Sapoti ya video itamaliza janjajanja
Muktasari:
- Hii sapoti ya video ndugu zangu itapunguza mbinu fulani hivi ambazo hazikuwa nzuri lakiji zikawa zinatumika katika harakati za baadhi ya timu kutafuta matokeo.
WALE ambao wamekuwa wakitegemea kupata matokeo kwa njia za samjosamjo kwenye Ligi Kuu sasa wabadilike.
Hii sapoti ya video ndugu zangu itapunguza mbinu fulani hivi ambazo hazikuwa nzuri lakiji zikawa zinatumika katika harakati za baadhi ya timu kutafuta matokeo.
Au nyie mnaonaje ndugu zangu si inatakiwa iendelee ili timu zipate matokeo yanayostahili badala ya kurudi katika yale matokeo yetu ya mang’amung’amu ambayo wote hatufurahishwi nayo.
Kwa hapa kijiweni sisi wote tunaunga mkono mambo ya video hayo yanayotumiwa na marefa kutoa uamuzi wa mechi maana tushaanza kuona matunda yake chanya.
Zile timu zetu kubwa pengine kusingekuwa na hicho kitu, zingekuwa zimeshanufaika katika hizi mechi za mwanzo kwa matukio ambayo hazikupaswa kunufaika lakini video zimesaidia.
Kadi nyekundu mbili ambazo Simba wameonyeshwa, Yanga kukataliwa goli kwa tukio la ofsaidi na Polisi Tanzania kupewa penalti dhidi ya Azam FC isingekuwa rahisi bila usaidizi wa video.
Aah TFF na Bodi ya Ligi wamenogesha sana msimu huu na hili jambo na sisi wote tunawapongeza maana ligi haina konakona sasa.
Sema sasa sisi tunajuana hasa kunapokuja jambo kama hili la kupunguza upataji matokeo kwa njia za panya lazima wataibuka watu wa kuhujumu mfumo.
Narudia tena tunajuana bhana hivyo tujitahidi kujishikilia na kuvumilia badala ya kuanza kutengeneza mazingira ya kukwamisha matumizi ya video kwa marefa.