RIPOTI MAALUM: Makocha wazawa wanafeli wapi?

KATIKA sehemu ya kwanza ya makala hii kuhusu sababu za ligi zetu nchini kutawalia na makocha wa kigeni huku makocha wazawa wakishindwa sio tu kwenda kusaka ajira na mafanikio nje ya nchi, bali wakipigwa kumbo hata katika klabu za hapa nyumbani. Ungana nasi katika sehemu hii ya mwisho…
MASLAHI
Hili nalo limekuja katika kutafuta ukamilifu wa ripoti hii. Baada ya kuzungumzia elimu, uongozi, uzoefu na uwezo ndipo likaibuka.
Kocha hufanya kazi kwa maslahi mapana yake na familia yake.
Imeelezwa kuwa makocha wengi hawataki kutoka Tanzania kwenda nje kwa kigezo cha maslahi.
Ndani ya miaka ya hivi karibuni soka la Tanzania limeonekana kuwa sehemu inayolipa vizuri, kuliko mataifa yaliyotuzunguka ya Afrika Mashariki na pengine Afrika ya Kati ambapo ndio ingekuwa rahisi kwa makocha wetu kuanzia kuonyesha ubora wao.
Sio Kenya, Burundi, Rwanda wala Uganda wanamichezo (soka) wao kwa sasa wanaitazama Tanzania kama sehemu yenye maslahi mapana kwao na wengi huja kufanya kazi hapa ili kupata kipato cha maana.
Kocha Juma Mwambusi aliyewahi kuzifundisha timu tofauti nchini Tanzania kwa mafanikio zikiwemo Mbeya City na Yanga, aligongelea nyundo katika jambo hili kwa kusema: “Kila mtu anatazama maslahi yake, kwa namna ilivyo sehemu rahisi ya makocha wazawa kutoka nje na kufundisha soka ni ndani ya Afrika Mashariki.”
“Lakini huko unaendaje na kwa maslahi gani? Nakumbuka niliwahi kupata ofa ya moja ya timu za Ligi Kuu nchini Rwanda, lakini sikwenda kutokana na maslahi yao kutoniridhisha,” alisema Mwambusi ambaye kwa sasa amepumzika kufundisha soka akiendelea kujisomea.
Kwa mantiki hiyo, inaonekana kwa upande wa soka hususan makocha kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania ndipo kuna maslahi mapana, hivyo makocha wengi wazawa hawafikirii kuyaacha na kutoka nje kujitangaza kupitia klabu za huko ili kukuza zaidi wasifu wao.
NDOTO NA MALENGO
Hii sio kwa makocha tu, bali hata wachezaji ndoto na malengo katika midomo wazitamkapo ni kubwa, lakini utekelezaji wake huwa wa kawaida.
Kila mchezaji atakuambia ana ndoto ya kucheza soka la kulipwa nje, lakini kiuhalisia haifanyii kazi ndoto hiyo. Vivyo hivyo kwa makocha. Kwa mujibu wa mmoja wa makocha wazoefu wa soka la Tanzania anaeleza kuwa makocha wengi wazawa ndoto na malengo yao ni ya muda mfupi na wengine hufundisha mpira kwa mazowea.
“Ukiingia sana huku ndio utajua namna tunavyoishi. Wengi wetu hatuna ndoto za kufundisha soka Real Madrid au Barcelona, tunazitaka hizi Simba na Yanga tu,” anasema kocha huyo na kuongeza:
“Mbaya zaidi na hizo Simba na Yanga hatuzipati na hapo ndipo malengo yanapotea tunabaki kupishana kwenye hizi timu za kawaida kwa mazowea.”
Kocha huyo anaongeza kuwa: “Kingine kinachoua ndoto na malengo yetu ni tamaa tu. Unaweza kuwa unatamani msimu huu umalize kwenye nafasi tano za juu na timu ya kawaida ili utengeneze CV yako kwa ajili ya biashara, lakini kesho ukipata ofa ya timu nyingine iliyoongeza laki (moja) kwenye mshahara wako unaondoka na kuua malengo yako. Hivyo ndivyo inakua kwa walio wengi wetu.” Kocha huyo anafundisha timu ya Ligi Kuu Bara hadi sasa.
Pia kocha mwingine aliyezungumza na Mwanaspoti anaeleza kuwa kila mmoja huwa na ndoto kubwa na malengo, lakini yote hayo kadri siku zinvyozidi kwenda hufifia kutokana na mazingira ya kazi yalivyo.
MSIKIE MWAISABULA
Mdau wa soka ambaye pia ni miongoni mwa makocha wenye elimu kubwa, Kenny Mwaisabula anafunguka kuwa makocha wazawa uwezo walionao ni mkubwa, lakini wanaangushwa na uongozi ambao hautaki kuwaamini.
“Kaka kuna mazingira ambayo mzawa anatengenezewa hawezi kuonekana bora, mfano timu hizi za Dar es Salaam akipewa kocha mzawa anakuwa chini ya kauli za mabosi.
“Pia kuanzia vitendea kazi mfano mipira, koni na viwanja atapangiwa tofauti na ilivyo kwa wageni,” anasema Mwaisabula.
“Mzawa atahitaji mipira 30 (ya kufanyia mazoezi katika timu), lakini hapewi, ila akija mgeni haraka tu atapewa kila kitu anachohitaji, hivyo mazingira hayo ndiyo hufanya wazawa wengi wasifanye vizuri na wengi wao hukata tamaa, lakini ukianza kuhesabu rekodi za wazawa na wageni utaona kuwa wazawa wamefanya ma-kubwa zaidi lakini watu hawae-lewi.”
KIGOGO TAFCA
Hata hivyo, aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Makocha Tanzania, (Tafca), Michael Bundala anawatetea makocha wazawa akitaka wapewe imani ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo kwa maslahi mapana ya timu wanazozifundisha na taifa kwa ujumla.
“Ujue wazawa wenyewe wanakata tamaa kutokana na kutoaminiwa kuanzia kwa wenye timu hadi mashabiki wa soka letu hawawaamini wazawa. Hii inafanya wao kukata tamaa kwa mapambano yao, lakini sio kwamba hawana uwezo mkubwa,” anasema Bundala.
“Kwani kina Kayuni waliwezaje na hawa wa sasa wanashindwa wapi?” Hata hivyo bosi huyo wa zamani wa Tafca anasema: “ Kikubwa ni kuwapa imani na naamini watafanya vizuri ndani na nje ya Tanzania.”
Katika Ligi Kuu Bara kwa sasa timu sita zina makocha wazawa, huku 10 zikiwa chini ya makocha wa kigeni. Kati ya hizo ni Polisi Tanzania ndio iliyo nafasi ya juu zaidi nane ikiwa chini ya kocha mzawa, Malale Hamsini.