Raundi ya 29, kibabe zaidi Bara
RAUNDI ya 29 ya Ligi Kuu Bara juzi ilifungwa kibabe kwa kushuhudia matokeo ya kushangaza, lakini gumzo likiwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya na Azam Complex, Dar es Salaama wakati vigogo Simba na Yanga vilivyoshangaza, huku Azam FC ikivunja mwiko Mkwakwani, Tanga.
Yanga iliyovaana na Mbeya City, jijini Mbeya ililazimika kupindua meza kwa kufanya comeback ya kibabe ya kutoka nyuma ya mabao 3-0 hadi kutoka sare ya 3-3, wakati Simba iliendelea na operesheni yake ya kuzishusha timu za majeshi kwa kuizamisha Polisi Tanzania kwa mabao 6-1.
Ushindi huo uliifanya Polisi kushuka rasmi daraja ikiifuta Ruvu Shooting walioshushwa pia na Simba wiki kadhaa zilizopita zilipokutana kwenye Uwanja wa Azam Complex na kuchapwa mabao 3-0.
Katika mechi hiyo ya Chamazi, Saido Ntibazonkiza alifanya kufuru kwa kufunga mabao matano pekee yake, huku jingine likiwekwa kimiani na beki Israel Mwenda na kumtibulia rekodi Kocha Mwinyi Zahera anayeinoa Polisi na kushindwa kuiokoa isishushe daraja.
Hat trick ya Saido ilikuwa ni ya pili kwake msimu huu akiwa na Simba, lakini ni ya nane kufungwa kwenye Ligi Kuu Bara, huku akiweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyehusika na mabao mengi hadi sasa akichangia 27, yakiwamo 15 ya kufungwa na asisti 12. Mabao manne na asisti sita alizipata akiwa na Geita Gold kabla ya kunyakuwaliwa na Simba dirisha dogo na kuifungia mabao 11 na asisti sita.
Ukiondoa na utamu wa Chamazi, kule jijini Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine, Yanga iliyoanza na kikosi cha pili kwenye pambano hilo, ilijikuta ikitanguliwa na City kwa mabao 3-0 kabla ya benchi la ufundi kufanya mabadiliko na kuingiza majembe ya maana yaliyoisaidia kupindua meza kibabe.
Mbeya City hadi dakika ya 63 ilikuwa mbele kwa mabao hayo, mawili yakifungwa kipindi cha kwanza na jingine moja la kipindi cha pili na mastaa wake waliamini wameshamaliza kazi kabla ya Yanga kuwabadilishia kibao hasa baada ya kuingia Jesus Moloko, Bernard Morrison, Tuisila Kisinda, Clement Mzize wakitanguliwa na Salum Abubakar 'Sure Boy' aliyechukua nafasi ya Fardi Musa aliyeumia mapema kwenye mchezo huo.
Kama hujui tu ni kwamba mara ya mwisho Yanga kufungwa mabao matatu kwenye ligi ilikuwa Februari 17, 2021 ilipotoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Mtibwa Sugar na kufanya kutimiza siku 554 ndio rekodi hiyo inavunjwa.
Ikumbukukwe Yanga baada ya kutamba kwa muda mrefu bila kufungwa kwenye ligi rekodi hiyo ilivunjwa katika ardhi ya Mbeya ilipochapwa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu katika Uwanja wa Highland Estates Novemba 29 mwaka jana.
Morrison alifunga mara mbili likiwamo la penalti, huku jingine likiwekwa kimiani na Sure Boy, japo Moloko hakumaliza mchezo baada ya kulimwa kadi nyekundu sambamba na Hassan Nassor 'Machezo' baada ya kupigana uwanjani.
Richardson Ng'ondya alifunga mawili na George Sangija aliitangulia City kwenye pambano hilo, ambalo liliwafanya mashabiki wa timu hiyo ya Mbeya kushindwa kuamini baada ya dakika 90.
AZAM NA MWIKO
Huko Mkwakwani, Azam FC ilivunja mwiko wa Coastal Union, ikiwa nyumbani kwao kwa kuwafunga mabao 2-0.
Mabao ya nyota wa kigeni, Idris Mbombo na Prince Dube zilitosha kuipa Azam ushindi humo ambao uliifanya izidi kujikita nafasi ya tatu kwenye msimamo mbele ya Singida Big Stars ambayo ikiwa nyumbani ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting, kwenye Uwanja wa Liti, Singida.
