PUMZI YA MOTO: Kayoko ‘akurupushwa usiku wa manane’ kuchezesha Ligi Kuu

Muktasari:
- Mungu si Athumani, Alhamisi ya Desemba 12, Ramadhan Kayoko akarudi ulingoni kwa kuchezesha mechi yake ya kwanza baada ya likizo hii ndefu.
TANGU achezeshe mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga, Oktoba 19 mwaka huu, mwamuzi Ramadhan Kayoko ‘alisahaulika’ kwenye viwanja vya Ligi Kuu Bara.
Kukosekana kwake kukazua mijadala mingi, ikiwamo moja ya maandiko ya ukurasa huu wa PUMZI YA MOTO.
Mungu si Athumani, Alhamisi ya Desemba 12, Ramadhan Kayoko akarudi ulingoni kwa kuchezesha mechi yake ya kwanza baada ya likizo hii ndefu.
Ilikuwa mechi ya Singida Black Stars dhidi ya Dodoma Jiji, kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida.
Wenyeji Black Stars, wakashinda 2-1 huku mshambuliaji wa Elvis Rupia akipanda kileleni kwenye msimano wa wafungaji bora, kwa kufikisha mabao 7.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Kayoko kupata nafasi hii ya kurudi uwanjani.
ILIVYOKUWA
Awali, mechi ya Singida Black Stars na Dodoma Jiji ilitakiwa kuchezeshwa na mwamuzi mmoja (jina kapuni) kutoka Tabora.
Lakini siku siku chache kabla ya mchezo huo, mwamuzi huyo akiwa na mmoja wa viongozi wa kamati ya waamuzi, alikutwa na makachero wa TFF akiwa na vigogo wa moja ya klabu zilizotakiwa kucheza mechi hiyo.

Hii ilitoa picha mbaya ikiashiria mchezo mchafu unaendelea kati ya wahusika.
Mawasiliano yakatembea baina ya wakubwa wa mamlaka za soka na waamuzi hao wakabadilishwa na ndipo Kayoko akapewa kazi.
Siku moja kabla ya mchezo Kayoko akasafirishwa na ndege ya usiku, zile ambazo husababisha taa kuzimwa na mechi kusimama pale Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Hivi ndivyo Kayoko ‘alivyorudi kutoka likizo’ iliyoanzia mechi ya watani.
Ni jambo la kuipongeza TFF kwa kusambaza makachero kila kona kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, lakini vipi kuhusu hatua zaidi?

Kayoko amerudi kwa kupitia mlango wa dharura, ni jambo jema lakini vipi yule mwamuzi aliyebadilishwa?
Maana yule mwamuzi wa kati aliyebadilishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Kayoko, akaenda kuwa mwamuzi wa akiba kwenye moja ya mechi za raundi ile.
YAANI SUALA LAKE LIMEISHA KIRAHISI NAMNA HII?
Taarifa za ndani zinasema yule ‘kigogo’ wa kamati ya waamuzi aliyekutwa akiwa na mwamuzi na kiongozi wa moja ya timu ambazo walipaswa kuzichezesha, amesimamishwa lakini kwanini mwamuzi kabaki salama?
TFF isiishie tu kubadilisha waamuzi, iende mbali zaidi. Kabla hajapewa mechi nyingine kwa nafasi yoyote ile, mwamuzi yule alipaswa kuchunguzwa kwa kina huku akiwa nje ya majukumu.
Mpira wetu kwa kadri unavyokua, na matukio yenye viashiria vya michezo michafu yatazidi kuwa mengi na makubwa.
Hivyo kuyakabili pia yapaswa kuchukulia hatua nyingi na kubwa.
Wacheza kamari au ‘wawekezaji wadogo wadogo’ kama wenyewe wanavyojiita, wamekuwa wengi sana, hasa kundi la wachezaji.
Kuna watu ambao kazi yao ni kuwasiliana na wachezaji ili ‘kuweka mikeka yao’.
Mchezaji anakuhakikishia kwamba tutaruhusu bao kwa hiyo weka hela yako kwenye upande wa timu zote zitapata bao.

