Selemani Makanya afunguka siri Simba Queens kubeba taji mara 5, vita na Yanga
Muktasari:
- Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, Makanya amezungumzia mambo mengi kuanzia namna anavyowapata wachezaji wa kigeni, siri ya kuwapiga Yanga Princess kwenye usajili na changamoto za bajeti zinazoumiza klabu.
UKITAKA kujua mafanikio ya soka la wanawake hapa nchini, huwezi kuacha kuitaja Simba Queens. Lakini nyuma ya mafanikio ya mabingwa hao mara tano wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), kuna mtu anaitwa Selemani Makanya. Huyu ndiye mratibu na mpishi mkuu wa mikakati ya timu hiyo.
Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, Makanya amezungumzia mambo mengi kuanzia namna anavyowapata wachezaji wa kigeni, siri ya kuwapiga Yanga Princess kwenye usajili na changamoto za bajeti zinazoumiza klabu.
UBINGWA MARA 5
Simba Queens imekuwa ikitawala soka la wanawake kwa muda mrefu. Makanya anasema msimu uliopita ulikuwa wa ushindani mkubwa, lakini siri ya kuchukua ubingwa bila kupoteza mechi ilitokana na kurekebisha makosa ya misimu miwili iliyopita ambapo walikosa taji kwenye mechi za mwisho.
“Ubingwa wa mara tano ni mafanikio makubwa, lakini malengo yetu kama klabu ni kuwa mabingwa kila msimu.
“Siri kubwa ya kuwa na mafanikio hayo ni mfumo wa Simba ambao unajali mahitaji ya timu na kuboresha pale panapolegalega,” anasema.
USAJILI NA SKAUTI
Makanya ni mtaalamu wa kunusa vipaji. Anasema tofauti yake na viongozi wengine ni kwamba yeye hafanyi skauti ligi inapomalizika.
“Mimi skauti yangu naifanya wakati ligi inaendelea. Tukifika raundi ya pili, tayari nishajua nani anakuja Simba na nani anaondoka,” anasisitiza.
“Hata zile sajili za kimataifa huwa nahudhuria baadhi ya mechi kama zile za Kenya, Uganda na wachezaji wengine huwa nawaangalia timu yetu ya taifa ikicheza hapa.”
Kuhusu bajeti, Makanya amekiri kuwa soka la wanawake sasa ni gharama kubwa hususani kwenye eneo la usajili na vibali. “Mpira wa wanawake unakimbizana na timu ndogo za Ligi Kuu. Kumiliki wachezaji 12 wa kigeni pekee, kulipia vibali vyao (TFF na Serikali), ni mamilioni ya fedha,” anasema.
“Vibali vya TFF pekee kwa wachezaji wa kigeni ni takriban Sh48 milioni, sasa fikiria wachezaji wote 12 ni kiasi gani.”
ALIVYONASA SAINI YA FASILA
Moja ya sehemu ya kusisimua kwenye mahojiano haya ni jinsi Makanya alivyopambana kumnasa mchezaji Fasila Adhiambo kutoka Kenya.
Mratibu huyo anasema ilikuwa kazi ngumu kwani wazazi wake walitaka akajiunge na Jeshi (Ulinzi Starlets) nchini Kenya ili apate ajira ya kudumu.
“Nilienda Kenya zaidi ya mara tatu. Safari ya mwisho nilitoka Nairobi nikasafiri kwa saa tisa hadi ‘Western’ karibu na mpakani. Nililala nyumbani kwao kwa sababu mimi Kenya ni kama nyumbani karibu timu zote, wachezaji na makocha wananifahamu,” anasimulia Makanya.
“Baada ya kukaa na familia, bibi, mama, na dada zake, hatimaye walinielewa dhamira yangu na kusaini mkataba. Leo hii, Fasila ni bingwa na amesaidia familia yake kwa kiasi kikubwa.”
VITA NA YANGA
Linapokuja suala la ushindani na watani wao wa jadi, Yanga Princess, Makanya anasema wamekutana kwenye dili nyingi za wachezaji lakini Simba imekuwa ikishinda kila mara.
“Mimi hawawezi kushinda mbele yangu. Nikimtaka mchezaji nitamchukua, hata JKT Queens wanajua hilo,” anasema kwa kujiamini.
Alitolea mfano wa usajili wa beki wa kushoto, Asha Omari kutoka Yanga Princess uliokuwa na changamoto baada ya klabu yake ya zamani kudai ana mkataba ilhali ulikuwa umeisha.
Ma k anya anasema uko mavu wa mchezaji huyo ulimsaidia kujiunga na Simba licha ya shinikizo kubwa lililokuwepo.
