Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shanga za kiunoni, pambo lenye ujumbe katika ndoa

Muktasari:

  • Katika baadhi ya jamii, rangi za shanga zimehusishwa na ishara zinazoweza kumsaidia mwanaume kuelewa hali ya mwenza wake, ikiwamo kipindi cha hedhi na utayari wa wanandoa kuwa faragha.

Kwa baadhi ya wanawake, shanga za kiunoni ni mapambo yanayoongeza urembo na mvuto. Hata hivyo, kwa wengine, mapambo hayo yana maana inayozidi urembo, yakitumika kama njia ya kuwasilisha ujumbe kuhusu hali ya mwili na uhusiano wa wanandoa.

Katika baadhi ya jamii, rangi za shanga zimehusishwa na ishara zinazoweza kumsaidia mwanaume kuelewa hali ya mwenza wake, ikiwamo kipindi cha hedhi na utayari wa wanandoa kuwa faragha.

Hata hivyo, maarifa hayo si ya jumla kwa wanawake wote wanaovaa shanga, kwa kuwa maana na matumizi yake hutofautiana kulingana na mila, mafundisho na makubaliano ya wahusika.

Kungwi anayewafunda wanawake wanaojiandaa kuingia katika ndoa, Zainab Ally, akizungumza leo Alhamisi, Oktoba 15, 2026, na Mwananchi kuhusiana na pambo hilo, amesema matumizi ya shanga ni miongoni mwa mila ambazo baadhi ya wanawake hufundishwa kuzitumia kama njia ya mawasiliano ndani ya ndoa.

Zainab anasema katika mafundisho anayotoa kwa baadhi ya wanawake, shanga za rangi nyeupe, nyekundu na nyeusi zina maana maalumu.

“Shanga za kiunoni ni urembo na zipo za aina na rangi mbalimbali, lakini katika mafundisho yetu, rangi hizi tatu zina umuhimu kwa walio kwenye ndoa. Wanandoa wanapofahamu maana ya ishara hizo, zinaweza kuwasaidia kuelewana na kupunguza migogoro inayohusiana na wivu wa mapenzi, kuchepuka na mahusiano ya faragha,” amesema.

RANGI TATU, UJUMBE TOFAUTI

Zainab amesema katika mafundisho yake, rangi hizo hutumiwa kuwasilisha ujumbe kuhusu hali ya mwanamke na utayari wake wa kushiriki faragha na mwenza wake.

Ameeleza kuwa baadhi ya mafundisho hayo yanahusisha rangi nyeusi na ishara za kipindi cha hedhi, huku nyeupe ikihusishwa na usafi na utayari wa kuwa karibu na mwenza. Rangi nyekundu nayo hutumiwa katika mfumo wa ishara unaofundishwa kwa baadhi ya wanandoa.

Amesema uelewa wa ishara hizo unaweza kumsaidia mwanaume kuelewa hali ya mwenza wake na kuepuka migogoro inayoweza kutokea pale mmoja anaposhindwa kueleza anachopitia.

“Watu wengi siku hizi wanavaa shanga kama mapambo bila kufahamu maana zinazohusishwa nazo katika baadhi ya mila. Jambo muhimu ni wanandoa kuelewana na kuwa wazi kuhusu hali zao,” amesema.

Zainab anasisitiza kuwa hedhi ni hali ya kawaida ya mwili wa mwanamke na inapaswa kueleweka na wanandoa wote, badala ya kuwa chanzo cha lawama au kutokuelewana.

Kwa mujibu wake, mawasiliano kuhusu mzunguko wa hedhi na mahitaji ya kila mmoja yanaweza kuwasaidia wanandoa kupanga maisha yao kwa uelewano zaidi, ikiwamo masuala yanayohusu kupata watoto.


WAZAZI WAKUMBUSHWA WAJIBU

Licha ya kutoa mafunzo kwa wanawake wanaojiandaa kuingia katika ndoa, kungwi huyo amesema wazazi na walezi wana nafasi muhimu katika kuwaandaa watoto wao kwa maisha ya ndoa.

Amesema elimu hiyo haipaswi kuishia kwenye mila na desturi pekee, bali inapaswa kuwajengea mabinti uwezo wa kuwasiliana na wenza wao, kuelewa wajibu wa kila mmoja na kutafuta suluhu pale tofauti zinapojitokeza.

