Redondo: Vipaji vinapotea, agoma kutundika daruga
Muktasari:
- Redondo amesema kwa sasa ameamua kupumzika na kujiendeleza kielimu, huku akiandaa akademia itakayosaidia kuibua na kukuza nyota wapya wa Tanzania.
KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Simba, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, amesema vipaji vya wanasoka wazawa vinapotea kutokana na kukosekana kwa vituo vya kulea na kukuza vipaji, huku akisisitiza kuwa hajafikiria kustaafu soka licha ya kukaa nje ya ushindani kwa zaidi ya misimu miwili.
Redondo amesema kwa sasa ameamua kupumzika na kujiendeleza kielimu, huku akiandaa akademia itakayosaidia kuibua na kukuza nyota wapya wa Tanzania.
Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalumu, kiungo huyo amesema hajaridhishwa na mwenendo wa soka la wazawa katika miaka ya karibuni, akilinganisha hali ya sasa na kipindi alichokuwa akicheza, ambacho wachezaji wa Tanzania walikuwa na nafasi kubwa katika vikosi vya klabu.
“Nasikitika sana vipaji vinapotea. Hatuna vituo vya kulea na kukuza vijana kwa ajili ya maisha yao na Taifa kwa ujumla. Tunaendekeza sana wachezaji wa kigeni. Si jambo baya kwa sababu wanatupa kitu, ila inahitaji juhudi,” amesema.
Ameongeza: “Haiwezekani kila siku wachezaji bora wanatoka nje kwenye ligi yetu na wanalipwa vizuri. Ndiyo maana nimeamua kupumzika kwa muda, nitengeneze kitu kwa faida ya Taifa letu baadaye.”
Redondo amesema baada ya kuondoka Polisi Tanzania, ambayo ilikuwa klabu yake ya mwisho kucheza soka la ushindani, ameamua kutulia Magomeni, Dar es Salaam, akiendelea na mipango ya kukuza vipaji.
Akikumbuka enzi zake akiwa Simba, amesema wachezaji wazawa walitawala kikosi, huku akiwataja Emmanuel Okwi na Joseph Owino kuwa miongoni mwa nyota wa kigeni waliokuwa wamepenya katika timu hiyo.
“Miaka hiyo Mussa Mgosi ndiye mfungaji bora, kikosi tunakitawala sisi wazawa. Kukutana na timu za Mtibwa Sugar na Coastal Union kinawaka sana. Kwa sasa kuna mabadiliko makubwa,” amesema.
Ameshauri kurejeshwa na kuongezwa kwa vituo vya kukuza vipaji ili Tanzania izalishe nyota wengine kama Mbwana Samatta, yeye mwenyewe, Ibrahim Ajibu na John Bocco.
SISTAAFU HADI MESSI, RONALDO WATUNDIKE DARUGA
Licha ya kuwa nje ya soka la ushindani kwa muda, Redondo amesema hana mpango wa kutangaza kustaafu hadi Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, ambao amekuwa akiwashuhudia katika safari yake ya soka, watakapostaafu.
Amesema kwa sasa anaandaa programu maalumu kwa wachezaji wanaocheza nafasi ya kiungo, itakayowasaidia kuboresha uwezo wao na kuwa bora zaidi uwanjani.
“Nimeanza mpira nikiwaona kina Messi na Ronaldo, na ndiyo walikuwa wameanza kuwa mastaa. Wenyewe hawajastaafu, inakuaje mimi nitangulie? Wenyewe ndiyo wenye mpira wao duniani kwa sasa.
“Nitafanya hivyo pale wenye mpira wao watakapotangaza kutundika daruga. Kwa sasa naandaa programu kwa ajili ya wachezaji wa nafasi ya kiungo, kuwafundisha namna ya kuwa bora uwanjani,” amesema.
AWAKUBALI FEI TOTO, NADO, MUDATHIR
Pamoja na kulalamikia kupungua kwa ubora wa wachezaji wazawa, Redondo amewataja Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mudathir Yahya, Idd Nado na Dickson Job kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowakilisha vyema soka la Tanzania kwa sasa.
Amesema uwezo wao unamkumbusha enzi ambazo wachezaji wazawa walikuwa na mchango mkubwa katika timu zao, akisisitiza kuwa wadau na Serikali wanapaswa kushirikiana kuwekeza katika soka la vijana.
“Wanafanya vizuri sana. Yupo pia Dickson Job. Kwa sasa wanawakilisha vyema. Lazima tuamke, kila mmoja awe tayari kusapoti na kupenda vya nyumbani. Tufungue akademia nyingi ili tupate warithi wa baadaye.
“Fikiria miaka ya nyuma hata mimi nimetokea akademia hadi kuwa staa. Ibrahim Ajibu na John Bocco wote tumefundishwa na kulelewa na mpira. Lazima Serikali nayo iwaamshe wadau na wenyewe wajitolee,” amesema.
SAFARI YA SWEDEN, NORWAY
Redondo amesema miongoni mwa matukio asiyoweza kuyasahau ni safari ya kwenda Sweden mwaka 2000 kushiriki mashindano ya soka la vijana akiwa na umri wa miaka 13.
Pia amesema aliishi Norway kwa zaidi ya miaka saba, ambako alipata malezi na mafunzo ya soka, lakini mpango wa kupata uraia wa nchi hiyo haukufanikiwa.
“Siwezi kusahau tukio la kwenda Sweden. Fikiria nilikuwa na miaka 13, lakini nilichaguliwa kwenda kushiriki mashindano ya kombe la dunia nikiwa na mastaa wengine wa Ulaya.
“Lakini kilichoniuma sana ni kukosa uraia wa Norway, ambapo Serikali iligoma kwa sababu nilikuwa bado mdogo, lakini wenyewe walikuwa tayari kunipa uraia kwa kuwa walikubali uwezo na tabia zangu,” amesema.
NZENGELI AMKOSHA
Redondo amesema winga wa Yanga, Maxi Nzengeli, ni miongoni mwa wachezaji anaowakubali kutokana na uwezo wake wa kuisaidia timu hata anapokuwa hajafikia kiwango chake cha juu.
“Mchezaji lazima uwe na kitu cha ziada uwanjani pale unapopewa nafasi. Ndicho Nzengeli anachofanya. Akishuka kiwango, hakosi cha kusaidia timu yake kufanya vizuri,” amesema.
AIKUMBUKA BIASHARA UNITED
Licha ya kucheza klabu mbalimbali, zikiwamo Simba na Azam, Redondo amesema Biashara United na mji wa Musoma vilikuwa miongoni mwa maeneo aliyoyapenda zaidi kutokana na heshima, ukarimu wa watu na mazingira ya maisha.
Amesema Biashara United ilimpa heshima kubwa na kufanikiwa kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu msimu wa 2021/22, matokeo yaliyoiwezesha klabu hiyo kupata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
“Biashara iliniheshimisha sana na ule mji wa Musoma siwezi kuusahau. Watu wakarimu sana, chakula na mazingira nilipenda sana maisha, japokuwa hata timu nyingine kama Simba nilipata maisha mazuri,” amesema.
Hata hivyo, amesema jambo linaloendelea kumuuma ni kukosa kusafiri na timu hiyo kwenda kucheza mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli, baada ya Biashara United kushinda mechi ya kwanza Dar es Salaam kwa mabao 2-0.