Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serengeti Boys kuvunja rekodi ya Uswisi Kombe la Dunia

SERENGETI Pict

Muktasari:

  • Kwa kikosi cha kocha Elieneza Nsanganzelu, mashindano hayo ni zaidi ya kutimiza ndoto ya kufuzu, ni nafasi ya kuingia kwenye orodha ya mataifa yaliyotumia nafasi yao ya kwanza kufanya makubwa.

HISTORIA inaonyesha kwenye mashindano ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17 imekuwa na bahati kwa timu zinazoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Baadhi ya mataifa yaliyoingia kwenye mashindano hayo bila historia kubwa ya mafanikio yaliweza kuandika simulizi zilizozishtua dunia, huku mengine yakifika mbali kiasi cha kutwaa ubingwa.

Hiyo ndiyo nafasi inayosubiri Tanzania kupitia Serengeti Boys, ambayo Novemba 19 itaanza safari yake ya kwanza katika fainali za Kombe la Dunia la U-17 zitakazofanyika Qatar hadi Desemba 13, 2026.

Kwa kikosi cha kocha Elieneza Nsanganzelu, mashindano hayo ni zaidi ya kutimiza ndoto ya kufuzu, ni nafasi ya kuingia kwenye orodha ya mataifa yaliyotumia nafasi yao ya kwanza kufanya makubwa.


SERE 01

USWISI

Ukiangalia historia ya mashindano hayo tangu yalipoanzishwa mwaka 1985, mfano unaoweza kuipa Tanzania matumaini makubwa ni Uswisi ya mwaka 2009. Taifa hilo lilifika kwenye fainali hizo kwa mara ya kwanza kabisa, lakini halikuishia kushiriki tu, lilikwenda mbali zaidi na kutwaa ubingwa baada ya kuifunga Nigeria bao 1-0 katika mchezo wa fainali.

Uswisi ilifanya jambo ambalo halikuwa rahisi kutabirika, hasa ikizingatiwa ilikuwa inakutana na Nigeria, iliyokuwa mwenyeji na bingwa mtetezi. Bao la Haris Seferovic dakika ya 63 liliipa Uswisi taji lake la kwanza la dunia. Kilichotokea Nigeria ni ushahidi uzoefu wa kushiriki mashindano hayo si kigezo pekee cha kuamua timu itakayofanya vizuri.

Maandalizi, nidhamu na uwezo wa kutumia nafasi vinaweza kubadilisha historia.


SERE 02

IVORY COAST

Ivory Coast ni miongoni mwa mataifa yaliyotumia vizuri nafasi ya kwanza kushiriki Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17.

Ilifanya hivyo mwaka 1987 nchini Canada, ambako ilianza kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Korea Kusini, kabla ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Marekani na kuifunga Ecuador kwa matokeo kama hayo.

Matokeo hayo yaliifanya kumaliza hatua ya makundi ikiwa kileleni mwa kundi lake na kufuzu robo fainali.

Katika hatua ya robo fainali, Ivory Coast iliendeleza ubora wake kwa kuifunga Qatar mabao 3-0 na kutinga nusu fainali, ambako ilikutana na Umoja wa Kisovieti.

Hata hivyo, safari ya kutafuta ubingwa ilishindwa kuendelea baada ya kutandikwa kwa mabao 5-1. Pamoja na kipigo hicho, haikukata tamaa, kwani katika mchezo wa kuwania mshindi wa tatu iliifunga Italia mabao 2-1 baada ya dakika za nyongeza  na kumaliza katika nafasi ya tatu.


SERE 03

BAHRAIN

Bahrain nayo iliandika historia ya mashindano hayo iliposhiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1989 nchini Scotland. Ilianza kwa kishindo baada ya kuifunga Cuba mabao 3-0, kisha kuichapa Ghana bao 1-0 na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji Scotland.

Matokeo hayo yaliifanya kumaliza hatua ya makundi ikiwa kinara wa kundi, ikiwa na pointi tano kutokana na ushindi wa mechi mbili na sare moja.

Katika robo fainali, Bahrain ilikutana na Brazil na baada ya dakika 120 kumalizika bila mabao, ikashinda kwa penalti 4-1 na kufuzu nusu fainali.

Hata hivyo, ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Saudi Arabia na kushindwa kuingia fainali. Katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu, ilifungwa mabao 3-0 na Ureno na kumaliza nafasi ya nne.


