Serie A inavyorejea na maajabu mapya
Muktasari:
- Msimu wa Serie A 2026/27 utaanza Agosti 22, huku mabingwa watetezi Inter wakitarajia kuanza kwa kishindo dhidi ya Monza, iliyopanda daraja kwenye Uwanja wa San Siro. Wakati huohuo, Como ya Cesc Fabregas itasafiri kucheza na Udinese.
MILAN, ITALIA: JE, Inter Milan itaweza kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Italia (Serie A)? Ni timu zipi zitafuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya? Na je, klabu zilizopanda daraja zitaweza kubaki katika ligi? Haya ni majibu ya maswali muhimu kupitia utabiri wa msimu wa Serie A 2026/27.
Msimu wa Serie A 2026/27 utaanza Agosti 22, huku mabingwa watetezi Inter wakitarajia kuanza kwa kishindo dhidi ya Monza, iliyopanda daraja kwenye Uwanja wa San Siro. Wakati huohuo, Como ya Cesc Fabregas itasafiri kucheza na Udinese.
Kocha Cristian Chivu alifurahia msimu wake wa kwanza mzuri akiwa Inter Milan akiiongoza kutwaa mataji mawili ya ndani baada ya pia kushinda Coppa Italia. Chivu alikuwa kocha wa tano katika historia kushinda Scudetto katika msimu wake wa kwanza akiwa Inter kwenye Serie A, baada ya Arpad Weisz 1929/30, Alfredo Foni 1952/53, Giovanni Invernizzi 1970/71 na Jose Mourinho 2008/09.
Hata hivyo, Inter itakabiliwa na mambo mengi yasiyojulikana katika harakati za kutetea ubingwa, hasa kutokana na timu nyingi zinazoweza kuwa wapinzani wao kubadilisha makocha. Napoli ilishinda Supercoppa Italiana msimu uliopita na kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi chini ya Antonio Conte, lakini sasa Massimiliano Allegri ndiye atakayekuwa kocha katika Uwanja wa Diego Armando Maradona.
Nafasi iliyoachwa na Allegri AC Milan imejazwa na kocha wa zamani wa Manchester United, Ruben Amorim, huku Gennaro Gattuso akiiongoza Lazio baada ya kuondoka timu ya taifa ya Italia mapema mwaka huu. Kwa upande wake Maurizio Sarri amepeleka uzoefu Atalanta, wakati Roma na Juventus zimeendelea kuwaamini Gian Piero Gasperini na Luciano Spalletti mtawalia. Venezia na Frosinone zimepanda Serie A, lakini je, zitaweza kubaki msimu huu?
Nani kubeba ubingwa Serie A?
Kama ilivyokuwa msimu uliopita, Inter Milan inatarajiwa kutwaa tena ubingwa wa Serie A kwa mujibu wa utabiri mwingi wa mifumo ya ubashiri.
Inter ilitwaa ubingwa msimu uliopita kwa tofauti ya pointi 11, huku ikiwa kinara wa kufunga mabao mengi zaidi, 89, ikifungwa 35 pekee idadi iliyokuwa ya nne kwa uchache. Como ilifungwa mabao 29, Roma 31 na Juventus 34.
Chivu ameimarisha safu ya ulinzi kwa kumsajili mshindi wa mataji mengi, John Stones, kwa uhamisho wa bure baada ya kuondoka Manchester City. Stones alishinda mataji makubwa 17 akiwa Man City yakiwemo sita ya Ligi Kuu England. Na sasa atataka kuongeza Scudetto kwenye mkusanyiko wake wa mataji. Inter inapewa nafasi ya asilimia 35.1 ya kutetea ubingwa wa Serie A na wapinzani wake wakubwa wanatarajiwa kuwa Roma, Como na Juventus.
Roma haijashinda Serie A tangu 2000/01, wakati kikosi cha Fabio Capello kilichokuwa na wachezaji kama Gabriel Batistuta na Francesco Totti kilipoishinda Juventus katika mbio za ubingwa.
Kwa upande wa Gasperini alikuwa na msimu mzuri wa kwanza akiwa Roma, akiiongoza kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 2017/18. Pia, Roma ilivuka pointi 70 kwa mara ya kwanza tangu msimu huo. Pia imefanya usajili muhimu ikimuongezea Paulo Dybala mkataba kwa msimu mwingine na kumnunua moja kwa moja Donyell Malen baada ya awali kuwepo kwa mkopo akitokea Aston Villa.
Kati ya wachezaji waliomaliza msimu wakiwa na chini ya mechi 20 katika kipindi ambacho ushindi una thamani ya pointi tatu, Zlatan Ibrahimovic pekee ndiye aliyefanya vizuri zaidi kuliko Malen. Ibrahimovic alifunga mabao 15 katika mechi 19 msimu wa 2020/21, huku Malen akifunga 14 katika mechi 18 msimu uliopita.
Roma inapewa asilimia 12.7 kushinda ligi, huku Como ya Fabregas ikiwa na nafasi kubwa zaidi ya 13.6% ya kutwaa Scudetto. Como itaingia ikijiamini baada ya kuifunga Cremonese 4-1 katika siku ya mwisho ya msimu uliopita na kufuzu Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza katika historia yake. Matarajio ya kuwania ubingwa yameongezeka baada ya nyota wao Nico Paz kukubali kubaki kwa mwaka mwingine, hivyo kuahirisha kile kinachoonekana kuwa kurejea kwake Real Madrid.
Paz alihusika moja kwa moja katika mabao mengi zaidi kuliko kiungo mwingine yeyote wa Serie A msimu uliopita, 18, akifunga 12 na asisti sita.