“Changamoto ni pale mtu anapoingia kwenye ndoa bila kuelewa namna ya kuwasiliana na mwenza wake kuhusu mahitaji na hali anazopitia. Hapo ndipo mambo madogo yanaweza kugeuka kuwa migogoro,” amesema.

Ameongeza kuwa mafundisho ya ndoa yanapaswa kuzingatia pia heshima, uaminifu na ushirikiano wa wanandoa katika kutekeleza majukumu ya familia.


TEKNOLOJIA NAYO YATAJWA

Katika hatua nyingine, kungwi Zainab anataja mabadiliko ya kijamii na matumizi ya teknolojia za mawasiliano kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuleta changamoto katika baadhi ya uhusiano, kutegemea namna wenza wanavyozitumia.

Amesema wakati wa kuwafunda mabinti, huwakumbusha umuhimu wa kujenga mawasiliano yenye kuheshimiana, kutatua tofauti kwa mazungumzo na kuepuka tabia zinazoweza kuvunja uaminifu.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa kudumu kwa ndoa kunahitaji juhudi za pande zote mbili, badala ya kumtegemea mwanamke pekee kutekeleza majukumu ya kumfurahisha mume.

Zainab amesema amekuwa akitoa mafunzo hayo kwa zaidi ya miaka 15 na amewafunda takribani mabinti 50, akieleza kuwa lengo lake ni kuwasaidia kujiandaa kukabiliana na changamoto za maisha ya ndoa.

Amesema katika mafunzo yake, huwaeleza wanawake umuhimu wa kuwajali wenza wao, kuwahudumia katika masuala ya faragha na kushirikiana katika shughuli za kila siku za familia.


BIASHARA YA SHANGA NAYO YANUFAISHA

Kwa upande wa biashara, Hawa Hussein, mfanyabiashara wa shanga, amesema katika miaka mitano aliyofanya biashara hiyo amebaini kuwa wateja wana mahitaji tofauti kulingana na aina na rangi za shanga wanazopendelea.

Amesema shanga za rangi moja na zile zenye mchanganyiko wa maua au rangi mbalimbali hutofautiana kwa bei, huku baadhi ya wateja wakiagiza kulingana na mapendeleo yao.

“Shanga za rangi hizi tatu zina wateja wake, lakini pia wapo wanaopenda za mchanganyiko. Bei hutegemea aina ya shanga; baadhi huuzwa kati ya Sh1,500 na Sh2,000, huku nyingine zikiuzwa kati ya Sh3,000 na Sh5,000,” amesema.

WAVAAJI WENGINE HAWAZIJUI MAANA HIZO

Christina Petro amesema amekuwa akivaa shanga kwa takribani miaka mitano kama pambo la kumfurahisha mwenza wake, bila kufahamu maana zinazohusishwa na baadhi ya rangi katika mafundisho ya ndoa.

Amesema amekuwa akipendelea shanga zenye mchanganyiko wa rangi mbalimbali, lakini hakuzielewa kama njia ya kuwasilisha ujumbe kuhusu hali ya mwanamke kwa mwenza wake.

“Nimevaa shanga kwa miaka mitano, lakini sikuwa nafahamu maana hizo. Kuna wakati nikiwa kwenye hedhi na kumweleza mwenza wangu kuwa sijisikii vizuri, tumewahi kutofautiana kwa sababu hakuwa ameelewa hali yangu,” amesema.

Christina amesema ipo haja ya jamii kupata elimu itakayosaidia kupunguza migogoro ya ndoa inayotokana na ukosefu wa mawasiliano. Anasema hali hiyo inaweza kuchochea wivu na migogoro ya kimapenzi, ambayo katika baadhi ya matukio husababisha wanawake kupata ulemavu au kupoteza maisha.


WANAUME WAPAZA SAUTI

Daud Sanga, mkazi wa Simike jijini Mbeya, amesema kwa mtazamo wake, baadhi ya wanaume hukumbana na changamoto za uaminifu katika mahusiano, hali inayoweza kuchochea migogoro na kuwafanya baadhi yao kufikiria kutoka nje ya ndoa.

“Tupo wengine tumeoa wake bila kupitia kwenye mafundisho. Wakati ukitaka faragha, anajisikia kusema niko kwenye hedhi ili akunyime, ndipo vurugu zinaanza na migogoro. Lakini elimu ikitolewa kwa walio katika ndoa, itakuwa mwarobaini na suluhisho kubwa,” amesema.