Prime
Sakata la ‘Ninju’ Yanga, azam FC liko hivi
Muktasari:
- Kwa niaba ya mchezaji, mkataba huu ulisainiwa na mlezi wake, anayeitwa Abraham Nizar Othman.
AGOSTI 6, 2024 Azam FC ilimpa kijana Abubakar Nizar Othman ‘Ninju’ mkataba wa malezi, yaani wa akademi, wa miaka mitatu ambao ulitakiwa kukoma mnamo Agosti 5, 2027.
Kwa niaba ya mchezaji, mkataba huu ulisainiwa na mlezi wake, anayeitwa Abraham Nizar Othman.
Haya yote yalikuja baada ya familia ya mchezaji kuridhia kijana wao kulelewa kwenye akademi ya Azam.
Familia iliandika barua rasmi kuiruhusu Azam FC kumchukua kijana na kumlea ili kuendeleza kipaji chake.
Mama mzazi wa mchezaji, Hamida Jaha Ameir, mlezi wa mchezaji, Abraham Nizar Othman pamoja na msimamizi wa mchezaji, Salum Rashid Salum, waliweka saini zao kwenye barua hiyo.
Maana yake, Azam ilikabidhiwa kwa maandishi dhamana ya kumlea kijana Abubakar Nizar Othman.
Kijana huyo maarufu a.k.a Ninju, alitokea akademi ya An Nour Football Club ya Zanzibar.
Akademi hiyo pia iliridhia kwa barua rasmi Ninju kujiunga na Azam FC.
Kwa hiyo baada ya familia kuandika barua ya ridhaa na akademi yake kuridhia, ndio Azam FC ikampa mkataba ambao pia ulisainiwa na mlezi wake ambaye ni mwanafanilia, kama ilivyoelezwa huko juu.
Januari mwaka huu klabu ya JKU ya Zanzibar ikamuomba mchezaji huyo kwa mkopo wa miezi sita.
Akiwa JKU akashiriki mashindano ya Kombe la Muungano yaliyofanyika kisiwani Pemba Aprili mwaka huu, ambalo Yanga ililibeba kwa kuifunga JKU katika mechi ya fainali.
Huko kijana Nizar aling’ara sana kuanzia mechi yao ya kwanza dhidi ya Singida Black Stars.
Licha ya kuisaidia timu yake kushinda kwa changamoto ya mikwaju ya penalti, yeye binafsi alipoteza penalti yake.
Sio kwamba alipiga nje, au kipa alidaka, hapana...alikosea sheria.
Wakati anataka kupiga, alipoufikia mpira, akatishia kisha akapiga...akafunga.
Lakini sheria ya upigaji penalti inakataza mpigaji kutishia akiwa ameshafika kwenye mpira.
Anatakiwa kutishia kabla ya hatua ya mwisho ya kuufikia mpira.
Kosa hili adhabu yake ni kufutiwa penalti na kadi ya njano...ndicho kilichomtokea.
Hata hivyo, JKU ilishinda na ikaendelea kushinda hadi ikafika fainali iliyowakutanisha na Yanga.
Japo walipoteza mchezo huo, lakini bado Ninju alicheza vizuri sana na haikuwa ajabu aliposhinda tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa mashindano.
Viongozi wa Yanga, akiwemo Rais Hersi Said, walimtafuta baada ya mechi na kufanya naye mazungumzo mafupi na kupiga naye picha.
Baada ya mashindano hayo, Azam ikamuita Chamazi aje ashiriki mashindano maalumu ya kusaka vipaji.
Mashindano hayo yaliandaliwa na Azam FC na kuzishirikisha timu zake za vijana tu.
Wasaka vipaji kutoka klabu kadhaa vza Ulaya walialikwa kuja kuangalia vipaji.
Mashindano hayo yalipoisha, akarudi JKU kumalizia mkopo wake.
Msimu wa soka Zanzibar ulipoisha, JKU wakamrudisha Azam FC.
Alipaswa kuripoti Azam Agosti 10, siku ambayo wachezaji wote wa timu za vijana wanapaswa kurudi kambini.
Lakini kabla tarehe hiyo haijafika, akatangazwa kusajiliwa na Yanga.
Azam FC wakawasiliana na JKU kujua kama kuna taarifa yoyote upande wao.
JKU wakasema wao hawahusiki, kwani walishamtaarifu kwamba anapaswa kurudi klabuni kwake Azam FC punde tu msimu ulipoisha.
Baada ya hapo ndipo Azam FC wakapeleka barua rasmi ya malalamko kwa mamlaka za mpira, TFF, na kuwajulisha Yanga wenyewe.
Abubakar Nizar Othman au Ninju ni kipaji cha hali ya juu chenye kuzimudu namba zote za nyuma, kuanzia kiungo wa ulinzi.
Alizaliwa Julai 12, 2009 kwenye hospitali ya Mombo, Tanga. Leo, Jumanne ya Agosti 12, 2025 anafikisha miaka 16 na mwezi mmoja kamili. Mojawapo ya malalamiko yake klabuni Azam FC ni mkataba wa timu kubwa. Anajihisi ameshakua vya kutosha kuweza kupewa mkataba rasmi wa timu kubwa.
Lakini Azam FC imekuwa ikimwambia asubiri kwani hata timu ya chini ya miaka 20 hajapandishwa. Alianzia timu ya chini ya miaka 15 akapanda ile ya chini ya miaka 17.