SHAURI LA MWAKALEBELA PICHA PANA
Muktasari:
NI bahati mbaya sana kwamba wapenzi na wadau wa soka hukimbilia katika majumuisho rahisi rahisi badala ya kujadili kwa mapana hoja zinazotokana na vitendo fulani, maamuzi au tukio fulani.
NI bahati mbaya sana kwamba wapenzi na wadau wa soka hukimbilia katika majumuisho rahisi rahisi badala ya kujadili kwa mapana hoja zinazotokana na vitendo fulani, maamuzi au tukio fulani.
Na wengi hukimbilia kuangalia historia ya mtu aliyetoa hoja na si kuangalia anazungumza nini. Ndivyo ilivyo katika shauri la Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, ambaye katika mazingira ya ajabu amefungiwa kujishirikisha na soka kwa miaka mitano kwa kosa ambalo bado halijaeleweka. Binafsi, bado sijaielewa vizuri Kamati ya Maadili kwa kufikia uamuzi ule kwa kosa kubwa kama la ‘uchochezi’ ambalo ni moja ya makosa mawili aliyoshtakiwa. Ni dhahiri kuwa kosa hilo ni kubwa sana na hata kulithibitisha ni vigumu sana, lakini Kamati ya Maadili ilifikia uamuzi bila ya kulithibitisha, yaani kupata ushahidi usio na shaka kwamba maneno ya Mwakalebela yana chembechembe za uchochezi.
Katika mahakama za kiraia, ambako mpira wa miguu uliamua kuondoka ili kuwezesha mambo yanayohusu mpira yaende kwa kasi ambayo soka inaitaka, uchochezi huthibitishwa na anayeshtaki. Ndio maana katika kesi anayeshtaki hujaribu kupeleka mahakamani mashahidi ambao wana nia ya kuonyesha walishawishika na maneno ya uchochezi ya mshtakiwa kiasi kwamba walitaka ama walichukua hatua.
Hatua hizo ni kama kupanga kuandamana dhidi ya anayeshtaki, kupanga kufanya vurugu, kupanga kupiga au kupiga waamuzi au kufanya lolote lile baya baada ya kuchochewa na maneno ya mshtakiwa.
Hilo halikufanyika, badala yake Mwakalebela amehukumiwa kwa kile ambacho baadhi wameanza kuamini kuwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa viongozi wa Shirikisho la Soka (TFF).
Sisemi kwamba Mwakalebela hakufanya kosa, lakini naona kwamba alibambikiwa kosa kubwa ili apate adhabu kubwa. Kibaya zaidi ni kwamba hadi anahukumiwa kosa hilo halikuweza kuthibitishwa na aliyeshtaki. Kwa vyama ambavyo vimeendelea, vimeweka hadi mwongozo wa kauli ambazo viongozi au makocha wanatakiwa kutoa kabla na baada ya mechi au kuhusu uendeshaji wa mashindano ili kuepuka kuwaweka viongozi au waamuzi katika hali ngumu ya kufanya maamuzi kwa haki.
England, kwa mfano, wana huo mwongozo ambao umesababisha makocha wengi kushtakiwa Chama cha Soka (FA) baada ya kutoa kauli zinazoonekana kushinikiza waamuzi kufanya maamuzi tofauti au kuponda uamuzi wao au kuusisha na upendeleo.
Wakati Jose Mourinho akiwa Manchester United alishtakiwa FA kwa madai kuwa maneno aliyotoa katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi dhidi ya Liverpool Oktoba 17, 2016 yalikuwa na chembechembe za tabia isiyofaa na pia kwa kuudhalilisha mchezo wa soka (improper conduct and/or bringing the game into disrepute).
Katika mkutano huo, mwandishi wa habari alimuuliza Mourinho akisema; “Kwa sababu mengi yamefanyika Merseyside kuhusu ukweli kwamba mwamuzi (Anthony Taylor) anatoka Manchester, una maoni yoyote kuhusu suala hilo?”
Mourinho alijibu akisema; “Nina maoni yangu, lakini naelewa na najifunza kama utataka useme hivyo, napata somo kwa kuadhibiwa mara nyingi kutokana na baadhi ya maneno, kwa hiyo sitaki kusema chochote kuhusu suala hilo, lakini nadhani (mwamuzi) Taylor ni refa mzuri sana. Lakini nadhani kuna mtu, kwa makusudi, anamuwekea shinikizo kubwa, kiasi kwamba nafikiri itakuwa vigumu kwake kufanya vizuri.”
Ingawa alisema hataki kutoa maoni yake kuhusu mwamuzi huyo, Mourinho alionyesha msimamo wake katika sentensi ya mwisho aliposema kuna mtu anamuwekea shinikizo kubwa kiasi kwamba hataweza kufanya vizuri.
Kwa hiyo alikuwa amekiuka kifungu cha E3 cha kanuni za FA kuhusu maoni ya makocha au viongozi.
