tatu, huku MC Alger au Mazembe wakivuna pointi mikononi mwao, kwani itawaweka pabaya na huenda ikasikilizia hewani tu hatua ya robo fainali.

Ramovic na kikosi hicho wanapaswa kutumia siku 32 zilizosalia kabla ya kuhitimisha mechi za makundi kujipanga vyema na kuboresha kila eneo, hasa safu ya ushambuliaji, ikiwezekana Ramovic akawapa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza Clatous Chama na Clement Mzize, kwani wanaonekana wana faida wakiwa uwanjani kwa uweze wa kukaa na mpira na hata akili kubwa wakiwa mbele ya lango la adui.

Inawezekana kocha anajua zaidi kuhusu wachezaji hao, lakini namna wanapoingia na kubadilisha sura ya mechi mbili zilizopita ni sababu ya Ramovic kuliangalia hilo katika mechi hizo tatu za mwisho zenye uzito kwa mustakabali wa ndoto za Yanga za kufika mbali kwenye michuano hii ya kimataifa.

Hata eneo la ulinzi la Yanga linahitaji kumuona mtu kama Chadrack Boka anapewa shavu la kushoto ili ashirikiane na Yao Kouassi kutengeneza mashambulizi mengi, huku mabeki wa kati Ibrahim Baka na Dickson Job kucheza kwa utulivu mkubwa na kuwachunga nyota wa timu zote watakazokutana nazo.

Katika mechi ya juzi, Yanga ilifungwa bao la kichwa na Cheikh Fofana, baada ya mabeki hao kujisahau, pia kuna muda walikuwa wanakaba kwa macho na kama sio umakini m

Yanga 06

bovu wa washambuliaji wa Mazembe, Yanga ingeendeleza ile dozi ya 2x2.


NAFASI BADO IPO

Pamoja na Yanga kuwa mkiani katika kundi hilo, lakini bado ina nafasi kama itaamua kutumia dakika 270 kwa akili na kuvuna alama zote tisa, huku ikiziombea mabaya MC Alger na Mazembe katika mechi zao ili zisifikishe alama itakazovuna.

Muhimu zaidi ni Yanga kutumia vyema mechi za nyumbani tofauti na ilivyoanza hatua ya makundi na kufungwa mabao 2-0, ikiwa ni kipigo cha kwanza cha nyumbani katika hatua ya makundi ya michuano ya CAF tangu ilipofungwa mabao 3-2 na Gor Mahia ya Kenya kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Julai 29, 2018 timu hizo zikiwa Kundi D sambamba na Rayon Sports ya Rwanda na USM Alger, Yanga ilipata mabao yake kupitia kwa Deus Kaseke (dk59) na Rafael Daud (dk81), huku Wakenya wakitangulia mapema na bao la dakika ya kwanza la George Odhiambo kabla ya Jacques Tuyisenge kufunga dakika chache kabla ya mapumziko na Haroun Shakava kufunga hesabu katika dk 64.

Katika mechi sita mfululizo za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2022-2023 na zile za Ligi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, Yanga haikupoteza mchezo wowote wa nyumbani, hivyo kosa walilofanya mbele ya Al Hilal, halipaswi kurudiwa katika mechi hizo zijazo dhidi Mc Alger na Mazembe.

Kitu cha muhimu Yanga kujua kwamba nafasi bado ipo.