Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpo? FVS yaanza kutoa majibu Ligi Kuu

FVS Pict

Muktasari:

  • Katika mechi zilizochezwa Agosti 14, 2026 hadi Agosti 16, 2026, FVS ilihusika katika matukio manane yanayogusa moja kwa moja matokeo ya mechi, yakiwamo mabao, penalti, kuotea na kadi nyekundu.

TEKNOLOJIA ya FVS (Football Video Support) imeanza kutoa majibu katika Ligi Kuu Bara ya namna uamuzi wa waamuzi unavyoweza kusaidiwa wakati wa mechi, kama ilivyoshuhudiwa katika mechi za kwanza za msimu wa 2026-2027 kwa matukio muhimu kupitiwa kwenye mfumo huo.

Katika mechi zilizochezwa Agosti 14, 2026 hadi Agosti 16, 2026, FVS ilihusika katika matukio manane yanayogusa moja kwa moja matokeo ya mechi, yakiwamo mabao, penalti, kuotea na kadi nyekundu.

Matukio hayo yameanza kutoa picha ya namna teknolojia hiyo itakavyoweza kutumika katika ligi, pia yameonyesha jambo lingine muhimu, matumizi ya FVS hayalengi kubadilisha kila uamuzi wa mwamuzi, bali humpa nafasi ya kupata taarifa zaidi pale tukio linapokuwa na mashaka au linaweza kuwa na athari kubwa kwenye mchezo.

FV 03

KADI YA DUCHU

Miongoni mwa matukio makubwa zaidi ya raundi ya kwanza lilitokea katika mechi ya Kagera Sugar dhidi ya Simba, Agosti 16, 2026 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera na kumalizika kwa Simba kushinda mabao 2-0.

Mwamuzi wa mchezo huo, Saad Mrope, alifanya marejeo ya tukio la David Kameta ‘Duchu’ la kumfanyia madhambi beki wa Kagera Sugar, David Luhende.

Tukio hilo lilikuwa miongoni mwa yale ambayo kwa mwonekano wa kwanza yanaweza kuwa magumu kwa mwamuzi kuyatathmini kikamilifu kutokana na kasi ya mchezo na nafasi aliyokuwa nayo wakati tukio likitokea.

Baada ya kupata fursa ya kulitazama tena kupitia FVS, Mrope alichukua hatua ya kumwonyesha Duchu kadi nyekundu ya moja kwa moja, hivyo Simba kulazimika kuendelea na mechi ikiwa pungufu.

FV 02

SHALULILE NA LUKINDO

Katika mchezo wa Namungo dhidi ya Yanga, uliochezwa Agosti 15, 2026 kwenye Uwanja wa Majaliwa, mkoani Lindi na kumalizika kwa Yanga kushinda mabao 3-1, FVS ilitumika kwenye matukio mawili yaliyohusisha nafasi za kuotea.

Dakika ya 58, Shalulile alifunga bao ambalo mwamuzi wa mchezo huo Katanga Hussein kutoka Tabora alilikataa kwa tafsiri ya mfungaji aliotea, lakini Yanga iliomba marejeao. Hata hivyo, baada ya tukio hilo kufanyiwa marejeo, ilionekana mwamuzi alikuwa sahihi katika uamuzi wake wa awali, hivyo halikuhesabika kuwa bao.

Lakini dakika ya 75, FVS ilitumika tena baada ya Namungo kupata bao kupitia Herbert Lukindo. Kulikuwa na mashaka kama Lukindo alikuwa ameotea wakati alipofunga. Mwamuzi alishaamuru liwe bao, lakini Yanga ikaomba marejeo ambapo mwisho wa siku, uamuzi wa mwamuzi tena ukabaki kuwa sahihi. Bao hilo likathibitishwa kuwa halali.

FV 05

PENALTI ZILIVYOFUNIKWA

Mechi nyingine oliyokuwa na matumizi makubwa ya FVS ni ya Polisi Tanzania dhidi ya Azam, Agosti 15, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mwamuzi wa mechi hiyo, Hans Mabena alilazimika kupitia matukio mawili yaliyohusisha penalti.

Dakika ya 75, Henock Molia wa Azam, aliangushwa eneo la hatari na baada ya marejeo ya tukio hilo, matajiri hao wa Chamazi walipewa mkwaju wa penalti ambao ulifungwa na Abdul Suleiman 'Sopu'.

Dakika za mwisho za mechi zikaleta tukio lingine. Taiwo Abdulrafiu, raia wa Nigeria mwenye umri wa miaka 24 ambaye ni mchezaji mpya wa Azam FC, alihusika katika tukio la kumuangusha Baraka Mwambule ndani ya eneo la hatari.