SERE 04

UGANDA

Mfano mwingine ni Uganda katika mashindano ya mwaka 2025. The Cranes ilikuwa inashiriki kwa mara ya kwanza na ilifanikiwa kuvuka hatua ya makundi, kabla ya kuingia hatua ya 32 bora.

Katika hatua hiyo iliifunga Senegal kwa bao 1-0 na kufuzu hatua ya 16 bora, ikiwa ni mafanikio makubwa kwa taifa lililokuwa halijawahi kushiriki Kombe la Dunia katika ngazi yoyote.

Safari yao iliishia hatua iliyofuata baada ya kufungwa kwa penalti na Burkina Faso.

Uganda haikuwa timu pekee iliyovutia katika kundi la wageni wa mwaka huo. Jamhuri ya Ireland nayo ilifika hatua ya 16 bora katika ushiriki wake wa kwanza, huku Zambia ikifanikiwa kuingia hatua ya 32 bora.

Kwa maana nyingine, kati ya mataifa matano yaliyokuwa yakicheza kwa mara ya kwanza mwaka 2025, matatu yalivuka hatua ya makundi na kuingia kwenye hatua za mtoano.


SERE 05

MIFANO

Hiyo ndiyo mifano ambayo Serengeti Boys inapaswa kuitazama, hasa ikizingatiwa kuwa nayo haiji Qatar ikiwa haina kitu cha kujivunia. Tanzania ilipata tiketi ya Kombe la Dunia baada ya kumaliza nafasi ya pili katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 zilizofanyika Morocco mwaka huu.

Iliifikia hatua hiyo baada ya kuonyesha ushindani mzuri, ikiwemo ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Msumbiji katika mchezo wake wa ufunguzi na kuendelea mpaka fainali ambako ilipoteza kwa Senegal kwa penalti baada ya sare ya bao 1-1. Pia, kikosi hicho kina wachezaji waliothibitisha uwezo mkubwa katika mashindano ya Afrika. Dismas Athanasi alikuwa miongoni mwa vivutio vikubwa baada ya kufunga mabao matatu na kutwaa kiatu cha ufungaji bora.

Mwingine Issa Mussa Chole alikuwa mchezaji bora wa mashindano hayo. Hawa ni miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuwa na mchango mkubwa katika safari ya Tanzania.


SERE 06

NJIA NGUMU

Hata hivyo haitakuwa rahisi kwa Serengeti Boys kuvuka viunzi hivyo. Tanzania ipo Kundi I pamoja na Brazil, Costa Rica na Jamhuri ya Ireland.

Brazil ni moja ya mataifa yenye historia kubwa katika mashindano hayo, ikiwa imetwaa mataji manne, wakati Costa Rica imewahi kufika robo fainali mara nne. Ireland nayo ina uzoefu wa mashindano ya mwaka 2025 ilipofika hatua ya 16 bora. Hivyo, Serengeti Boys itahitaji kuonyesha kiwango kikubwa katika michezo yote mitatu.

Mchezo wa kwanza dhidi ya Costa Rica Novemba 21 utakuwa na umuhimu mkubwa katika kujenga mwelekeo wa safari ya timu hiyo, kabla ya kukutana na Brazil Novemba 24 na kumalizia dhidi ya Ireland Novemba 27.

Kwa mfumo wa mashindano ya mwaka huu wenye timu 48, nafasi ya kufuzu hatua ya 32 bora ipo kwa timu mbili za juu katika kila kundi pamoja na timu nane bora zilizomaliza nafasi ya tatu.

Kwa hiyo, Tanzania haihitaji kuanza safari ya Qatar kwa kujilinganisha na mataifa yenye mataji mengi, bali kutumia uwezo ilioonyesha Afrika na kuugeuza kuwa matokeo kwenye jukwaa hilo.

Uswisi ilionyesha kuwa mshiriki wa kwanza anaweza kuwa bingwa, Uganda na Ireland zikathibitisha kuwa mgeni anaweza kufika hatua ya 16 bora, huku Zambia ikionyesha kuwa hata hatua ya kwanza ya mtoano inaweza kuwa mafanikio ya kihistoria. Sasa ni zamu ya Serengeti Boys kuamua itaandikwa katika ukurasa upi wa historia hiyo.