Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Soann - Nyota pekee U-17 anayekipiga Ufaransa

SOAN Pict

Muktasari:

  • Kiungo huyo ambaye mmoja wa wazazi wake ni Mtanzania na mwingine Mfaransa ni mchezaji pekee anayecheza nje kwenye kikosi cha nyota 21 walioitwa na kocha Elieneza Nsanganzelu.

WAKATI Serengeti Boys ikishuka kwenye viwanja vya Qatar kuandika historia ya kwanza ya Tanzania katika Fainali za Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17, miongoni mwa nyota wa kuangaliwa kwenye kikosi hicho ni Soann Adam Juma anayekipiga Grenoble Foot 38.

Kiungo huyo ambaye mmoja wa wazazi wake ni Mtanzania na mwingine Mfaransa ni mchezaji pekee anayecheza nje kwenye kikosi cha nyota 21 walioitwa na kocha Elieneza Nsanganzelu.

Tofauti na wachezaji wengi wa kikosi hicho wanaotoka katika klabu na akademi za ndani, Soann ana uzoefu wa mfumo wa soka la vijana barani Ulaya, akijijengea jina kupitia akademi za soka nchini Ufaransa.

Ni safari iliyomfikisha katika jukwaa ambalo vijana wengi hulitamani, kucheza Kombe la Dunia, huku akiwa sehemu ya kizazi cha Serengeti Boys kilichoweka rekodi ya kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi.


SOA 05

SAFARI YAKE UFARANSA

Safari ya Soann katika soka la ushindani nchini Ufaransa imehusisha vituo viwili muhimu vya maendeleo ya wachezaji, AS Saint-Etienne ambako walimkuza hadi mwaka 2024 kutimkia Grenoble Foot 38 ya vijana.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za wasifu wake wa soka, kabla ya kuonekana Grenoble, kiungo huyo alikuwa amepitia mfumo wa vijana wa AS Saint-Etienne, klabu yenye historia kubwa katika soka la Ufaransa.

Hatua iliyofuata ilikuwa kujiunga na Grenoble Foot 38, ambako aliendelea kujijenga kupitia kikosi cha vijana chini ya miaka 17.

Soann alianza kuonekana katika kikosi cha U-17 cha Grenoble msimu wa 2025/26, huku akitajwa kwenye kikosi kilichoanza mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Lyon Duchère Agosti 23, 2025.

Hiyo ilikuwa hatua muhimu katika safari yake, kwani ilimpa nafasi ya kuonyesha uwezo wake katika mashindano ya vijana nchini Ufaransa na kupambana na wachezaji wanaokulia katika mfumo huo wa soka.

Katika msimu huo, takwimu za BeSoccer zinamuonyesha akicheza mechi 16 za ligi ya U-17, akifunga mabao mawili na kutoa asisti tatu.


SOA 04

GRENOBLE YAMFUNGULIA

Kukua kwake katika mfumo wa soka la Ufaransa kumeendelea kumuweka katika mazingira ya ushindani mkubwa ndani ya Grenoble Foot 38.

Klabu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Ufaransa, Ligue 2, ina mfumo wa timu mbalimbali za maendeleo, ikiwamo kikosi cha B kinachotoa nafasi kwa vijana kuendelea kujiandaa kwa hatua ya juu zaidi. Kwa taarifa za maendeleo yake klabuni, Soann amepata nafasi ya kupandishwa katika mfumo wa kikosi cha wakubwa, akitarajiwa kuanzia timu ya B huku akifuatiliwa kwa ukaribu kwa ajili ya hatua zinazofuata.

Hiyo ni hatua inayoweza kuwa muhimu katika maisha yake ya soka, kwani inamuweka karibu zaidi na mazingira ya ushindani wa soka la wakubwa.


SOA 03

SERENGETI BOYS

Pamoja na kukua nchini Ufaransa, Soann alipata nafasi ya kujiunga na Serengeti Boys na kuwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) Morocco 2026. Alikuwa mchezaji  pekee kutoka nje ya Tanzania katika kikosi hicho, akileta uzoefu wa soka la Ufaransa kwenye timu iliyokuwa na jukumu la kuandika historia.

Safari ya Morocco ilikuwa ya mafanikio makubwa kwa Serengeti Boys, iliyofika fainali kwa mara ya kwanza na kupata tiketi ya kucheza Kombe la Dunia baada ya kumaliza ikiwa mshindi wa pili.


SOA 02

KAZI IPO QATAR

Baada ya kukiwasha Morocco, Soann amejumuishwa tena kwenye timu iliyopo Qatar akiwa sehemu ya kikosi cha Serengeti Boys kitakachocheza Kombe la Dunia U-17.

Ni hatua inayomuweka katika mazingira tofauti kabisa na yale aliyoyazoea katika mashindano ya vijana nchini Ufaransa. Sasa anakutana na wachezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani, huku macho ya mashabiki na wadau wa soka yakielekezwa kwenye kipaji cha vijana hao.

Serengeti Boys ilikuwa London kwenye maandalizi ya mashindano ya Kombe la Dunia na pia ilipata nafasi ya kucheza mechi mbalimbali za kirafiki. Katika mechi dhidi ya Argentina kwenye Vertex Cup iliyochezwa London Oktoba 2026, alifunga bao kwenye kipigo cha mabao 3-2 cha Tanzania.

SOA 01

Pia, Novemba 9, 2026, alifunga bao katika sare ya mabao 2-2 dhidi ya Venezuela kwenye mashindano ya Dubai Youth Challenge, ambayo Serengeti Boys inayatumia kujiandaa na Kombe la Dunia. Hiyo inaonyesha namna kiungo huyo anavyoendelea kuwa sehemu ya mipango ya timu katika maandalizi ya mashindano makubwa.