Ronaldo waache waoane... alikuwa na hawa pia
Muktasari:
- Lakini, kinachoeleweka ni kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 42 aliwahi kuhusishwa kuwa katika mahusiano na wanawake mbalimbali maarufu kabla ya kuanzisha familia na mrembo aliye naye.
LISBON, URENOI: SUPASTAA wa soka duniani, Cristiano Ronaldo, anaripotiwa kuwa huenda akafunga ndoa na mchumba wake wa muda mrefu, Georgina Rodriguez.
Lakini, kinachoeleweka ni kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 42 aliwahi kuhusishwa kuwa katika mahusiano na wanawake mbalimbali maarufu kabla ya kuanzisha familia na mrembo aliye naye.
Miongoni mwa wanawake waliowahi kuhusishwa naye ni Paris Hilton, Kim Kardashian, mwanamitindo Irina Shayk, pamoja na mastaa wengi wengine wanaojihusisha na tasnia ya burudani.
Tangu 2016, Ronaldo amekuwa kwenye uhusiano thabiti na Georgina Rodriguez, mwenye umri wa miaka 32, baada ya wawili hao kukutana katika duka la Gucci mjini Madrid, Hispania wakati nyota huyo akiichezea Real Madrid.
Kwa sasa wamejenga familia yenye watoto watano ambao ni Cristiano Jr, Mateo, Eva Maria, Alana Martina na Bella Esmeralda.
Agosti mwaka jana, Georgina alitangaza kuwa wamechumbiana na Ronaldo baada ya kuonyesha pete kubwa ya almasi aliyovishwa. Ingawa haijatangazwa tarehe rasmi, lakini taarifa mbalimbali zinaeleza kuwa harusi yao inaweza kufanyika eneo la Quinta da Regaleira, Sintra nchini Ureno. Hawa ni miongoni mwa wanawae ambao Ronaldo maarufu kama CR7 alihusishwa nao kimapenzi na wengi walikiri kuwa wapenzi wake.
IMOGEN THOMAS
Mwaka 2006, Ronaldo alihusishwa na mwanamke aliyekuwa akishiriki wa mashindano ya Big Brother, Imogen Thomas, ambapo inadaiwa wawili hao walikutana wakati CR7 akiwa mchezaji wa Manchester United, na baadaye kuzua uvumi kuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Nyakati hizo kulikuwa pia na taarifa mwaka 2011 zilizodai walirudiana, ingawa zote mbili zilikanushwa na wawili hao.
GEMMA ATKINSON
Mwaka 2007, Ronaldo alianza kuhusishwa na mwigizaji wa Uingereza, Gemma Atkinson. Wawili hao walikutana kwenye mchezo mmoja uliokuwa ukiihusisha Manchester United na timu moja ya London, na walidumu pamoja kwa takribani miezi minne kabla ya kuachana.
Gemma aliwahi kusema Ronaldo alimshawishi kwa kumwalika kunywa chai na kutazama vipindi vya vichekesho vya Kiingereza.
BIPASHA BASU
Baadaye mwaka huo, Ronaldo alionekana akiwa karibu na nyota wa filamu za Bollywood, Bipasha Basu, katika klabu ya usiku mjini Lisbon, Ureno.
Inadaiwa uhusiano wao ulianza kutokana na mapenzi ya Ronaldo kwa filamu za Bollywood.
PARIS HILTON
Mwaka 2009, Ronaldo alihusishwa kutoka kimapenzi na mrithi wa familia ya Hilton, Paris Hilton, baada ya kuonekana pamoja kwa siku kadhaa mjini Los Angeles, Marekani. Uhusiano huo haukudumu kwa muda mrefu, huku Paris akieleza baadaye kuwa walikuwa marafiki wazuri.
KIM KARDASHIAN
Mwaka 2010, Ronaldo pia alihusishwa na nyota wa televisheni na mfanyabiashara, Kim Kardashian, baada ya kuonekana wakila chakula pamoja na kutumia siku kadhaa jijini Madrid wakijirusha katika maeneo tofauti.
Hata hivyo, uhusiano huo uliisha haraka na kila mmoja akaendelea na maisha yake.
IRINA SHAYK
Mwanamitindo wa kimataifa kutoka Urusi, Irina Shayk, ndiye aliyekuwa kwenye uhusiano mrefu zaidi na Ronaldo kabla ya Georgina, mama wa watoto wake. Walidumu pamoja mapenzini kuanzia 2010 hadi 2015 baada ya kukutana kwenye kampeni ya matangazo ya mitindo.
Katika kipindi hicho walionekana mara nyingi kwenye hafla mbalimbali duniani na hata kulikuwa na taarifa kuwa walichumbiana 2011, lakini ndoa haikufanyika.
DESIREE CORDERO
Kabla ya kuanza uhusiano na Georgina 2016, Ronaldo alijihusisha kimapenzi kwa muda mfupi na mwanamitindo wa Hispania, Desiree Cordero, aliyewahi kutwaa taji la Miss Spain 2014. Mahusiano hayo hayakudumu kwa muda mrefu, ambapo taarifa zilidai wawili hao walitengana kutokana na kutofautiana kuhusu malengo ya uhusiano wao.
Baada ya mitihani na pandashuka nyingi Ronaldo alinasa kwa Georgina na kwa sasa wanaendelea kufurahia maisha ya familia na wameonekana wakipumzika pamoja na watoto wao kwenye visiwa mbalimbali vya maraha duniani ikiwamo Mallorca kule Hispania.
Wakati uvumi wa harusi ukiendelea kushika kasi, mashabiki duniani wanasubiri kuona kama wawili hao watafunga rasmi ndoa katika siku zijazo.