Rangi za nguo za wanaume weusi
Muktasari:
- Ukweli ni kwamba, wanaume wenye ngozi nyeusi wana bahati ya kupendeza kwenye rangi nyingi. Kinachohitajika ni kujua zipi zinakufanya uonekane nadhifu, mwenye mvuto na mwenye kujiamini kila unapovaa.
Jamani, kuna wanaume wanavaa nguo bila kujali rangi inawapendeza au la. Mwishowe nguo nzuri zinaonekana hazina mvuto kwa sababu tu rangi haikuwafaa.
Ukweli ni kwamba, wanaume wenye ngozi nyeusi wana bahati ya kupendeza kwenye rangi nyingi. Kinachohitajika ni kujua zipi zinakufanya uonekane nadhifu, mwenye mvuto na mwenye kujiamini kila unapovaa.
Ukichagua rangi sahihi, hata nguo ya bei ya kawaida inaweza kukufanya uonekane wa kiwango cha juu. Hizi ni baadhi ya rangi ambazo huwapendeza sana wanaume wenye ngozi nyeusi.
DAKI BLUU
Bluu kole ni rangi inayowapendeza wanaume wengi wenye ngozi nyeusi. Ukiivaa utaonekana nadhifu na mwenye kujiamini. Inafaa kwa shati, fulana, suti au suruali. Kwa mwanaume anayependa kuonekana smart bila kupiga kelele, daki bluu ni chaguo sahihi. Unaweza kuivaa kazini, kwenye kikao, ibadani au hata ukienda kwenye mtoko wa wikiendi. Ukiichanganya na viatu vyeupe au vya kahawia, muonekano wako unakuwa wa kuvutia zaidi.
NYEUPE
Nguo nyeupe hufanya ngozi nyeusi ionekane safi na yenye mvuto zaidi. Fulana au shati jeupe linaweza kukufanya uonekane smart bila kutumia fedha nyingi. Wanaume wengi huogopa kuvaa nyeupe kwa sababu ya uchafu, lakini ukweli ni kwamba rangi hii huonyesha usafi na mpangilio. Ukivaa shati jeupe lililopigwa pasi vizuri, utaonekana mwenye kujitunza na mwenye ladha nzuri ya mavazi.
KIJANI CHA KIJESHI
Rangi hii ni tulivu lakini inapendeza sana. Ukiivaa utaonekana wa kisasa na mwenye ladha nzuri ya kuvaa. Inakwenda vizuri na rangi nyeupe au cream.
Kwa mwanaume anayependa style za kawaida lakini zenye mvuto, kijani cha kijeshi ni rangi nzuri sana. Inaonekana vizuri kwenye mashati, fulana, jaketi na hata suruali. Ni rangi inayofaa kwa matembezi, safari au kukutana na marafiki.
MARUNI
Hii ni nyekundu iliyokolea. Huongeza mvuto na kukufanya uonekane tofauti. Inafaa sana kwa shati, fulana au blazer.
Rangi hii humfanya mwanaume aonekane jasiri na mwenye kujiamini. Hata ukivaa shati la maruni na suruali nyeusi au ya daki bluu, utakuwa na muonekano wa kuvutia bila kuonekana umejitahidi sana.
KIJIVU
Kijivu ni rangi rahisi kuvaa. Inaendana na nguo nyingi na hukufanya uonekane msafi na wa kisasa. Unaweza kuivaa kazini au kwenye mtoko.
Kwa mwanaume anayependa simplicity, kijivu ni rangi inayofaa sana. Unaweza kuvaa suti ya kijivu, fulana ya kijivu au hata suruali ya kijivu na ukaendelea kuonekana smart muda wote.
RANGI YA MAZIWA (CREAM)
Rangi hii huonekana za kifahari na zimepoa. Hasa ukivaa shati au suruali ya rangi hii utaonekana nadhifu hasa wakati wa mchana au unapokuwa ofisini.
Kwa wanaume wenye ngozi nyeusi, cream huleta utofauti mzuri sana. Rangi hii huifanya ngozi ionekane yenye afya na huongeza mvuto. Pia ni rangi inayopendwa sana kwenye matukio ya mchana kwa sababu huonekana safi na yenye hadhi.
KAHAWIA
Kahawia ni rangi nzuri sana kwa viatu, mkanda au jaketi. Inapendeza zaidi ukivaa pamoja na daki bluu au cream. Mwanaume anayejua kuvaa viatu vya kahawia na mkanda unaofanana huonekana mwenye kujali muonekano wake. Kahawia pia ni rangi inayodumu kwenye fashion na haitoki kirahisi.
NYEKUNDU ILIYOKOLEA
Usiogope kuvaa nyekundu iliyokolea. Rangi hii hukufanya uonekane kwa urahisi hata ukiwa mbali, lakini ikizidi sana inapoteza mvuto kabisa.
Siri ni kutumia rangi hii kwa kiasi. Unaweza kuvaa fulana, shati au blazer ya nyekundu iliyokolea na ukaichanganya na suruali nyeusi au ya kijivu. Muonekano unakuwa wa kisasa na wenye kuvutia.
BROWN NA CHOCOLATE
Rangi kama camel, tan na chocolate brown pia huwafaa wanaume weusi. Huongeza muonekano wa utulivu kwa sababu ni rangi zilizopoa sana. Rangi hizi zinafaa sana kwa jaketi, makoti na viatu. Zinaonyesha ukomavu na huleta mwonekano wa mwanaume anayejitambua. Pia ni rahisi kuzichanganya na rangi nyingine nyingi.
CHANGANYA RANGI KWA USAHIHI
Usivae rangi nyingi kwa wakati mmoja. Chagua rangi mbili au tatu zinazolingana. Hilo pekee linaweza kukufanya uonekane smart kuliko kuvaa rangi nyingi zinazopingana.
Kwa mfano, unaweza kuvaa shati jeupe na suruali ya daki bluu, au fulana ya cream na suruali ya kahawia. Mchanganyiko mzuri wa rangi humfanya mwanaume aonekane nadhifu na mwenye uelewa wa fashion hata kama nguo zake si za gharama kubwa.