Baada ya marejeo, mwamuzi aliamua kuwa Polisi Tanzania ilistahili penalti. Anwar Jabir akafunga dakika ya 89 na kuifanya timu hiyo isawazishe.

Matukio hayo yote kabla ya kuamuliwa na FVS, yalionekana kwamba hayakustahili kuwa penalti, lakini teknolojia ikatumika kutenda haki.

FV 04

BAO LA CHIRWA

Agosti 14, 2026, katika mchezo wa Mbeya City dhidi ya Geita Gold, uliomalizika kwa Geita Gold kushinda bao 1-0, FVS ilitumika katika tukio la bao la Obrey Chirwa.

Mbeya City iliomba marejeo kwa kuwa kulikuwa na mashaka kama Chirwa alikuwa ameotea wakati bao hilo linapatikana.

Mwamuzi tayari alikuwa ameliona bao hilo kuwa halali, lakini baada ya tukio kupitia FVS, uamuzi huo uliendelea kuwa sahihi. Bao likaendelea kusimama na Geita Gold ikaondoka na pointi tatu.

FV 01

FVS NA TARATIBU ZA KUOMBA MAREJEO

Katika mchezo wa Pamba dhidi ya Dodoma Jiji, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, kulikuwa na tukio lililoonyesha umuhimu wa kuelewa taratibu za matumizi ya FVS.

Dakika ya 23, Deogratius Judika Mafie aliifungia Pamba bao la kusawazisha. Baada ya bao hilo, wachezaji wa Dodoma Jiji wakiongozwa na nahodha wao, Mwana Kibuta, walimzonga mwamuzi wakimtaka afanye marejeo ya tukio hilo.

Kanuni zinabainisha kwamba, wachezaji hawapaswi kutumia namna hiyo kumlazimisha mwamuzi kufanya marejeo. Kutokana na tukio hilo, Kibuta alionyeshwa kadi ya njano.

Kocha wa Dodoma Jiji, Vincent Mashami aliomba marejeo kwa utaratibu unaotakiwa. Tukio hilo lilipopitiwa kupitia FVS, ilionekana kuwa bao la Mafie lilikuwa halali. Bao hilo likaendelea kusimama na Pamba ikapata sare ya 1-1.


WASIKIE WADAU

Mwamuzi wa zamani, Juma Mwakalukwa kutoka Tanga, alisema: “FVS ni msaada mkubwa kwa mwamuzi hasa kwenye matukio ambayo yanatokea kwa kasi na yanaweza kuwa magumu kuyaona kwa wakati. Lakini mwamuzi hatakiwi kutegemea teknolojia kwa kila uamuzi. Lazima awe na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi kwa kile anachokiona uwanjani, huku FVS ikiwa ni nyenzo ya kumsaidia pale kunapokuwa na shaka katika tukio muhimu.”

Aliongeza; “Kwa upande wa timu, uwepo wa FVS unaongeza imani kwamba matukio muhimu yanaweza kuangaliwa tena. Lakini jambo muhimu ni wachezaji na makocha kufahamu vizuri taratibu zake. Huwezi kuona tukio na kuanza kuwazunguka waamuzi ukitaka video itumike. Kuna utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa na kila timu inapaswa kuuelewa.”

Kwa upande wake, nyota wa zamani wa Yanga na Toto Africans ya Mwanza, Ladislaus Mbogo, alisema: "Raundi ya kwanza imeonyesha FVS inaweza kubadilisha namna tunavyoangalia maamuzi ya ligi, cha muhimu si idadi ya maamuzi yaliyobadilishwa, bali ni uwezo wa teknolojia kumpa mwamuzi ushahidi wa ziada kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho. Kama mfumo huu utatumika kwa usahihi na kwa uwazi, unaweza kuongeza kiwango cha uaminifu katika mashindano.”


KANUNI INAVYOSEMA

Kanuni ya 20 ya Ligi Kuu toleo la mwaka 2026 inazungumzia Matumizi ya Teknolojia ya Video Support System (VS). kanuni hiyo yenye vifungu 11, inafafanuzi matumizi hayo ya VS yanavyokuwa kama inavyobainishwa hapa:

(1) Katika kuondoa utata wa maamuzi kutakuwa na matumizi ya teknolojia ya Video Support System (VS) ambayo itatumiwa na mwamuzi wa mchezo ili kujiridhisha na tukio ambalo maamuzi yake yatakuwa yamelalamikiwa na timu wakati wa mchezo husika.

