Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rekodi ilivyovunja rekodi

KWA kawaida rekodi ya michezo ikiwekwa kinachosubiriwa ni kuvunjwa na kuwekwa nyingine.

Kwa mfano rekodi ya dunia ya Pele (Edson Arantes do Nascimento) wa Brazil katika kandanda ya kufunga mabao 767 katika mechi rasmi za kimashindano ilidumu kwa zaidi ya miaka 40 hadi mwezi uliopita ilipovunjwa na Cristiano Ronaldo wa Ureno alipopiga hat-trick na kufikikisha mabao 770.

Hii imesababisha rekodi kongwe kabisa ya dunia iliyodumu muda mrefu ni ya mbio za mita 400 kwa wanawake iliyowekwa na Marita Kocha wa Ujerumani miaka 34 iliyopita.

Mwanamama huyu ambaye wakati ule aliiwakilisha iliyokuwa Ujerumani Mashariki (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani) alikimbia masafa hayo kwa muda wa sekunde 47.60 katika mashindano yaliyofanyika Canberra nchini Australlia.

Namna alivyokimbia ilishangaza wengi na mbio zile zilifanyiwa filamu fupi ya sinema iliyoitwa ‘Chui wa Ujerumani’

Rekodi ya Tanzania kwa mbio hizi inashikiliwa na Claver Kamanya aliyekimbia kwa sekunde 45.74 nchini Mexico katika michezo ya Olimpiki Oktoba 16, 1968.

Rekodi ya taifa ya mbio hizi kwa wanawake ni sekunde 54.99 iliyowekwa na Leticia Athanas tarehe Agosti 7, 1987 katika michezo ya Afrika iliyofanyika jijini Nairobi, Kenya.

Kama walivyo Watanzania wanavyoisubiri siku ya kuvunjwa rekodi ya Kamanya na ya Leticia, hivyo ndivyo ulimwengu unavyosubiri kuona kila yakifanyika mashindano ya kimataifa ya mbio hizi. Katika miaka ya karibuni yalikuwepo matumaini kwa rekodi ya Marita kuvunjwa na Salwa Eid Naser wa Bahrain ambaye polepole alikuwa anakimbia kwa kasi zaidi baada ya kila mashindano.

Mwanadada huyo mwenye miaka 23 aliyezaliwa Nigeria na jina lake la asili ni Ebelechukweu Aqbapounwu, amekuwa akijitahidi bila ya mafanikio kuvunja rekodi hiyo.

Mnamo Oktoba 3, 2019, Salwa alikuwa bingwa mdogo kabisa wa dunia wa mbio hizo katika mashindano yaliyofanyika jijini Doha nchini Qatar.

Alikimbia kwa sekunde 48.14 na kupunguza sekunde 0.94 ya muda mzuri kabisa aliowahi kukimbia mbio hizo.

Muda huo ndio ulikuwa wa kasi zaidi wa mwanamke kwa mbio hizo tangu 1985.

Mwanamke mwingine aliyewahi kukaribia rekodi ya huyo mwanamama wa Ujerumani ni Jarmila Karatochvilova wa Czech aliyekimbia kwa sekunde 47.99 mwaka 1983 wakati akiwa na miaka 31.

Hadi sasa Marita amejikusanyia rekodi za dunia 16 katika mbio za masafa mafupi kuruka vihunzi na mbio nyingine.

Tangu alipokuwa mdogo aliwashagaza watu kwa kuwashinda watoto wa kiume waliomzidi umri aliposhiriki mashindano ya shule na mitaani.

Alipotimiza miaka 15 alikwenda Rostock kuchukua mafunzo ya udaktari na kutokana na kubanwa na masomo aliacha kushiriki mashindano ya riadha.

Lakini baada ya masomo alirudi uwanjani na kujipatia umaarufu kwa kasi ya kukimbia mita 100, 200 na 400.

Aliweka rekodi ya kwanza ya dunia aliposhinda mbio za mita 400 zilizofanyika Milan, Italia, 1977 akitumia sekunde 51.8.

Mwaka uliofuata alikimbia masafa hayo kwa sekunde 49.19 na kuweka rekodi mbili za dunia katika kipindi cha mwezi mmoja.

Katika mwaka 1979 alikuwa mwanamke wa kwanza kukimbia mita 200 kwa muda wa chini ya sekunde 22 alipotumia sekunde 21.71 na rekodi hiyo ilidumu kwa miaka tisa.

Katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Moscow, Urusi mwaka 1980, Marita alinyakua medali ya dhahabu ya mita 400. Vilevile alishinda mbio hizo katika mashindano ya Bara la Ulaya miaka ya 1978, 1982 na 1980.

Baada ya hapo aliendelea kuchukua rekodi za dunia ikiwa ni pamoja na katika mbio za kupokezana vijiti.

Rekodi zake zote hizo nyingine zilivunjwa katika miongo mitatu iliyopita, lakini siyo ya mita 400.

Mwanamama huyo ambaye alipewa tuzo nyingi na nishani na nchi yake na nyingine alistaafu riadha 1987 na kutambuliwa kama mmoja wa wanariadha wa Ujerumani aliyepata mafanikio makubwa.

Mafanikio yake kama ya wanariadha wengine wa Ujerumani ya Mashariki ya zamani yalighubikwa na shutuma za huenda alitumia dawa za kuongeza nguvu.

Hata hivyo, kila alipopimwa wakati wa mazoezi, kabla ya mashindano na baadaye hata akiwa nyumbani kwake hakuonekana na dalili ya kutumia dawa hizo na ndio maana rekodi yake inatambuliwa hadi leo.

Mwanamama huyo ambaye hivi sasa ana miaka 58 hapendi kufanya mahojiano na vyombo vya habari kwa maelezo kwamba alizungumza sana alipokuwa kijana wakati alipokuwa anakimbia na sasa anataka kupumzika.

“Kama mnataka kujua zaidi juu ya hayo madai ya kutumia dawa za kuongeza nguvu za kukimbia waulizeni hao walionipima zaidi ya mara 30,” alisema katika mahojiano ya miaka michache iliyopita na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Katika mahojiano hayo alisema, “mafanikio yangu yalitokana na kujituma katika mazoezi na mashindano. Najua rekodi yangu ya mita 400 imeushangaza ulimwengu siku za nyuma na hivi sasa, lakini vuteni subira kwani huenda atayefanikiwa kuivunja ameshazaliwa na sasa yupo anajitayarisha kuivunja.”

Miaka 34 imepita na rekodi ya mama huyo imeganda. Jibu la ni nani ataibandua na kubandika nyingine na hii itatokea lini, ni muda ndio utaotoa jawabu sahihi siku za mbeleni.

Lakini kwa sasa rekodi hii imeganda na wa kuibandua na kuweka nyingine hajapatikana, na kwa sasa hakuna ishara ya hilo kutokea hasa wakati huu ambapo janga la Covid 19 limepoza mashindano ya kimataifa ya riadha.