Safari ya miaka 57 ya Tanzania na Olimpiki

Muktasari:
NI miaka 57 sasa tangu Tanzania ilipoanza kushiriki michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza mwaka 1964.
NI miaka 57 sasa tangu Tanzania ilipoanza kushiriki michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza mwaka 1964.
Wakati huo ilijulikana kama timu ya Tanganyika, wanariadha Pascal Mfyomi, Hassan Chabanga Dyamwale, Omari Abdallah na Daniel Thomas ndiyo Watanganyika wa kwanza kushiriki Olimpiki.
Hiyo ilikuwa ni baada ya miaka mingi ya michezo hiyo iliyoanzia Ugiriki ya Kale kufanyika.
Historia inaonyesha rekodi za mwanzo za michezo hiyo zilipatikana kwenye safu za marumaru za Uigiriki zilizochorwa mwaka 776 KK, japo inaelezwa michezo hiyo huko Ugiriki ilifanyika mapema zaidi kuliko tarehe hii.
Historia ya Olimpiki ipo takribani miaka 2800, hata hivyo inaelezwa mnamo 394 BK, michezo hiyo ilipigwa marufuku na mtawala wa Kirumi, ambaye hakupenda mashindano kama hayo.
Olimpiki ya kisasa
Olimpiki ya zama hizi ilianza mwaka 1896 huko Ugiriki, ilianzishwa na Mfaransa, Pierre de Coubertin.
Michezo hiyo haijawahi kuahirishwa tangu wakati huo, japokuwa haikufanyika mwaka 1916, 1940 na 1944 kwa sababu ya vita mbili za duniani.
Pierre de Coubertin anatajwa kama mwanzilishi wa michezo ya kisasa ya Olimpiki ambayo ina nembo za ringi tano zilizoungana na kuwa na rangi tano tofauti.
Rangi ya bluu ni ishara ya bara la Ulaya, nyeusi ni Afrika, nyekundu ni Amerika, njano ni Asia na kijani ni ishara ya Australia.
Bendera ya Olimpiki ina rangi nyeupe ambayo ni ishara ya amani, hutumika wakati wa kufungua na kufunga michezo hiyo na kisha kuhamishiwa katika jiji ambalo Olimpiki ijayo itafanyika miaka minne baadaye.
Mila ya zamani ilikuwa kuwasha moto wakati wa Olimpiki, mila hiyo imeendelea hadi sasa ambapo Tochi ya Olimpiki huwashwa miezi michache kabla ya kuanza kwa mashindano na msimu uliopita kwenye michezo ya Rio 2016 nchini Brazil, Tochi ya Olimpiki iliwashwa huko Ugiriki Aprili mwaka huo.
Tochi hiyo hukabidhiwa kwa mmoja wa wanariadha bora, ambaye huibeba kupitia miji ya Ugiriki, na kisha kuipeleka kwa nchi ambayo Olimpiki itafanyika, inawaka hadi michezo itakapomalizika, kisha inazimwa, michezo ya Olimpiki hufanyika katika msimu wa majira ya baridi na majira ya joto.
Tanzania imekuwa ikishiriki kwenye michezo ya majira ya joto tangu mwaka 1964 iliposhiriki kwa mara ya kwanza ikiwakilishwa na timu ya wanariadha wa mbio za kati na ndefu
“Naikumbuka ile safari, tuliweka kambi jijini Dar es Salaam, mimi nilikuwa mwalimu, hivyo nilichukuliwa kazini,” anasimulia Daniel Thomas mmoja wa wanariadha wa kwanza kuiwakilisha nchi kwenye Olimpiki.
Thomas sasa amekuwa mtu mzima, anaishi Bunda mkoani Mara, wakati Abdallah inaelezwa alihamia huko Falme za kiarabu na Mfyomi na Dyamwale wametangulia mbele za haki.
Olimpiki ya kwanza Ilikuwa HIVI
“Kocha wetu alikuwa Khalifa Abdallah, tuliweka kambi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati ule kila kitu cha michezo kilikuwa ni nyara za Serikali,” anasimulia Thomas.
Anasema kuanzia suti za michezo, raba za kukimbilia na vifaa vingine vya mazoezi vilikuwa vya Serikali.
“Hata tuliporejea tulitakiwa kuvirudisha,” anasimulia mwanariadha huyo ambaye katika Olimpiki alichuana kwenye mbio za mita 400 na kutumia sekunde 50.4.
Mfyomi alikuwa mwanariadha wa mbio za mita 10,000 na Abdallah alikimbia marathoni na kumaliza wa 47 akitumia saa 2:40:06 kwenye michezo hiyo iliyofanyika Tokyo huku Dyamwale akikimbia mbio za mita 800 na kutumia dakika 1:54:09.
“Mimi na Dywamwale nakumbuka hatukufuzu hatua inayofuata, mimi nilimaliza wa sita katika mchujo, na hiyo ilichangiwa na ushamba wa mashindano,” anasema.
Thomas anasema wakati huo wao walizoea kukimbia pekupeku, hivyo kufika kwenye Olimpiki, hakukuwa na utaratibu wa kutokuvaa raba za kukimbilia.
“Nililazimishwa kuvaa kabla ya mbio kuanza, nilihisi raba zinaniumiza miguu, nikazivua kisirisiri, lakini nilionekana na kutakiwa nivae, hicho ndicho kiliniathiri,” anasimulia.
Anasema ushamba mwingine wa timu ya Tanganyika ilikuwa ni kwenye vyakula.
“Tulishindwa kuelewana lugha, hivyo tulipohitaji nyama tulibuni mbinu ya kulia kama mnyama halisi anavyolia, kama tulitaka nyama ya ng’ombe basi tulilia kama mnyama huyo na walituelewa,” anasema.
Licha ya kutorejea na medali, Thomas anasema waliporejea nchini walipokewa kwa hamasa na Rais Nyerere.
“Nakumbuka ndiye alinifanya niwe staa, kitendo cha kutupokea na kutupongeza kwa kutupa mkono ilikuwa ni cha kishujaa kwetu, ilikuwa ni gumzo mkoani Mara nilikozaliwa,” anasimulia.
Kwenye Olimpiki iliyofuata mwaka 1968 kule Mexico, si Dyamwale, Thomas, Mfyomi wala Abdallah waliokuwa kwenye kikosi cha Tanzania, timu ilibadilika na sura mpya zikapata nafasi.
Ilikuwa zamu ya bondia Titus Simba aliyechapwa na Chris Finnegan kwa majaji wote watano raundi ya awali.
Mwanariadha, Norman Chihota aliyekimbia kwa sekunde 10.57 kwenye mita 100 na sekunde 21:28 katika mbio za mita 200 sanjari na Claver Kamanya aliyetinga nusu fainali ya mbio za mita mita 400 akitumia sekunde 46.22 ndiyo walifanya vizuri japo hawakufuzu kwenye fainali.
Mwaka huo, ikitambulika kama timu ya Tanzania, mwanariadha John Stephen Akhwari aliweka historia ya kukimbia kwa saa 3:25:17 kwenye marathoni na kumaliza wa 57.
ITAENDELEA....