(2) Maamuzi ambayo yatahitaji matumizi ya VS ni yenye utata juu ya maamuzi yafuatayo: goli au siyo goli, penati au siyo penati, kosa linastahili kadi nyekundu ya moja kwa moja au kadi ya pili ya njano, kumtaambua mchezaji mwenye hatia ya kosa endapo kuwakuwa na malalamiko kuwa mwamuzi amemwadhibu mchezaji asiye na hatia.

(3) Matumizi ya VS yatafanywa na mwamuzi pale tu ambapo timu inayodhani itathirika na maamuzi hayo itaomba mwamuzi ajiridhishe kuhusu kufanyika kwa tukio husika kwa kurejea picha za tukio hilo kwenye VS.

(4) Kocha mkuu wa timu au kiongozi mwingine wa juu kwenye benchi la ufundi la timu inayolalamika ndio watakaokuwa na haki ya kuwasilisha maombi ya marejeo ya picha katika VS kwa kuwasiliana na mwamuzi wa akiba (fourth official).

4.1 Iwapo mchezaji atakuwa na mtazamo kuwa tukio linahitaji marejeo katika VS, mchezaji atawajibika kuwasiliana kwa ishara na Kocha Mkuu au kiongozi mwingine wa benchi la ufundi ili Kocha au kiongozi huyo aweze kuwasilisha lalamiko hilo kwa mwamuzi wa akiba.

4.2 Itakuwa ni marufuku kwa mchezaji yeyote kumkabili mwamuzi kwa nia ya kuomba au kushinikiza marejeo ya tukio kwenye VS. Mchezaji atakayekiuka masharti ya kifungu hiki ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 17:62.

(5) Malalamiko na maombi ya marejeo (VS review) lazima yafanywe haraka iwezekanavyo ndani ya dakika moja tangu tukio hilo litokee au kabla mwamuzi hajaruhusu mchezo kuendelea baada ya tukio husika kufanyika. Malalamiko yakichelewa kuwasilishwa, mwamuzi msaidizi hatawasilisha lalamiko kwa mwamuzi wa mchezo. Mwamuzi wa mchezo atakuwa na wajibu wa kupuuza wasilisho la malalamiko yaliyowasilishwa nje ya muda na mwamuzi hatasimamisha mchezo au kubadili maamuzi ya awali kwa namna yoyote.

(6) Iwapo katika mazingira yoyote mwamuzi atakuwa na mashaka na tukio lolote ambalo halijalalamikiwa, anaweza kurejea tukio hilo kwenye VS ili kujiridhisha ufanyikaji wa tukio ili achukue hatua stahiki kuhusu tukio hilo.

(7) Baada ya kupokea malalamiko, mwamuzi msaidizi atawasiliana na mwamuzi wa mchezo (main referee). Iwapo mchezo ulikuwa unaendelea baada ya tukio linalolalamikiwa, mwamuzi atasimamisha mchezo na kwenda kujiridhisha katika VS juu ya uhalali/ukweli wa maamuzi ya tukio husika katika eneo uliposimikwa mtambo wa VS.

(8) Wakati wa marejeo ya tukio katika VS, mwamuzi atasaidiwa na mafisa wa mfumo (floor manager wa mrusha matangazo akishirikiana na afisa wa TFF/TPLB watakaokuwepo uwanjani kumsaidia mwamuzi kurejesha nyuma picha za tukio hilo (replay) kwa muonekano wa pande mbalimbali (different camera angles) kwa kadri inavyowezekana kwa wakati huo.

(9) Maamuzi ya awali ya mwamuzi hayatabadilika mpaka pale ambapo itathibitika wazi na pasipokuwa na utata wowote kuwa maamuzi ya awali yalikuwa na makosa. Iwapo marejeo ya picha kwenye VS bado yanaacha utata kuhusu uhakika na uhalisia wa tukio linalolalamikiwa, maamuzi ya awali yatabaki kama yalivyo.

(10) Ili kuondoa utata wa uhalali wa goli lililofungwa, kila baada ya goli kufungwa, mwamuzi wa akiba (fourth official) atafanya rejea (review) ya tukio hilo kwenye VS na kuwasiliana na mwamuzi wa mchezo endapo kuna kosa lilitendeka kabla ya goli kufungwa. Iwapo kutakuwa na mgongano wa misimamo kati ya alichokiona mwamuzi na taarifa ya mwamuzi msaidizi, mwamuzi wa mchezo ataondoa utata kwa kufanya marejeo yeye mwenyewe ili kujiridhisha na maamuzi yake yatakuwa ya mwisho.

(11) Iwapo mfumo wa VS utakuwa na hitilafu, mchezo utaendelea bila uwepo na matumizi ya VS. Makocha na manahodha wa timu husika watajulishwa kuhusiana na hitilafu hiyo kabla ya kuanza kwa mchezo au baada ya kutokea kwa hitilafu.