Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Athari za kukosa usingizi kwenye urembo

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya na urembo wamekuwa wakisisitiza kuwa usingizi si mapumziko tu ya mwili, bali ni sehemu muhimu ya mchakato wa mwili kujijenga upya. Muda wa usiku unapofika, mwili huanza kazi ya kurekebisha seli zilizochoka ikiwemo seli za ngozi. Hivyo unapokosa usingizi mara kwa mara, athari zake zinaweza kuonekana moja kwa moja kwenye uso na mwonekano wa nje.

KATIKA harakati za kila siku watu wengi wamekuwa wakitumia fedha nyingi kwenye bidhaa za urembo wakiamini ndiyo njia kuu ya kuboresha mwonekano wa ngozi na sura kwa ujumla. Wengine huwekeza kwenye vipodozi, huduma za ngozi na matibabu mbalimbali, lakini kuna jambo moja rahisi ambalo mara nyingi husahaulika ambalo ni usingizi wa kutosha.

Wataalamu wa afya na urembo wamekuwa wakisisitiza kuwa usingizi si mapumziko tu ya mwili, bali ni sehemu muhimu ya mchakato wa mwili kujijenga upya. Muda wa usiku unapofika, mwili huanza kazi ya kurekebisha seli zilizochoka ikiwemo seli za ngozi. Hivyo unapokosa usingizi mara kwa mara, athari zake zinaweza kuonekana moja kwa moja kwenye uso na mwonekano wa nje.


DALILI YA KWANZA

Moja ya dalili za kwanza za kukosa usingizi ni ngozi kuonekana imechoka. Mtu anaweza kuwa ametumia bidhaa nzuri za urembo lakini bado uso ukaonekana hauna mng’ao wa kawaida. Hii hutokea kwa sababu wakati wa usingizi mwili huongeza mzunguko wa damu kwenye ngozi na kusaidia kurejesha mwonekano wake wa asili. Kukosekana kwa muda wa kutosha wa kupumzika kunaweza kufanya ngozi ionekane kavu, isiyo na uhai na kupoteza mvuto wake.


WEUSI CHINI YA MACHO

Athari nyingine ambayo watu wengi huiona mapema ni kutokea kwa madoa au weusi chini ya macho. Kukosa usingizi huifanya mishipa ya damu chini ya macho ionekane zaidi na kusababisha eneo hilo kuwa na rangi tofauti na sehemu nyingine za uso. Hali hii huongeza mwonekano wa uchovu hata kama mtu hajafanya shughuli nzito.


KUZEEKA MAPEMA

Pia, usingizi mdogo unaweza kuchangia kuonekana kuzeeka mapema. Wakati wa usingizi mwili huzalisha baadhi ya homoni zinazosaidia kurekebisha tishu na kusaidia ngozi kubaki na uimara wake. Mtu anayelala muda mfupi kwa kipindi kirefu anaweza kuanza kuona mikunjo midogo, ngozi kupoteza unyevunyevu na uso kutokuwa na mwonekano wa ujana kwa muda mrefu.


HADI NYWELE

Siyo ngozi pekee inayopata athari. Nywele pia zinaweza kuathirika. Kukosa usingizi kwa muda mrefu kunaweza kuongeza uchovu wa mwili na kuathiri mzunguko wa kawaida wa ukuaji wa nywele. Matokeo yake baadhi ya watu huanza kuona nywele kukosa nguvu, kukatika kirahisi au kuonekana zimepoteza mwonekano wake wa kawaida.


CHANGAMOTO MWONEKANO WA KILA SIKU

Mbali na athari za moja kwa moja kwenye ngozi na nywele, usingizi mdogo unaweza kuathiri hata namna mtu anavyoonekana kwa ujumla. Watu wengi wanaokosa usingizi huonekana hawana nguvu, uso hukosa mng’aro na wakati mwingine hata tabasamu huonekana limepungua. Hii inaweza kuathiri kujiamini na namna mtu anavyojihisi anapokuwa kazini au kwenye shughuli za kijamii.


CHANZO CHA MAWAZO

Mbali na hilo, usingizi mdogo unaweza kuongeza kiwango cha msongo wa mawazo. Hali hii huweza kuathiri moja kwa moja afya ya ngozi kwa kuongeza uwezekano wa kupata chunusi au kuwashwa kwa ngozi kwa baadhi ya watu. Ndiyo maana wakati mwingine mtu anaweza kubadilisha bidhaa nyingi za urembo bila kupata matokeo anayotarajia ilhali chanzo kikubwa ni kutopata usingizi wa kutosha.

Kwa upande mwingine, kutolala vizuri kunaweza pia kuchangia maumivu ya kichwa. Maumivu haya yanaweza kumfanya mtu ashindwe kupumzika vizuri zaidi na kuingia kwenye mzunguko unaoendelea wa uchovu na mwonekano usiovutia.


USHAURI

Ili kulinda urembo wa asili, wataalamu hushauri kuweka ratiba nzuri ya kulala kila siku. Kupunguza matumizi ya simu kabla ya kulala, kuepuka vinywaji vyenye msisimko usiku na kutengeneza mazingira mazuri ya usingizi kunaweza kusaidia mwili kupumzika vizuri zaidi. Pia ni muhimu kuhakikisha muda wa kulala unakuwa wa kutosha kila siku badala ya kujaribu kufidia usingizi kwa siku chache.

Urembo hauanzi kwenye chupa ya bidhaa bali huanzia kwenye afya ya mwili. Ngozi yenye mng’ao, macho yenye nguvu na mwonekano wa kuvutia mara nyingi hujengwa na tabia ndogo za kila siku, na usingizi ni moja ya silaha kubwa ambazo wengi huzipuuzia.