Kifungu hicho kinasema: “Wakati wote, mshiriki atatakiwa kufanya jambo kwa maslahi ya mchezo na kwa njia yoyote asifanye kitu kwa namna ambayo si sahihi au kuudhalilisha mchezo, kufanya lolote kati ya hayo, au yote mawili, kucheza rafu mbaya, kufanya fujo, kutishia, kutumia lugha chafu, maneno yasiyofaa au matusi au tabia mbaya.” Kwa hiyo, FA ikamshtaki Mourinho kwa makosa hayo mawili. FA imeweka mwongozo kuwa wachezaji na viongozi wa klabu ikisema wanatakiwa wajue kuwa chama hicho kimeweka viwango vya maoni ambayo yanaweza kutolewa na washiriki. Maana ya maoni yanayoweza kusababisha mtu kushtakiwa ni maoni yoyote-- ama yawe chanya au hasi-- kuhusu mwamuzi aliyeteuliwa kuchezesha mechi, maoni yoyote yanayomaanisha mwamuzi anapendelea, kuhoji uadilifu wa mwamuzi, kumshambulia kwa maneno, kumtishia, maoni kuhusu kabila au rangi yake, dini, utaifa, jinsia, ulemavu na kadhalika. Haya yote yanazaa makosa yanayoitwa kuonyesha tabia isiyofaa au kuudhalilisha mchezo wa mpira wa miguu. Haya ndiyo makosa ambayo Mwakalebela angeshtakiwa, badala ya neno zito la uchochezi.
Ni kweli maswali aliyohoji kuhusu utendaji wa TFF yangeweza kusababisha kila kifanywacho na shirikisho hilo kisichukuliwe kwa uzito na pengine kionekane kinalenga kumbeba mtu au kundi fulani na badala yake mchezo kupoteza hadhi yake. Katika kumuadhibu, kamati iliangalia historia ya Mourinho katika kuzungumzia mechi na ikamkuta na mashtaka kadhaa baadhi akishtakiwa wakati akiwa Chelsea. Mourinho alikiri kuonyesha tabia ambayo si sahihi, lakini akakana kuudhalilisha mchezo, hata hivyo rekodi yake ilionyesha kuwa alikuwa na tatizo na hivyo kupigwa faini ya Pauni 50,000 na kupewa onyo asirudie vitendo hivyo. Nimetoa mfano huo nikijua kuwa suala la Mwakalebela limejadiliwa kijuujuu sana na kufikia majumuisho ya kirahisi kwamba alistahili kuadhibiwa bila ya kujadili suala hilo katika picha kubwa zaidi. Leo ni Mwakalebela na kesho anaweza kuwa mtu mwingine.
Tayari viongozi wawili wa kamati za TFF wameshafungiwa na Baraza la Michezo (BMT) kwa makosa ambayo Kamati ya Maadili ya TFF ingeweza kufanya maamuzi, lakini haikufanya. Hii inamaanisha udhaifu katika kamati hiyo hadi serikali ikaingilia kati.
Na Yanga imeonyesha kumuunga mkono Mwakalebela kwa kuwasilisha suala hilo wizarani, jambo ambalo linazidi kuweka maswali katika uadilifu wa vyombo vya maamuzi vya TFF. Binafsi nilipoona mabadiliko ya Katiba ya TFF kuipa Kamati ya Utendaji ya TFF mamlaka ya kuengua wajumbe wa Kamati ya Maadili wakati wowote, nilijua uhuru wa chombo hicho umeshaondolewa na haitakuwa na uwezo tena wa kufanya maamuzi yake kwa uhuru kama ilivyo ile ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) ambayo ilimshamfungia Rais wake, Sepp Blatter wakati akiwa bado hajaondoka madarakani.
Kamati ya Maadili ni chombo cha Mkutano Mkuu wa TFF, hivyo Kamati ya Utendaji imekamisishwa mamlaka ya uteuzi wa wajumbe tu. Shughuli ya kuwaondoa kwa makosa yoyote yale, inatakiwa ibakie kwa Mkutano Mkuu, lakini hilo limebadilishwa. Mkutano Mkuu umeporwa mamlaka yake na Kamati ya Maadili na hivyo inaweza kutumiwa kwa njia yoyote ile na viongozi.
Unaposikia mdau amepewa adhabu kubwa kama vile alitoa rushwa, unaanza kuhisi tatizo katika ufanisi wa vyombo vya maamuzi vya TFF. Na unahisi huo ni mwanzo tu. Kwa hiyo, sikutaka kuonyesha kuwa Mwakalebela hakufanya kosa, bali kiini cha haya matatizo ni nini na tafsiri yake, hasa wakati huu wa kuelekea Mkutano wa Uchaguzi Mkuu wa viongozi wa TFF.
Ni muhimu sana kwa Kamati ya Maadili kufanya kazi kwa uadilifu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha washtakiwa wanaadhibiwa kwa kosa ambalo ni sahihi na limethibitika kiushahidi.
Mwandishi ni katibu mkuu wa zamani wa TFF anapatikana kwa simu 0659-626656