“Huwezi kuamini yule mtoto alikuwa na akili sana kwa sababu timu yake ilikuwa inasema bado ina mkataba naye, lakini kumbe hakuwa amesaini mkataba mpya, nilivyojiridhisha kuwa kweli tukamchukua na hadi sasa tuko naye.”
MAKOCHA WAZAWA VS WAGENI
Kumekuwa na changamoto ya timu kubwa za Simba na Yanga kuwaamini zaidi makocha wa kigeni kuliko wazawa. Simba iliwahi kuwa na Yussif Basigi kutoka Ghana msimu wa 2024-2025 ambaye hakufanikiwa kubeba taji. Charles Lukula msimu wa 2022-2023 na wengineo.
Baada ya kutofanikiwa kwa makocha wa kigeni, ikaanza kuwaamini Sebastian Nkoma, Juma Mgunda na sasa timu ikiwa chini ya Mussa Hassan ‘Mgosi’.
Makanya anasema walijaribu makocha wa kigeni zaidi ya mara mbili lakini hawakufanikiwa.
“Hakuna haja ya kubeba mzigo wa gharama kwa makocha wa kigeni wakati mzawa anafanya vizuri,” anasema.
CHANGAMOTO
Pamoja na mafanikio hayo, Makanya ametoa rai kwa makampuni kujitokeza kudhamini ligi ya wanawake. Anasema timu nyingi ndogo zinapitia changamoto kwa sababu zinategemea mifuko ya watu binafsi na mechi ni bure hazina viingilio.
“TFF inaweka juhudi, lakini tunatamani ligi yetu iwe kama ya wanaume naamini ikiwa na wadhamini itakuwa bora zaidi ya hapa kwa sababu tayari imekuwa ila bado kuna timu zinapambana hata usafiri hakuna,” anasema.
TABIA ZA WACHEZAJI
Makanya amegusia pia tabia za watoto wa kike kambini. Kuhusu wachezaji kuiga mionekano ya kiume, Makanya anasema wanajaribu kuwaelimisha kuwa maisha ya mpira ni mafupi na baadaye watahitaji kutengeneza familia.
“Tunajaribu kuwapa elimu na hasa kocha huwa anazungumza na wachezaji kuhusu mionekano yao na tunashukuru baadhi wanatuelewa kwa sababu kwenye kundi la wachezaji kama hilo kila mmoja amelelewa mzingira yake,” anasema
UJAUZITO KWA WACHEZAJI
Kuna idadi ndogo ya wachezaji wa kike ambao nje ya kazi yao wamejenga familia kama kuolewa na kuwa na watoto kama ilivyo Ulaya ambapo kumekuwa na wimbi kubwa.
Mfano kwa Tanzania, Asha Mwalala ni miongoni mwa wachezaji aliyeolewa na beki wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars, Hassan Kessy na kubarikiwa mtoto mmoja.
Mwanaspoti ilipomuuliza mratibu huyo kama kwenye mikataba na wachezaji inawazuia kuwa na familia, alisema: “Mchezaji akipata ujauzito, mkataba hausitishwi. Anapewa wiki 14 za mapumziko ya uzazi na huduma zingine zinaendelea.”
Alitolea mfano wa aliyekuwa mchezaji wao, Danai Bhobho ambaye licha ya kuwa na watoto watatu lakini alikuwa na kiwango bora ambacho kilimfanya kuwa mchezaji muhimu kikosini akionyesha uwezo mzuri.
MILIONI MOJA
Kwa mujibu wa Makanya, mchezaji wa kike katika klabu kubwa kama Simba anaweza kufikisha mshahara wa hadi Sh1 milioni kwa mwezi kwa kima cha chini.
Hii inaonyesha tofauti kubwa iliyopo ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo soka la wanawake lilikuwa bado linapambana kupata nafasi na thamani inayolingana na mchango wa wachezaji.
Makanya anasema, fedha hizo zimeanza kubadilisha maisha ya wachezaji ambao sasa wanaweza kujitegemea, kusaidia familia na ndugu zao na wengine kufikia hatua ya kujenga nyumba.
“Mpira huu sasa hivi unalipa. Kuna watu wamejenga, kuna watu wanaendesha familia zao na kusaidia ndugu kupitia soka la wanawake,” anasema Makanya.
USAJILI MILIONI 20
Ukiachana na mishahara ya kila mwezi, Makanya anafichua kuwa ‘signing fee’ (pesa ya usajili) imekuwa ikivunja rekodi kila msimu. Anasema kwa sasa mchezaji anaweza kuvuta hadi Sh20 milioni kama dau la usajili kwa msimu mmoja tu.