Juventus, kwa upande mwingine, ilikosa nafasi nne za juu msimu uliopita baada ya kushinda mchezo mmoja tu kati ya mitano ya mwisho.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Spalletti kumaliza nje ya Ligi ya Mabingwa tangu alipomaliza wa sita akiwa Roma 2008/09. Hata hivyo, kocha huyo anajua namna ya kushinda ubingwa, baada ya kutwaa Scudetto akiwa Napoli 2022/23. Juventus pia imeimarisha kikosi kwa kumsajili kinda mwenye kipaji Kerim Alajbegovic na kumrudisha Randal Kolo Muani.
Kwa maana nyingine ni kwamba Juventus ina nafasi ya asilimia 11.4 ya kushinda Serie A 2026/27, huku Napoli ikiwa na 7.5 na Atalanta 6.8.
Itakuwa vigumu kuiondoa Napoli kwenye hesabu kutokana na kuwa na Allegri, ambaye ni kocha aliyeshinda Serie A mara nyingi kuliko wengi. Ni Giovanni Trapattoni pekee aliyeshinda zaidi yake, mara saba.
Nani kucheza Ligi ya Mabingwa?
Mbio za nafasi za Ligi ya Mabingwa 2025/26 zilikuwa kali hadi mwisho, huku Como ikiipita AC Milan na Juventus siku ya mwisho na kumaliza nafasi ya nne. Timu zote 20 zina angalau asilimia 0.9 ya kufuzu mashindano makubwa ya Ulaya, lakini nne zinazopigiwa upatu zaidi ni Inter, Roma, Como na Juventus kufuzu Ligi ya Mabingwa, huku Juventus ikiwa na asilimia 47.8 kurejea katika mashindano hayo.
Napoli inatabiriwa kuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kumaliza nje ya nne bora kuliko ndani ya nne bora, lakini bado ina asilimia 38.4 ya kubaki miongoni mwa timu bora za Ulaya. Afya ya Kevin De Bruyne itakuwa jambo muhimu katika mafanikio ya Napoli msimu wa 2026/27. Nyota huyo alikosa sehemu kubwa ya msimu uliopita kutokana na majeraha ya paja. De Bruyne ametoa asisti 156 katika ligi tano bora za Ulaya tangu alipoanza kucheza katika mashindano hayo 2012/13. Ana angalau asisti tano zaidi kuliko mchezaji mwingine yeyote, huku Lionel Messi akiwa wa pili kwa 151.
Atalanta ilipata changamoto katika msimu wake wa kwanza bila Gasperini tangu 2015/16. Ilimaliza nafasi ya saba Serie A chini ya Raffaele Palladino baada ya Ivan Juric kutimuliwa Novemba, mwaka jana. Hata hivyo, kwa kuwa sasa Sarri ndiye kocha wa La Dea Atalanta ina asilimia 34.9 kumaliza ndani ya nne bora. Milan bado itakuwa na kumbukumbu mbaya ya kipigo dhidi ya Cagliari siku ya mwisho ya msimu uliopita, ambacho kiliifanya Rossoneri iondoke kwenye nne bora.
Mbali na kumteua Amorim, Milan pia imetoa ishara katika soko la usajili kwa kumsajili Goncalo Ramos kutoka PSG, ambapo mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alifunga mabao 45 katika mechi 131 akiwa Ligue 1, ingawa alianza mechi 54. Milan inapewa asilimia 30.7 kufuzu Ligi ya Mabingwa, huku Bologna ikiwa na 14.5 na Lazio 14.2 kumaliza ndani ya nne bora.
Nani kushuka Serie A?
Monza ilipanda Serie A kupitia mchujo wa Serie B, ikitoka sare 2-2 dhidi ya Catanzaro katika fainali, lakini ikapanda kutokana na kuwa na nafasi nzuri zaidi katika msimamo wa ligi. Hata hivyo, inatabiriwa kushuka daraja kwa asilimia 42.9 ikiwa ndiyo timu yenye uwezekano mkubwa zaidi wa kushuka kati ya timu zote za ligi. Monza ina mchezaji anayefahamika katika safu yake ya ushambuliaji, baada ya mshambuliaji wa zamani wa Milan na Fiorentina Patrick Cutrone kukamilisha uhamisho wa kudumu kutoka Como.
Cutrone amefunga mabao 28 na kutoa asisti tisa katika mechi 169 za Serie A kwenye maisha yake ya soka. Frosinone pia ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kushuka, ikiwa na uwezekano wa asilimia 40.7. Nafasi ya mwisho ya kushuka inaweza kuwa kati ya Venezia (33.7%) na Lecce (34.3%). Matumaini ya Venezia kuepuka kurejea Serie B yatategemea mchango wa Akor Adams aliyesajiliwa kutoka Sevilla.
Miongoni mwa wachezaji wa Sevilla msimu uliopita, Adams alikuwa kinara wa kufunga mabao 10, michango ya moja kwa moja ya mabao 14 na mashuti 63. Pia alitoa asisti nne, akiwa wa pamoja katika nafasi ya pili kwa idadi hiyo.
Lecce, kwa upande wake, iliepuka kushuka daraja msimu uliopita baada ya kushinda mechi tatu kati ya nne za mwisho na kupoteza moja kati ya sita za mwisho, ikiwa na ushindi mara tatu na sare mbili. Timu hiyo ilifunga mabao machache ya tatu katika Serie A msimu wa 2025/26, ikiwa na mabao 28, lakini imeongeza mshambuliaji Willem Geubbels ili kujaribu kutatua tatizo hilo. Mfaransa huyo ameanza vizuri maisha yake Lecce, akifunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 wa maandalizi ya msimu dhidi ya Monopoli.