Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dismas anaamini Tanzania itacheza robo fainali Kombe la Dunia

DISMAS Pict

Muktasari:

  • Kiungo mshambuliaji huyo aliyezaliwa mwaka 2011 alikwenda Morocco kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) 2026 akiwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika mashindano hayo.

AKIWA na umri wa miaka 14 tu, tayari kiungo Dismas Athanasi aling’ara katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana, AFCON U-17 Morocco 2026 na sasa anajiandaa kuandika historia nyingine Kombe la Dunia.

Kiungo mshambuliaji huyo aliyezaliwa mwaka 2011 alikwenda Morocco kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) 2026 akiwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika mashindano hayo.

Dismas alianza kwa kishindo baada ya kufunga bao katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Msumbiji, kabla ya kuendelea kung’ara na kumaliza mashindano akiwa na mabao matatu yaliyompa kiatu cha ufungaji bora.

Mafanikio hayo yalienda sambamba na safari ya kihistoria ya Tanzania iliyofika fainali na kumaliza mshindi wa pili baada ya kupoteza kwa penalti dhidi ya Senegal.

DIS 01

Akizungumza na FIFA kuhusu safari hiyo, Dismas anakiri hakukuwa na mchezo mwepesi, hasa kutokana na tofauti ya miili na nguvu kati yake na baadhi ya wapinzani aliokutana nao. Hata hivyo, anasema msaada wa wachezaji wenzake na imani waliyoonyesha kwake vilimsaidia kujiamini na kufanya vizuri.

“Wachezaji wengine walikuwa wagumu sana. Walikuwa na nguvu na miili mikubwa! Wenzangu walinisaidia kucheza vizuri. Walikuwa wanawasiliana nami sana.

“Pia wananiamini. Wakati mwingine nikiwa uwanjani, nahisi wanajua nitafunga! Nina uhakika asilimia 100 nitafunga! Pia wananiambia ninaweza kuwa bora zaidi, jambo linalonifanya nijikite zaidi katika mchezo,” anasema Dismas.


DIS 02

AJIFANANISHA NA HAZARD

Mbali na uwezo wake wa kufunga, Dismas anaonekana kuwa na mapenzi makubwa na soka la kushambulia, akieleza anaweza kucheza nafasi mbalimbali katika safu ya ushambuliaji, lakini kiungo mshambuliaji ndiyo nafasi anayopendelea zaidi.

Katika safari yake ya kuendelea kujifunza na kuboresha kipaji chake, kijana huyo anamtazama nyota wa zamani wa Ubelgiji, Eden Hazard, kama mfano wa kuigwa. Anasema anavutiwa na namna nyota huyo alivyokuwa akitumia kasi na ufundi wake kuvuruga safu za ulinzi za wapinzani, kutengeneza nafasi na kufunga mabao.

“Hazard ni mchezaji anayefanana na mimi. Anakimbilia mbele, anafunga mabao na kutengeneza nafasi. Napenda kumtazama na ninatumaini kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwake. Ndiye mchezaji ninayempenda zaidi,” anasema.

Hazard alikuwa miongoni mwa nyota walioiwezesha Ubelgiji kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, ambako alitwaa tuzo ya Mpira wa Fedha baada ya kumaliza nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha tuzo ya mchezaji bora wa mashindano hayo.


DIS 05

BRAZIL NI MTIHANI, ROBO FAINALI NDOTO

Dismas anasema akili yake kwa sasa iko Qatar ambako Tanzania itashiriki kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17. Ni hatua nyingine kubwa kwa Serengeti Boys baada ya kuonyesha uwezo wake katika mashindano ya Afrika.

Katika mashindano hayo, Tanzania imepangwa Kundi I pamoja na Brazil, Costa Rica na Jamhuri ya Ireland. Hata hivyo, macho mengi yataelekezwa kwenye pambano dhidi ya Brazil, mabingwa mara nne wa mashindano hayo na moja ya mataifa yenye historia kubwa katika soka la dunia.

Dismas anafahamu ukubwa wa wapinzani hao, hasa baada ya kusikia maelezo kutoka kwa makocha wake kuhusu uzoefu wa baadhi ya wachezaji wa Brazil katika timu za wakubwa za klabu zao.

DIS 04

“Nimewasikiliza makocha wangu na wanasema wachezaji wengi wa Brazil wamewahi kucheza katika timu za wakubwa za klabu zao. Nitahitaji kuzingatia sana mawazo yangu na kila nitakalofanya lazima nilifanye kwa weledi,” anasema.

Licha ya ukubwa wa changamoto inayowakabili, Dismas hana hofu ya kwenda Qatar, bali anaamini Tanzania inaweza kufanya vizuri zaidi ya ilivyofanya Morocco. Kijana huyo, ambaye anatarajia kutimiza miaka 15 Desemba 26, anasema ushiriki huo ni nafasi ya kipekee kwa kizazi chake kuweka alama katika historia ya soka la Tanzania.

“Tunajivunia sana kuwa wachezaji wa Tanzania tutakaocheza Kombe la Dunia U-17 kwa mara ya kwanza.

DIS 03

“Ninafikiri tutafanya vizuri na kucheza vizuri zaidi hata kuliko tulivyofanya katika AFCON. Ninaamini tunaweza kwenda mbali katika Kombe la Dunia. Natumaini labda tunaweza kufika robo fainali. Tutaona,” anasema Dismas.

Ni kauli inayodhihirisha ukubwa wa ndoto alizonazo kijana huyo. Baada ya kuanza kujitambulisha Afrika kwa mabao matatu na kiatu cha ufungaji bora, sasa anataka kuitumia Qatar kama jukwaa jingine la kuonyesha kuwa Serengeti Boys haijaenda kushiriki tu, bali ina uwezo wa kupambana na timu kubwa na kwenda mbali.