Kwa miaka nane Azam ilikuwa haijawahi kuishinda Coastal nyumbani kwake, tangu ilipoichapa bao 1-0, katika mechi iliyopigwa Machi 22, 2015 na matokeo ya juzi yalikuwa ni faraja kubwa kwa Wauza Mikate hao ambao wanarudi jijini Dar es Salaam kumalizana na Polisi Tanzania katika mechi ya kufungia ligi kesho kabla ya kurudi tena Mkwakwani kuisubiri Yanga katika fainali ya ASFC.
GEITA NYANYA
Geita Gold iliyokuwa na mwenendo mzuri kwenye Ligi juzi iliendelea kuwa urojo kwa kufungwa mechi tatu mfululizo, ikianza kulala nyumbani mbele ya Tanzania Prisons, Mbeya City na juzi kulala ugenini mbele ya wanambeya wengine, Ihefu iliyowanyoosha mabao 3-1.
Vipigo hivyo vinaelezwa vimezidi kuwatibua mabosi wa Geita juu ya kutaka kuendelea kufanya kazi na kocha Fred Felix 'Minziro' ambaye walimrudisha hivi karibuni baada ya kumchunia kwa muda wakihisi kama amezingua flani kwenye mechi za Nyankumbu zilizohitimisha rekodi ya kutofungwa tangu ilipopanda daraja misimu miwili iliyopita.
Mabao ya Yacouba Songne, Rafael Daud na Rashid Juma yalizidi kuiumiza Geita iliyoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu na kutolewa raundi ya kwanza na Wasudan, licha kupata bao a kufutia machozi kupitia beki wake, Amos Charles Kadikilo.
Katika mechi nyingine za kukamilisha raundi hiyo ya 29, Mtibwa Sugar iliinyoa Kagera Sugar ilifumuliwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, huku Tanzania Prisons ikijiweka pazuri kwenye janga la kuangukia kwenye play-off kwa kuikandamiza KMC kwa bao 1-0.
Kipigo hicho kilichopatikana kwenye pambano lililopigwa Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga, Rukwa kimeiachia msala KMC kusubiri majaliwa yao kwenye mechi ya mwisho kesho itakapovaana na Mbeya City ili kuona ikakwenda kucheza play-off ili kuepuka kushuka daraja.
Namungo nayo ikiwa nyumbani mjini Ruangwa, Lindi ilichapwa bao 1-0 na Dodoma Jiji na kuwapa nafuu wageni katika kuepuka presha za kushuka daraja kwani pointi ilizokusanya zimewaiacha salama kwa sasa, japo inasikilizia matokeo ya mechi za mwisho wa ligi hiyo kesho Ijumaa.
Ukiondoa presha za timu zilizopo kwenye nafasi mbaya ya kuangukia kwenye play-off ili zisizifuate Polisi na Ruvu Shooting katika Ligi ya Championship, kwenye mbio za ufungaji mabao vita imeanza upya baada ya Saido kubakisha bao moja tu kumfikia Fiston Mayele wa Yanga aliyekaa kileleni mwa muda mrefu na mabao yake 16. Mayele hakusafiri na timu kwenda Mbeya na kukosa mechi ya juzi dhidi ya Mbeya, ingawa inaelezwa jana alikuwa njiani kwenda kuifuata Tanzania Prisons.
Misimu miwili iliyopita ilishuhudiwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara anapatikana kwenye mechi za mwisho, ikiwamo ile ya 2020-2021 wakati John Bocco alipompiku Chris Mugalu kwa kufunga mabao 16, moja zaidi ya aliyokuwa nayo mchezaji mwenzake huyo walipokuwa wote Simba.
Msimu uliopita George Mpole aliyekuwa Geita alimpiku Mayele kwa kufikisha mabao 17, moja zaidi na aliyomaliza nayo Mayele ambaye kama atachemsha mechi ya kesho dhidi ya Prisons kisha Saido anatumia tena kwa fujo mbele ya Coastal kama alivtyofanya juzi kwa Polisi basi tuzo inaweza kutua Msimbazi kwa msimu wa tano kati ya sita mfululizo iliyopita. Marav ya mwisho kwa Yanga kutoa Mfungaji Bora ilikuwa 2017-2018 wakati Simon Msuva alipofungana mabao na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting na tangu hapo, tuzo hiyo mara nne imetua Msimbazi a moja Geita. Tusubiri!