Mechi ikianza, utashangaa kuna mabao ya ajabu ajabu yanapatikana, halafu mchezo unarudi kawaida.
Unaweza ukadhani yalikuwa makosa ya kibinadamu kwa sababu ‘aliyechomesha’ anabadilika na kuwa makini kwa kucheza kwa kujituma sana katika sehemu yote ya mchezo iliyobaki kumbe kazi yake alishaimaliza.
Kuna mchezaji (jina kapuni) aliibuka kuwa bora sana na kutabiriwa kufika mbali. Lakini sasa hana timu na amejikita huko.
Yeye ndo kamanda mkuu kwa sasa katika vita vya ‘kumpiga mhindi’.
Kama ambavyo inawafuatilia waamuzi na kumnasa yule wa mechi ya Liti, TFF iwafuatilie na hawa wawekezaji wadogo wadogo wakiwamo wachezaji.
Mpira unapokuwa biashara kubwa, kila mmoja angependa kufaidika nao -- yaani kila mmoja angependa kuimega hii keki.
Kuna watakaokuja kuimega kwa kufuata utaratibu na kuna watakaokuja kuimega bila kufuata utaratibu.
Ni jukumu la mamlaka kuhakikisha wote wanafuata utaratibu ili tuwe salama na mchezo wetu pendwa.
Tusipokuwa makini tutaruhusu mpira kuangukia kwenye mikono ya magenge ya wahalifu. Rushwa, kutakatisha pesa chafu na kamari.
Magenge haya hutumia nguvu kubwa ya pesa kutengeneza ushawishi na msipokuwa makini mtashangaa kuona baadhi yao wameingia katika sehemu za uamuzi.
Na hapa inatakiwa mkono mkubwa zaidi kuhusika, nao ni serikali, badala ya TFF peke yao.
Serikali inapaswa kutunga sheria maalumu kwa ajili ya kudhibiti mambo machafu michezoni, ikiwamo upangaji matokeo, badala ya kutegemea tu sheria mama ya kupambana na na rushwa na uhalifu kwa ujumla.
Upangaji matokeo na rushwa michezoni ni sawa ugonjwa sugu unaotakiwa kuwa na dozi maalumu, hauwezi kutibiwa kwa dawa za homa kama homa nyingine.
Kwa hiyo tunatakiwa tuwe na sheria maalumu, kama ambavyo serikali ya awamu ya kwanza ilivyotunga sheria maalumu ya uhujumu uchumi, haikuacha tu uhujumu uchumi usimamiwe na sheria ya kawaida ya uhalifu mwingine.
Magenge ya wahalifu wa michezoni yamekuwa makubwa sana duniani yakiongozwa na Don Tan wa Singapore, ambaye ni kinara duniani katika kuratibu matukio hayo.
REJEA MKASA WA ODDEN MBAGA, JESSE ERASMO NA KHAMIS CHANG’WALU
Juni 5, 2010, waamuzi watatu wa Tanzania; Oden Mbaga, Jesse Erasmo na Khamis Chang’walu, walichezesha mechi ya kirafiki kati ya Bafana Bafana na Denamark, iliyofanyika Afrika Kusini.
Baadaye zikazuka taarifa kwamba waamuzi hao walihusika na upangaji matokeo kwa kushirikiana na Wilson Perumal, gwiji wa upangaji matokeo na rushwa za michezoni, kutoka Singapore.
Mwaka 2014 wakasimamishwa lakini mwaka 2018 Oden Mbaga akafungiwa maisha na FIFA.
Ukiangalia hapa utaona magenge ya wahalifu wa michezo ya Singapore yanahusika yaani Tanzania imekuwa na mawasiliano na magenge ya Singapore tangu mwaka 2010.
Kwa hiyo siyo suala la kuyachukulia kirahisi mambo haya, Don Tan na Wilson Perumal wanaogopwa dunia nzima katika upangaji matokeo.
TFF na serikali ziongeze mbinyo kuhakikisha nchi haugeuki kiwa pepo ya magenge ya wahalifu michezoni kama Singapore.
Na hii huanza kwa hatua kama dhidi ya yule mwamuzi aliyekutwa na viongozi wa moja ya timu ambazo alitakiwa kuzichezesha!