Prime
Remontada feki tunazisubiri Anfield, Allianz Arena
SOMETIMES in April. Wakati Fulani Aprili mwaka jana. Huku Afrika tukiwa tunanyeshewa na mvua ghafla likaja neno Remontada. Neno la Kihispaniola lenye maana ya kisasi. Malipizo.
Mwaka jana Aprili, Arsenal waliapizwa wangekiona cha moto pale Santiago Bernabeu. Kwamba wangekumbana na Remontada kule Hispania. Pale London Arsenal walikuwa wamepiga mipira miwili ya faulo ya Declan Rice na yote ikaingia katika nyavu za Thibaut Courtois.
Tukaapizwa wangekiona cha moto Santiago Bernabeu. Remontada ingefanya kazi. Tukasubiri wiki ikapita Arsenal wakapanda ndege kutoka Heathrow kwenda Uwanja wa Barajas pale Madrid. Siku ya Remontada ilipofika Arsenal ikashinda tena mabao 2-1. Hakukuwa na remontada wala ndugu yake remontada.
Nimekumbuka mbali. Wale wote wanaomini zaidi historia kuliko hali halisi. Kuna watu wanaamini kuna viwanja vimekuwa maalumu kwa ajili ya mashindano fulani. Kwamba ni viwanja vigumu.
Kwamba kuna timu zimekuwa maalumu kwa ajili ya michuano fulani. Real Madrid na Liverpool huwa zinawekwa katika daraja hilo. Ni kweli wametwaa taji mara nyingi lakini moja kati ya sababu ya kutwaa mara nyingi ni ubora wao pamoja na udhaifu wa wapinzani.
Wiki ijayo tutasubiri remontada nyingine feki kutoka kwa hawa mabwana mawili. Liverpool watakuwa nyumbani wakiwasubiri PSG ya Ufaransa. Ulitazama mechi ya kwanza? PSG wangeweza kuondoka uwanjani na ushindi wa mabao zaidi ya matano. Ni vile tu walizembea.
Real Madrid pia walikuwa Santiago Bernabeu katika usiku mwingine wa Ulaya. Wakachezea kichapo cha mabao 1-2 huku mwamuzi wa mechi akiwanyima Bayern penalti ya wazi. Ingeweza kuwa mabao 1-3.
Na sasa tunawasubiri Liverpool wakiwa nyumbani kuikaribisha PSG. Unadhani kutakuwa na maajabu? Yanahitajika zaidi ya maajabu kwa namna Liverpool wanavyocheza. Kwa sababu ya ulinzi ya rafiki zetu Ibrahim Konate na Virgil van Dijik ambaye umri umemkamata basi tunasubiri zaidi ya remontada.
Mo Salah miguu yake imechokwa. Aliwekwa benchi katika pambano dhidi ya PSG na usingeweza kumlaumu Kocha Arne Slot. Tatizo kubwa ni Slot mwenyewe anashindwa kuhalalisha maamuzi yake ya kumuweka Salah nje. Hata akimweka Salah nje timu yake haifanyi chochote cha maana. Hata akimpanga Salah timu yenyewe haionyeshi chochote cha maana.
Unafikia kupata jibu tu Salah amechoka, Liverpool imechoka na Slot mwenyewe amechoka. Kwa sasa hakuna suluhisho. Salah akipangwa sawa, akikaa nje sawa. Salah hapaswi kulalamika lakini hata wanaomtetea wanaweza kufanya hivyo kwa sababu Slot naye hakuna anachohalalisha kwa Salah kukaa nje.
Halafu kuna ndugu zangu Real Madrid. Msimu uliopita hadi msimu huu mapungufu yao yapo pale pale. Kwa wataalamu wanaotandika mikeka watakwambia timu haina hata maajabu. Huwa wanafungwa kirahisi tu na kina Osasuna kule Hispania.
Ni vile tu Barcelona anayeongoza ligi naye huwa anashindwa kukaza vinginevyo angeweza kuwa anaongoza ligi kwa zaidi ya pointi 10 sasa hivi. Ni vile na kocha, Hans Flick naye anajifanya timu yake inaweza mtego wa juu wa kuotea. Anapitika kirahisi na anafungika kirahisi.
Kwa wanaoifuatilia Bayern Munich kule Ujerumani na wanaoifuatilia Real Madrid kule Hispania ungeweza kuhisi matokeo yanaweza kuwa vipi kabla hata ya mechi. Popote pale ambako pambano lao lingechezwa Bayern walikuwa katika nafasi nzuri ya kumchapa Real Madrid.
Msimu uliopita Madrid walipaswa kuifanya remontada dhidi ya Arsenal katika uwanja wa nyumbani Santiago Bernabeu, lakini safari hii wanalazimika kuifanya remontada katika uwanja wa Allianz Arena.
Bayern wakiwa kwao nao huwa wanakuwa watu wengine. Allianz Arena imejaa bender ana mashabiki wenye hisia. Madrid kazi wanayo. Wangeweza kufanya mapinduzi kama wangekuwa na timu. Hapana. Kwa sasa hawana timu. Wana wachezaji mastaa wakiongozwa na Kylian Mbappe na Vinicius Junior. Wapo wengine pia kina Jude Bellingham lakini mpira wa kisasa ni mchezo wa timu kuliko wachezaji.
Tupunguze kuzizungumzia baadhi ya timu zinaweza kufanya lolote muda wowote kama vile wanahodhi michuano yenyewe. Hizi Madrid na Liverpool zina uwezo mkubwa wa kufanya lolote pale tu wanapokuwa na wachezaji wazuri waliotengeneza timu bora.
Sio kila msimu wana uwezo wa kufanya lolote mahala popote. Kama tulivyoshuhudia msimu uliopita Madrid ilitolewa na Arsenal ndivyo inavyokuwa hivyo hivyo katika misimu mingi tu ambayo hawajiandai vema. Kama adui akiachana na habari ya kuogopa jina akacheza soka lake maridhawa basi ana uwezo wa kushinda popote kama Arsenal alivyoonyesha msimu uliopita na namna ambavyo Bayern Munich anakaribia kutuonyesha msimu huu.
Na kwa ndugu zangu Liverpool nadhani hata wenyewe wanajua hawapo katika hadhi ya kutwaa ubingwa wa Ulaya. Sidhani kama wanajiongopea kitu. Shabiki wao moja majuzi aliniuliza wamefikajefikaje katika hatua hii ya michuano hii.
Kwa mara nyingine tena tumelazimishwa kusubiri remontada za wakubwa wetu wa Ulaya. Kina Real Madrid na Liverpool. Hata hivyo sioni dalili zozote za remontada. Mpira unachezwa hadharani.
Liverpool ya Roberto Firmino, Sadio Mane na Mo Salah aliyekamilika ningeweza kuhisi harufu ya remontada. Ningeweza kuhisi kwamba labda walikuwa wameotewa kwa Bahati mbaya. Kwa Liverpool hii ya Konate na VVD waliochoka sidhani kama akina Vitinha watafanya makosa ya kuruhusu remontada ya kijinga.
Ni sawa kwa wale jamaa zangu wa Bernabeu. Wanapitika sana. Wanapitika kirahisi. Nahisi Bayern Munich wataendelea pale pale ambapo Arsenal waliishia. Mpaka Madrid na Liverpool watengeneze timu za uhakika ndipo neno remontada litakapopata maana. Kwa sasa ni kudanganyana tu.